muhtasari

Latest Article Get our latest posts by subscribing this site

BENO,MAGARI YAWAPATA YANGA...


Mwenyekiti wa Yanga Yusuf Manji (kushoto), Afisa Habari - Baraka Kizuguto na Beno Njovu Katibu Mkuu mpya(kulia)




















Mwenyekiti wa Young Africans Yusuf Manji leo amemtambulisha rasmi Bw. Beno Njovu kuwa katibu mkuu mpya wa klabu akichukua nafasi ya Lawrence Mwalusako aliyekua kaimu katibu mkuu kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Akiongea na waandishi wa habari makao makuu ya klabu ya Yanga, Mwenyekiti wa Yanga Bw.Yusuf Manji amesema Beno Njovu anaanza kuitumikia hiyo nafasi mpya kuanzia leo na Mwalusako atakua nae pamoja kwa kipindi cha mwezi mmoja mpaka atakapokabidhi kazi rasmi.

Aidha Manji ametangaza mkutano mkuu wa wanachama Januari 19,2013 ambapo wanachama watapata fursa ya kupitia mapato na matumizi,  na ajenda zingine mbalimbali ambazo zitajadiliwa katika mkutano huo.

Kikao cha kamati ya utendaji kilichoketi mwishoni mwa wiki kimemteua Bw.Seif Ahmed "Magari" kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa na kutokana na nafasi hiyo pia ameteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Utendaji wa klabu ya Yanga. 

Katika mkutano na wandishi wa habari makao makuu ya klabu Manji ametangaza rasmi kutogombea tena uenyekiti katika uchanguzi mkuu ujao, hili nimeliamua mwenyewe binafsi bila shinikizo na kikubwa nimefuata demokrasia.

Nina miezi saba kabla ya uchanguzi mkuu mwakani hivyo sasa ninajitahid kukamlisha shughuli zote ambazo nilianza kuzifanya ndani ya Yanga nikiwa kama mwenyekiti ili uongozi mpya utakaoingia uweze kuendeleza mipango ya kuifanya Yanga iwe klabu bora Tanzania.

Source: youngafricans.co.tz

PICHA: HIVI NDIVYO KILIMANJARO STARS ILIVYOTOKA SARE NA ZAMBIA...


 Timu ya Taifa, kilimanjaro Stars Leo imecheza mechi yake ya kwanza ya CECAFA Challenge Cup  na timu ya Taifa ya Zambia katika mji wa Machakos, ambao uko takriban kilometa 60 kutoka Nairobi. Timu hizo zimefungana 1-1. Kwa ujumla mchezo ulikuwa mkali na wa kusisimua sana, Katika mechi iliyotangulia ambayo iliwakutanisha Burundi NA Somalia, Burundi iliwafunga Somalia goli 2. Yafuatayo ni matukio katika picha
 Hapa vijana wetu wakiwa katika Picha ya Pamoja Kabla ya kwanza kwa kipindi cha kwanza
 Bwana shiyo Pamoja na Gavana wa Machakos wakiwasalimia wachezaji.
 Mtanange ukiendelea uwanja wa Machakos
 Kilimanjaro Stars wakipata dua kabla ya mchezo 
 Kocha wa Zambia akihojiwa na wanahabari
 Mashabiki wa Kilimanjaro Stars wakishangilia timu yao
 Wachezaji wetu wakitoka nje ya uwanja baada ya mchezo huo
 Makocha wa timu zote mbili wakihojiwa baada ya mchezo
Bwana Innocent Shiyo wa tatu  kutoka kushoto wakati wa wimbo Wa Taifa wa Tanzania ukipigwa. kulia kwa Bwana Shiyo ni Balozi  wa Zambia nchini kenya Mh Josephine Mumbi Phiri. Picha kwa Hisani ya Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya

MOTO WA CECAFA KUWAKA KUANZIA LEO JIJINI NAIROBI, STAR vs ZAMBIA…TAKWIMU ZA TIMU ZOTE

Na Baraka Mbolembole

Timu ya Taifa ya Kenya ' Harambee Stars', leo itakata ' utepe' wa
michuano ya Mataifa ya ukanda wa CECAFA, kwa kucheza na timu ya Taifa ya Ethiopia. Wenyeji hao wa michuano ya sasa na makamu bingwa wa taji hilo, wanapewa nafasi kubwa ya kuvuka kundi A, mbele ya Ethiopia,
Zanzibar, na Sudan Kusini.

