muhtasari

Latest Article Get our latest posts by subscribing this site

CCM, CHADEMA, CUF WANAVURUGA BUNGE, ASEMA DOVUTWA…

Mjumbe wa bunge maalumu la katiba Fahmi Dovutwa akichangia mada wakati wa semina ya wajumbe hao ya kupitia vifungu vya rasimu ya kanuni juzi.Picha na Silvan Kiwale 

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Fahmi Dovutwa alichafua hali ya hewa baada ya kuvituhumu vyama vya CCM, Chadema na CUF kuwa ndiyo vinavuruga Bunge kwa sababu ya misimamo yao.
Hali hiyo ilitokea wakati mjumbe huyo akichangia mjadala wa Rasimu ya Kanuni za Uendeshaji wa Bunge Maalumu la Katiba juzi.
Dovutwa alitoa shutuma hizo baada ya mjumbe mwingine, Julius Mtatiro kueleza kuwa amepitia Rasimu ya Kanuni lakini hakuona mahali panapoeleza mpangilio wa ukaaji wakati wa kupiga kura.
Hali hiyo ilimfanya Dovutwa, kusimama na kutoa tuhuma kuwa baadhi ya wajumbe wamehongwa na kwamba kuruhusu mpangilio maalumu ni kukaribisha mgawanyiko.
Alisema kukaa kwa mpangilio huo kutawapa nafasi viongozi mbalimbali kushinikiza wajumbe wao katika maamuzi ya mambo