Mabingwa watetezi, Uganda wao wapo kundi C, pamoja na Rwanda, Sudan, na Eritrea katika kundi linalotarajiwa kuwa gumu zaidi katika michuano hiyo. Moi Kasarani na Nyayo Stadium, ni viwanja viwili vilivyopo
katika jiji la Nairobi, Kisumu Stadium, Mombasa, na Machakos ni idadi
ya viwanja vitano ambavyo vitazipokea timu 12. Mapema leo mchana wawakilishi wengine wa Tanzania, timu ya Zanzibar Heroes itacheza na  Sudan Kusini katika mchezop wa kwanza kabisa mwaka huu.
  KILIMANJARO STARS vs ZAMBIA
Timu ya Taifa ya Tanzania Bara itaanza kibarua chake cha kwanza siku ya kesho, Alhamis kwa kucheza na timu ' alikwa' ya Zambia katika mchezop unaosubiliwa kwa hamu na wapenzi wa soka. Zambia, mabingwa wa michuano ya Mataifa ya Ukanda wa Kusini mwa Afrika, COSAFA, iliifunga Kilimanjaro Stars katika mchezo wa mwisho kukutana katika michuano hii, walipoalikwa kwa michuano iliyofanyika, Dar es Salaam, 2010.
Mbele ya Rais wa Jamhurio ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Stars ilipoteza kwa kulala bao 1-0 siku ya ufunguzi. Disemba mwaka uliopita, Taifa Stars iliifunga timu ya Zambia kwa bao 1-0 katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki huku ' Chipolopolo' wakiwa na nyota wao waliotwaa taji la mataifa ya Afrika, februari, 2012.
  STARS, MATUMAINI YOTE KWA NGASSA
Moja kati ya silaha za hatari katika michuano hiyo ni kiungo mshambuliaji, Mrisho Ngassa. Ni mchezaji ambaye huvuta hisia kubwa za mashabiki hasa timu yake inapokuwa nje ya Tanzania, kasi, ujanja, unyumbulifu, na kucheza kwa kuhaha sehemu kubwa ya uwanja ni sifa ambazo zinampa nafasi ya kipekee kutamba katika michuano hii.
Wakati, kocha wa Stars itambidi asubiri hadi mapema mwezi ujao kupata huduma za washambuliaji wake wawili, kati ya watatu katika safu ya mashambulizi, Mbwana Samatta na Tomas Ulimwengu, ambao watakuwa na mchezo wa marejeano wa fainali ya kombe la shirikisho Afrika, wikiendi hii wakiiwakilisha klabu yao ya TP Mazembe, Kim Poulsen atamtegemea mfungaji huyo bora wa michuano iliyopita nchini Uganda.
Elius Maguli, Juma Luizio, Joseph Kimwaga, na Amri Kiemba wawili kati yao wanataraji kuanza sambamba na Ngassa katika safu ya mashambulizi. Itakuwa ni nafasi nzuri kwao na pengine kijana Said Dilunga anaweza kufanya vizuri zaidi yao kama atapewa nafasi ya kutosha.
Katika nafasi ya kiungo, KIM, bado anao wachezaji ambao wana uwezo na uzoefu wa kutosha, SAlum Abubakary atakuwa akicheza michuano yake ya pili, sambamba na Frank Domayo na wawili hao waliweza kucheza vizuri japo waliambulia nafasi ya nee baada ya kufungwa na Zanzibar katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu. Kwa upande wa uzoefu itakuwa ni pigo kubwa kwa Stars kama wachezaji hao vijana watashindwa kuendena na michuano kwa kigezo cha uzoefu wao mdogo. Ni vijanma ambao wameshikilia namba katika vilabu vyao vya Azam FC, na Yanga kwa zaidi ya miezi 14 sasa, na wamekuwa chaguo la kwanza katika michezo zaidi ya 15 ya Kilimanjaro Stars, na Taifa STars katika kipindi cha mwaka mmoja sasa
Wanatakiwa kujiam,ini zaidio na kuongeza uimakini katika mchezo dhidi ya Zambia, timu ambao husifika kwa kasi yao mchezoni na mchezo wa pasi za haraka haraka zile fupifupi, Kwa, Salum sina shaka ataweza kuwazima kama ilivyo kawaida yake, ni mtaalamu wa pasi fupi na ndefu, ni nadra kupoteza au kupiga pasi ' fyongo' uwanjani, wakati Domayo akisifika kwa utulivu wake, bado viongo hao wamekuwa wakisumbuliwa na tatizo la kushindwa kutengeneza nafasi za mwisho japo muda mwingine huoneka kumiliki mchezo kwa kiasi kikubwa.
Wakati, Samatta na Ulimwengu tukisubiri huduma zao silaha yetu kubwa sasa ni Ngassa, ni vipi tunaweza kumchezesha na akaisadia timu, mbio zake, akili yake na uwezo wake alionao wa kutambua afanye nini atapokuwa amefika katika lango la adui, Domayo anaweza kupiga pasi ndefu zilizotimilifu itakuwa vyema kumtumia huyu kupiga pasi za haraka kwa Ngassa. Ni wazi Zambia watamili mpira mpira hiyo ni kutokana na namna tunavyoshindwa kuwa mashindanoni. Kwa nini nasema hivyo? Wakati mwingine ni lazima tuwe wazi wachezaji wetu hutuangusha hasa pale tunapokuwa tunaweka imani kubwa juu yao.
Kufungwa michezo mitatu, kati ya sita katika michuano iliyopita ni sawa na kutoa udhibitisho huo, wakati tulipofungwa mchezo wa kwanza na Burundi, ilitukumbusha kupandisha kiwango chetu cha uchezaji, hiyo ilitusaidia hadi kuwa na wafungaji bora wawili siku ya mwisho wa michuano. Tulicheza vizuri katika michezo miwili tu iliyofuata, lakini kipigo kutoka kwa Uganda kilikuwa ni ' kizito sana' katika vichwa vya mashabiki wa soka nchini. Tulifungwa kidhaifu sana katika mchezo wa nusu fainali huku Watanzania wakiamini kuwa ilikuwa nafasi yetu kuvunja utawala wa zaidi ya miaka kumi wa Uganda kutofungwa nyumbani.
Uzoefu wa wachezaji kama Kelvin Yondan, Athumani Idd ' Chuji' , Kiemba, Ngassa, Erasto Nyoni, Ivo Mapunda, usiishie katika uwakilishi wa uwanjani tu, wanatakiwa kuwakumbusha wachezaji vijana kama kina Ramadhani Singano, Domayo, Dilunga, Kimwaga na wengine umuhimu wa kuona fahari kushinda mataji wakiwa katika jezi ya taifa. Wakati tulipopata taji la mwisho mwaka 2010 kuna vijana ambao walitoka mitaani na kupata nafasi ya kukutana na watawala wa juu wa nchini. Ni fahari kuichezea timu yako ya Taifa. Ila mafanikio ndiyo kipimo sahihi cha ubora wa jambo lolote. HIvyo wachezaji wanatakiwa kufahamu kuwa tangu kizazi na kizazi wapo wachezaji ambao wamekuwa wakiiwakilisha nchi, ila wale waliofanikiwa kushinda chochote ndiyo waliopata nafasi ya kufika bungeni, ikulu na sehemu nyingine ambazo si rahisi kufika.
 KUJIAMINI KUPITA KIASI
Japo umakini limekuwa tatizo kubwa kwa Stars, kujiamini kupitiliza imekuwa ni sumu ambayo imekuwa ikituangamiza sisi wenyewe. WAtazame, Salum, Domayo na safu ya ulinzi. JInsi wanavyokuwa wanacheza wakati tukimiliki mpira imekuwa kama hawajui umuhimu wa kutengeza nafasi za kufunga mabao. Hii ni michuano ya mtoano. Nafasi moja, bao moja, kufungwa inamaanisha kuwa mchezo ujao utakuwa ni mgumu kuliko kama mngeshinda, na nafasi inakuwa ndogo ya kusawazisha mambo.
Safu ya ulinzi, Nyoni, anatakiwa kupevuka kiuchezaji sasa na kuacha na soka la ' kipima joto', huwa hatabiriki , ingawa akiwa katika siku yake nzuri utapenda kuona anavyokuwa akiisaidia timu katika mashambulizi na kuzuia, ila akiwa hovyo utatamani apasi, akisumbuliwa mara mbili au tatu hupoteza kujiamini na umakini wake unakuwa chini zaidi. Kwa kifupi safu za ulinzi wa pembeni zikiwa imara na kufanya kazi ipasavyo hufanya ulinzi wote kuimarika, ila wakiwa katika kiwango cha kupoteza mipira hovyo na kushindwa kujiamini katika maamuzi yao hupelekea kuvuruga mambo na wakati walinzi wa kati wakishirikiana na viungo kujaribu kuweka mambo sawa mara nyingi tunajikuta tukipotea kabisa uwanjani. Wachezaji wa ulinzi watakiwa kucheza soka lililokamilika kwa wakati huu wakiwa na michezo mingi katika historia yao.
" Kama utacheza vizuri na kushinda hilo ni bora, ila kama hautocheza vizuri kwa namna yoyote ile, hakikisha ushanda kwa  namna yoyote" aliwahi kusema, Luis Aragones, kocha wa kwanza kuipa Hispania taji baada za kupita miaka zaidi ya 40.
 BURUNDI, UGANDA, ETHIOPIA
Stars itacheza tena na Burundi katika kundi la B, na matokeo yao dhidi ya ' Risasi za Shaba' hapo kesho yanaweza kuufanya mchezo dhidi ya makamu bingwa hao wa mwaka 2004 kuwa mgumu zaidi na kuamua hatma ya kundi. Mwaka jana bao lililofungwa na Suleimani Ndikumana lilizamisha Stars nchini Uganda katika mchezo wa hatua ya makundi. Burundi, sambamba na Uganda, na Ethiopia wanaitumia michuano hii ili kujiweka sawa na michuano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani, CHAN 2014, nchini Afrika ya Kusini, mapema mwaka ujao.

TAKWIMU
Hizi ni takwimu za kila nchi katika michuano hiyo tangu kuanzishwa.
Namba ni nafasi ambayo timu huonesha ilimazima katika nafasi gani
1' Huonesha ni nafasi ya kwanza, Namba mbili huwakilisha nafasi ya pili, Namba tatu kwa nafasi ya tatu kama ilivyo kwa namba nne kwa nafasi ya nne.

Burundi
1 –
2 2004
3 –
4 1999, 2007, 2008
Ivory Coast
1 –
2 2010[b][i]
3 –
4 –
Eritrea
1 –
2 –
3 –
4 1994
Ethiopia
1 1987, 2001, 2004, 2005
2 –
3 2000
4 1995, 2010
Kenya
1 1975, 1981, 1982, 1983, 2002
2 1979, 1985, 1991, 1999, 2001, 2008, 2012
3 1978, 1988, 1989, 1994, 1995, 2003
4 1977, 1984, 1996, 2004
Malawi[i]
1 1978, 1979, 1988
2 1975, 1984, 1989
3 1977, 1980, 1985
4 1983, 1992
Rwanda
1 1999[b]
2 2003, 2005, 2007, 2009, 2011
3 1999, 2001, 2002, 2006
4 2000, 2001[b]
Sudan
1 1980, 2006, 2007
2 1990, 1996[b]
3 1996, 2004, 2011
4 1991, 2003
Tanzania
1 1974, 1994, 2010
2 1973, 1980, 1981, 1992[b], 2002
3 1979, 1990, 2008
4 2009, 2011, 2012
Uganda
1 1973, 1976, 1977, 1989, 1990, 1992, 1996, 2000, 2003, 2008, 2009, 2011, 2012
2 1974, 1982, 1994, 1995[b], 2000
3 1983, 1984, 1987, 1991, 2007, 2010
4 1978, 1981, 1985, 2002, 2005, 2006
Zambia[i]
1 1984, 1991
2 1976, 1977, 1978, 1988, 2006
3 1981, 1992
4 1980, 1989
Zanzibar
1 1995
2 –
3 2005, 2009, 2012
4 1979, 1982, 1987, 1990
Zimbabwe[i]
1 1985
2 1983, 1987
3 1982
4 1988
By number of titles won and editions participated in Team 1ST 2ND 3RD 4TH Pld Pldlst Uganda 13 5 6 6 35 2012 Kenya 5 7 6 4 34 2012 Ethiopia 4 – 1 2 17 2012 Tanzania 3 5 3 3 33 2012 Malawi 3 3 3 2 21 2012 Sudan 3 2 3 2 19 2012 Zambia 2 5 2 2 20 2010 Zimbabwe 1 2 1 1 16 2012 Zanzibar 1 – 3 4 32 2012 Rwanda B 1 – – – 2 2001 Rwanda – 5 4 2 16 2012 Burundi – 1 – 3 13 2012 Côte d'Ivoire B – 1 – – 1 2010 Eritrea – – – 1 10 2012 Djibouti – – – – 10 2011 Kenya B – – – – 2 1994 Seychelles – – – – 2 1994 Somalia – – – – 23 2012 South Sudan – – – – 1 2012 Sudan B – – – – 1 1996 Tanzania B – – – – 1 1992 Uganda B – – – – 2 2000 Zimbabwe U23 – – – – 1 2

MASHABIKI WA SIMBA NA YANGA KUCHUANA NANI MTANI JEMBE DODOMA, MUSOMA NA SINGIDA...

Na Mwandishi Wetu

Kampeni ya Kili Nani Mtani Jembe itaendelea kuunguruma tena Jumapili wiki hii na kuwapa nafasi mashabiki wa Simba na Yanga walioko Dodoma, Musoma na Singida na kuchuana vikali katika michezo mbalimbali huku wakihakikisha timu zao zinaibuka na kitita cha shilingi milioni mia moja zilizotengwa na Kilimanjaro Premium Lager kwa ajili ya Watani wa Jadi kupitia kampeni hiyo.

Mratibu wa mabonanza hayo, Lawrence Andrew amesema jijini Dar es salaam jana kwamba mashabiki watapata fursa ya kushiriki katika michezo mbalimbali kama vile foosball, kuvutana kamba, soka la wachezaji saba kila upande maarufu kama “Seven aside” na kuongeza kuwa ili kuhakikisha mashabiki hao wanafurahia ipasavyo burudani mbalimbali za muziki zitakuwepo pamoja na Nyama choma.
Andrew alisema kuwa katika mji wa mji wa Dodoma bonanza la Kili Nani Mtani Jembe litafanyika katika uwanja wa shule ya Dodoma Sekondari ambapo bendi maarufu ya The TNC Band itatumbuiza. Na huko Musoma bonanza litafanyika katika uwanja wa Mukonde na kupambwa na bendi ya Musoma Stars huku mkoani Singida likifanyika katika Uwanja wa Namfua na burudani kabambe ikishushwa na Wana Pamba Music Band aka Watoto wa Mujini bendi ambayo imejizolea umaarufu mkubwa sana mkoani humo.
Andrew pia amesema kuwa vilevile kuwa michezo mbalimbali ya kujifurahisha kama vile kufukuza kuku wa kienyeji, kukimbia na gunia na kupiga penati ukiwa umefungwa kitambaa usoni itapamba mabonanza hayo ambayo yatafanyika katika mikoa hiyo kwa mara ya kwanza kupitia Nani Mtani Jembe. Kampeni hii ya aina yake inatoa fursa ya kipekee kwa mashabiki hao kujumuika pamoja na kuburudika na vile vile imeongeza chachu ya ushindani na utani wa jadi kati ya mashabiki hao huku ikiwapa fursa ya kipekee kuonyesha mapenzi kwa timu zao.
Mabonanza hayo yanalotarajiwa kuanza saa tatu asubuhi ni mwendelezo wa kampeni ya Nani Mtani Jembe ambayo inafanyika nchi nzima ikiwashirikisha mashabiki wa timu kongwe za Simba na Yanga. Kupitia kampeni hiyo, Kilimanjaro Premium Lager inayozidhamini timu za Simba ya Yanga imetenga kiasi cha shilingi milioni 100 na kisha kuzigawanya kwa timu hizo ambapo kila timu inazo shilingi milioni 50 ambazo zinashindaniwa na mashabiki wao.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro George Kavishe alisema kuwa mashabikiwa Simba na Yanga wanatakiwa kushindana kwa kushiriki kwenye kampeni hiyo ili kuhakikisha kuwa timu mojawapo inapata fedha nyingi zaidi ya timu nyingine.
Akielezea namna ya kushiriki, Kavishe alisema kuwa mpaka kila timu imetengewa shilingi milioni 50 na kuwa mshiriki wa shindano hilo la Nani Mtani Jembe ambaye ni shabiki wa Simba au Yanga anachotakiwa kufanya ni kununua bia ya Kilimanjaro Premium Lager ambayo kwenye kizibo chake kuna namba ya kushiriki.
Alisema baada ya shabiki kununua bia ya Kilimanjaro na kuona namba ya kwenye kizibo, anachotakiwa kufanya ni kuchukua simu yake ya kiganjani na kuandika ujumbe mfupi wa maneno akianza na jina la timu anayoshabikia kisha anaandika namba iliyo kwenye kizibo na kuituma kwenye namba 15440.
Alisema baada ya shabiki kutuma namba hiyo, atakuwa amepunguza shilingi 10,000 kutoka kwa timu pinzani yaani ikiwa shabiki aliyetuma ujumbe huo ni wa Simba atakuwa amefanikiwa kupunguza shilingi 10,000 kutoka kwenye fungu la Yanga na ikiwa shabiki ni wa Yanga pia atakuwa amepunguza shilingi 10,000 kutoka kwa Simba.
Kwa mujibu wa Kavishe matokeo ya uwiano wa fedha zinavyopungua kutoka Simba au Yanga yatangazwa kila siku hadi siku ya mwisho wa shindano hilo Desemba 14, mwaka huu siku ambayo watani wa jadi Simba na Yanga watacheza mechi ya kuhitimisha kampeni hiyo kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

PIGO TENA KWA KASEJA... APIGWA CHINI KIKOSI CHA STARS CHALLENJI: IVO, DILUNGA, KIMWAGA, SAMATA NA ULIMWENGU NDANI ...

Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen ametaja kikosi cha wachezaji 23 watakaoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayofanyika nchini Kenya kuanzia Novemba 27 mwaka huu.
Kilimanjaro Stars iliyotwaa kombe hilo mara ya mwisho mwaka 2010 chini ya Kocha Jan Poulsen, na ambayo imepangwa kundi B katika michuano ya mwaka huu itacheza mechi yake ya kwanza Novemba 28 mwaka dhidi ya Zambia kwenye Uwanja wa Machakos.
Wachezaji wanaounda kikosi hicho cha Tanzania Bara ni makipa Deogratius Munishi (Yanga), Ivo Mapunda (Gor Mahia, Kenya) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Erasto Nyoni (Azam), Himid Mao (Azam), Ismail Gambo (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Michael Pius (Ruvu Shooting) na Said Moradi (Azam).
Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Ramadhan Singano (Simba) na Salum Abubakar (Azam).
Safu ya ushambuliaji inaundwa na Elias Maguli (Ruvu Shooting), Faridi Musa (Azam), Joseph Kimwaga (Azam), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar), Mbwana Samata (TP Mazembe, DRC), Mrisho Ngasa (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC).
Kilimanjaro Stars inatarajia kuondoka Jumatatu (Novemba 25 mwaka huu) kwenda Nairobi kushiriki michuano hiyo itakayoanza Novemba 27 mwaka huu na kumalizika Desemba 13 mwaka huu.   
MECHI DHIDI YA STARS, ZIMBABWE YAINGIZA MIL 50/-
Mechi ya kirafiki ya kimataifa ya FIFA Date kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Zimbabwe (The Warriors) iliyochezwa juzi (Novemba 19 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 50,980,000 kutokana na watazamaji 7,952.
Tiketi za kushuhudia mechi hiyo ziliuzwa kwa sh. 5,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.
Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 7,776,610.17 wakati wa gharama za uchapaji tiketi ni sh. 3,682,560.
Asilimia 15 ya uwanja sh. 5,928,124, asilimia 20 ya gharama za mechi sh. 7,904,166 na asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 1,976,041.
Asilimia 60 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 17,784,373 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 889,219 ambayo ni asilimia 5 kutoka kwenye mgawo wa TFF.

MWISHO WA RAGE SIMBA SASA UMEFIKA...


Na Baraka Mbolembole

Kuelekea mwisho wa utawala wa Hassan Dalali kama mwenyekiti wa klabu ya soka ya Simba, timu hiyo ya ' Msimbazi' ilikuwa katika wakati mgumu kiutawala. Dalali, alikua aishi kuvurugana na aliyekuwa katibu wake mkuu, Mwina Kaduguda. 

Kwa mtazamo wa haraka, Dalali ndiye ' Mwanachama- kiongozi' anayekubalika zaidi na ' Wana- Simba', ila katika utendaji wake wa mambo muhimu katika makaratasi ilikuwa ni tatizo kubwa. Kumalizika kwa muda wa utawala wake, klabu ikaingia
katika uchaguzi huru na wa haki na hapo, Julai, 2010, Ismail Aden Rage akaingia madarakani.
Nchi yetu bwanaaa, kila mahali migomo tu, hadi wenye maduka wameingia katika hali hiyo ili kutetea usawa wao. Je, haki ni nini? Bila shaka haki ni kitu ambacho kinajiendesha chenyewe bila choyo, Mtu mwenye hekima na Busara hutembea na kitu hiki huku kikimuongoza katika harakati zake za maisha. Harakati ni nini? Harakati ni njia ya maisha tu. Ni lazima tuitende haki na kuisadiki. Yule mwenye kufanya dhuluma, atalipwa dhuluma, na malipo ya dhuluma hiyo huwa ni kubwa kuliko dhuluma yenyewe.

 'MTU MKUBWA NI MWANAFUZI'
Kwa, Rage bila shaka Simba, ilifikiriwa ingesogea hatua fulani mbele, ila matokeo yake ni watu kukosa imani zaidi kwa Mwenyekiti huyo wa zamani wa Moro United, na katibu mkuu wa zamani wa Chama cha Soka Nchini, FAT, ( Sasa, TFF).. Mimi kwa upande wangu nilikuwa mara zote nikiangukia katika upande wa hoja za Mh. Rage, si kutokana na ' Siasa' zake bali kutokana na aina ya mtazamo wake wakati akiwa anazungumzia mipango ya maendeleo.
Wakati akiingia klabuni Simba, kama Mwenyekiti wa klabu nilifikiri labda sasa Simba itakuwa katika hali fulani nafuu, kiuchumi, kiutawala, na kiuendeshaji. Matokeo yake imekuwa ni fedhea kubwa. Wakati huu, ' Wasomi' kama Rage wakitawala soka la Tanzania, ni wazi mawazo yao mapya yanaweza kupingwa na upande mwingine, hasa upande ule ambao wanaamini kuwa soka linaweza kuendeshwa na mwanasoka wa zamani. Hapana, kuondoka kwa Dalali, hakukuja kwa bahati mbaya, alikuwa kiongozi mzuri lakini elimu yake ikamuondoa huku kundi kubwa la wanachama likitaka aorodheshwe katika orodha ya mwisho ya wagombea kinyume na katiba.
Funzo la kuondoka madarakani kwa Dalali, huku wanachama wengi wakimpigania lilipita nje ya fikra za Rage ambaye alikuja kushinda kwa kishindo katika uchaguzi. Ahadi zake zilikuwa ni nzuri, zilimvutia kila mmoja na ndiyo maana alishinda. ' Mtu mkubwa ni Mwanafunzi, kwani hutamani vitu zaidi kuliko watu wengine', na kwa Rage jambo moja kubwa lililomuingiza madaraki ni kuhiimariasha klabu kutoka katika utegemezi wa pesa za watu binafsi. Alisema kuwa ndani ya utawala wake Simba itakuwa na uwanja wake binafsi. Muda umekwenda sasa, na suala la Mwenyekiti huyo aliyesimamishwa na kamati ya utendaji kutoitisha mkutano wa katiba mpya ya klabu limewakera wengi na kumuona ni mtu mbinafsi, hasiye shahurika na mwenye maamuzi mabaya kwa klabu.

MALINZI KUFUNGUA MICHUANO YA UHAI 2013...


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi atafungua rasmi michuano ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 (U20) kwa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom mwaka huu.
Uzinduzi wa mashindano hayo utafanyika kesho (Novemba 17 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam saa 2 kamili asubuhi. Mechi ya ufunguzi itakuwa ya kundi A kati ya Azam na Coastal Union.
Mechi nyingine za kesho ni kundi; Yanga na Mbeya City (saa 8 mchana- Uwanja wa Karume), kundi B ni Ruvu Shooting na Ashanti United (saa 4 asubuhi- Uwanja wa Karume), Oljoro JKT na Simba (saa 10 jioni- Uwanja wa Karume).
Kundi C kutakuwa na mechi kati ya Kagera Sugar na Mtibwa Sugar itakayochezwa saa 2 kamili asubuhi kwenye Uwanja wa Azam Complex, na kwenye uwanja huo huo saa 10 jioni ni Rhino Rangers dhidi ya Tanzania Prisons.
RAMBIRAMBI MSIBA WA NYOTA COPA COCA-COLA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa Sayari, Fatuma Bahau ‘Crouch’ kilichotokea jana (Novemba 15 mwaka huu) kwenye Hospitali ya Temeke, Dar es Salaam.
Msiba huo ni mkubwa katika mpira wa miguu kwani Fatuma ndiyo kwanza alikuwa anachipukia katika mpira wa miguu wa wanawake ambapo alikuwa mfungaji bora wa michuano ya U15 Copa Coca-Cola ya mwaka huu akichezea timu ya Ilala, hivyo mchango wake katika mchezo huu tutaukumbuka daima.
Kwa mujibu wa mlezi wa mchezaji huyo, Stephania Kabumba, marehemu anasafirishwa kesho kwenda kwao Mwanza kwa ajili ya maziko ambapo kifo chake kimesababishwa na ugonjwa wa malaria.
TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Bahau, klabu ya Sayari, Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA) na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Mungu aiweke roho ya marehemu Fatuma mahali pema peponi. Amina

KIFAA KINGINE YANGA HIKI HAPA BAADA YA KASEJA...


VUJO ZATAWALA LIGI KUU YA VODACOM,KATI YA SIMBA NA KAGERA,JIONEEE MWENYEWE...

1  
October 31 2013 kulikua na mechi ya Simba vs Kagera Sugar kwenye uwanja wa taifa ambapo timu hizo zilitoka 1-1 huku goli lililoleta malalamiko likiwa ni la Kagera Sugar ambalo lilifungwa kwa njia ya penat.
Kocha wa Kagera Sugar amesifia maamuzi ya refa na kusema ‘nafurahi timu imesawazisha kwenye dakika za mwisho na refa amefanya kazi yake kwa sababu ni siku nyingi sana marefa hawagawi penat kama hizo, timu nzuri inacheza mpaka goli’

Kocha Kibaden wa Simba kasema ‘nashukuru tumemaliza mpira salama na vijana wametoka salama, sijafurahishwa na jinsi mpira ulivyochezeshwa, sitaki kusema hayo kwa sababu watu wana macho na wanaweza kukosoa lakini uamuzi haukuwa sawasawa, kama tutaendelea na mpira wa aina hii nafikiri tutaondoka kwenye mwelekeo… 
naomba TFF mpya iliyokuja ijaribu kutazama watu wapumbavu wa aina hii wanaokuja pale kuwaudhi watu, sijafurahishwa na mpira ulivyochezeshwa mwanzo hadi mwisho na nilijua kitatokea nini’

WAZIRI WA HABARI NA MICHEZO,MKURUGEZI WAFUNGIWA NA VYOMBO VYA HABARI...

VYOMBO vya habari nchini vimeandika historia ya aina yake ya kupitisha azimio la kuwafungia kwa muda usiojulikana, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene.
Hatua hiyo inakuja ikiwa ni takriban wiki mbili tangu viongozi hao kutumia mamlaka wanayopewa na sheria ya magazeti ya mwaka 1976, kuyafungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania kutochapishwa kwa madai ya kuchapisha habari za uchochezi.
Wakati gazeti la Mwananchi likifungiwa kwa siku 14, Mtanzania limefungiwa kwa siku 90.
Vilevile hatua hiyo imekuja zaidi ya mwaka mmoja tangu viongozi hao walifungie gazeti la wiki la MwanaHalisi pia kwa madai ya kuchapisha habari za uchochezi.
Taarifa iliyotolewa na Jukwaa la Wahariri (TEF) jana, ilisema kuwa uamuzi huo umefikiwa kwa pamoja na Jukwaa hilo, Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT) na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA Tan).
Wamo pia Baraza la Habari Tanzania (MCT), Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Dar City Press Club (DCPC) na Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDC).
Hatua hiyo inamaanisha kuwa kuanzia jana, habari zozote zitakazotolewa au kuwahusisha Waziri Mukangara na Mkurugenzi wa Maelezo, Mwambene, hazitaandikwa ama kutangazwa na chombo chochote cha habari kwa muda usiojulikana.
Hatua ya kuwafungia viongozi hao inafuatia kikao cha pamoja cha wadau hao kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam kutokana na hatua ya serikali kuyafungia magazeti hayo.
Mukangara na Mwambene wamefungiwa kwa tuhuma ya kudharau na kufanya uamuzi wa kuyafungia magazeti hayo bila kusikiliza hoja za upande wa pili.
Wanadaiwa pia kutoa maneno yaliyolenga kupotosha umma kwa makusudi juu ya hatua ya kuyafungia magazeti hayo.
Wadau hao walieleza kusikitishwa na hatua ya serikali ya kupuuza kilio chao cha kuomba kusitishwa kwa sheria kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976.
Vilevile wanalalamikia kudhoofishwa kwa mchakato wa kuibadilisha sheria hiyo iliyotajwa na Tume ya Jaji Francis Nyalali mwaka 1992, kuwa ipo kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Hivyo tunasitisha kuandika, kutangaza na kupiga picha shughuli zozote zitakazowahusisha au kuratibiwa na Waziri Mukangara na Mwambene hadi hapo itakapotangazwa vinginevyo.
“Wadau wa habari tutaendelea kupinga sheria ya magazeti ya mwaka 1976 kwa kupigia kelele kufutwa kwa sheria hiyo na kuongeza nguvu ya kisheria mahakamani kwenye kesi iliyofunguliwa na Kampuni ya Hali Halisi Publishers Ltd, mwaka 2009 inayopinga sheria hiyo,” ilisema taarifa ya TEF.
-TANZANIA DAIMA

HUU NDIO MSIMAMO WA LIGI KUU YA VODACOM ULIVYO MPAKA SASA BAADA YA ROUNDI YA SABA...

RUVU SHOTING YAIBANA SIMBA LIGI KUU - YATOKA SARE 1-1 NA SIMBA...


 Mshambuliaji wa Simba, Haruna Chanongo akichuana na beki wa Ruvu shooting, stephano Mwasyika. (Picha na Habari Mseto Blog)
 Amri Kiemba akichuana beki wa Ruvu Shooting, Abuu Hashim.
 Hekaheka katika lango la Ruvu Shooting.
 Mshambuliaji wa Simba, Betram Mombeki akimiliki mpira huku akizongwa na beki wa Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania bara uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
 Golikipa wa Ruvu Shooting, Abdul Seif akiokoa moja ya hatari langoni mwake.
 Berntram Mombeki akiruka daruga la beki wa Ruvu Shooting, Abuu Hashim. 
Henry Joseph, Abel Dhaira na Joseph Owino wakiteta jambo wakati wakitoka mapumziko. PICHA NA FRNACIS NDADE

AZAM YATOKA SARE NA WAGOSI COASTAL UNION - MECHI YATAWALIWA NA VURUGU...


 Leo golikipa wa Azam Mwadini Ally alikuwa na wakati mgumu sana, ingawa bahati haikuwa ya Wagosi.


                             Yayo Kato akitafuta mbinu za kumtoka beki wa Azam FC.
 Nahodha Jerry Santo akikunjuka nje kidogo ya lango la Azam, ingawa shuti lake halikuleta madhara.
 Kocha wa Coastal Union, Hemed Moroco akiwabwatukia wachezaji wake wacheze kama alivyowafunza.



 Hili ndilo bao la kipindi cha pili walilokosa Coastal Union, ambapo shuti la Selembe lilipita mikononi mwa Mwadini Ally na kugonga mwamba.


SULUHU ya bila kufungana kati ya Coastal Union na Azam FC katika uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga imezidi kuwaongezea idadi ya suluhu Wagosi wa kaya katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Mchezo huo uliokuwa na presha kubwa kwa mashabiki na wachezaji ulimuweka katika wakati mgumu mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani, kutokana na kushutumiwa kuwapendelea Azam FC.

Kipindi cha kwanza timu zote zilicheza kwa nguvu zikihakikisha zinapata mabao ya mapema na kujihakikishia ushindi lakini hakuna hata timu moja iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake.

Kipindi cha pili kilianza kwa Azam FC kushambulia kwa kasi huku wakimiliki mpira hali iliyowachanganya wachezaji wa Coastal Union wakaanza kupoteana na kucheza bila kufuata mfumo. Hali hiyo ilizidi kuwachanganya Wagosi wa Kaya hasa baada ya mwamuzi kuanza kutoa maamuzi ya utata, kwani katika dakika ya sabini alitoa kona kwa Azam wakati ilikuwa ni goal kick.

Mashabiki wakaanza kuhamaki na kutaka kuvuruga mchezo baada ya mwamuzi kuzidisha kutoa maamuzi ya utata kama faulo zisizoeleweka na kona za utata. Hali hiyo ilimtisha mwamuzi na kusimamisha mchezo mara kwa mara ili kuwataka wasimamizi wa mchezo huo kuwatuliza mashabiki.

Tukio lililotokea kipindi cha kwanza ambapo mwamuzi wa pembeni alipigwa na kitu kisichojulikana kutoka jukwaa la 'Rasha' lilitaka kujirudia kipindi cha pili baada ya chupa na mawe kutupwa uwanjani baada ya mwamuzi kutoa faulo nje kidogo ya 18 upande wa Coastal Union.

Dakika ya 65 mwalimu Hemed Moroco alifanya mabadiliko na kumtoa Pius Kisambale akaingia Suleiman Kassim 'Selembe'. Mabadiliko hayo yaliongeza uhai kwa Wagosi hasa kutokana na aina ya uchezaji wa Selembe kutumia mipira ya kasi.

Azam FC walianza kuelemewa kutokana na Mganda, Yayo Kato kutumia vema mwili wake mfupi na wenye nguvu kuwashambulia mabeki wa Azam, hali hiyo iliwafanya Azam kubadilika na kucheza mpira wa hovyo uliowapa nafasi Coastal Union kupiga mipira mirefu ambapo ilipofika dakika ya 75 kipindi cha pili katika jukwaa la African Sports, Wagosi walikosa bao la wazi baada ya Selembe kupiga krosi iliyopenya ngome ya Azam akiwemo mlinda mlango Mwadini Ally na kugonga mwamba.

Kutokana na piga nikupige ya lala salama kufika dakika ya 74 mwamuzi alimnyooshea mlinzi wa kulia wa Coastal Union, kinda Hamadi Juma 'Basmat', kadi nyekundu baada ya kubadilishiana maneno na mchezaji wa Azam, Kipre Tchetche.

Tukio hilo lilianzia kwa Kipre kumpiga Hamadi kiwiko cha shingo hali iliyomfanya kinda huyo kumfuata kwa jazaba huku akimuuliza kwanini amemfanyia hivyo. Mwamuzi baada ya kuona Hamadi amemuelekezea kichwa Kipre akadhani kinda huyo anapigana ndipo akatoa kadi ya moja kwa moja.

Baada ya kadi hiyo hali ya uwanja ilichafuka ambapo mashabiki walikuwa wakipiga kelele huku wachezaji wakitaka kupigana, ndipo mchezaji mwingine wa Coastal Union beki wa kushoto Othman Tamim akapewa kadi ya njano papo hapo.

Baadaye mchezo ulirudi katika hali yake lakini ngome ya Coastal Union ilikuwa imepwaya hali iliyomfanya Juma Said 'Nyoso' kuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha ngome yao inakuwa imara.

Ilipofika dakika ya 84 mwlimu Moroco alifanya mabadiliko kwa kumtoa Uhuru Suleiman na kumuingiza Yusuf Chuma. Ambapo kinda huyo alionyesha uwezo mkubwa na kurudisha uhai wa safu ya ulinzi.

Mpaka mwamuzi wa leo anapuliza kipyenga cha mwisho matokeo yaliendelea kusomeka hivyo hivyohivyo 0-0, na kuendelea kuibakisha Coastal Union katika nafasi ya nne ikiwa na point 11 nyuma ya Azam iliyo nafasi ya tatu yenye point 11 lakini ikiwa na mabao mengi ya kufunga.

Baada ya mechi ya leo Coastal Union itashuka dimbani wiki ijayo katika uwanja wa Chamazi dhidi ya Ashanti United wanaoshika mkia katika ligi
.

Popular Post

 
Support : OBAMA | OBAMA | OBAMA
Copyright © 2013. DiraYaLeo - All Rights Reserved
Template Created by Barakaeli Aremu Published by Dira Ya Leo
Proudly powered by Blogger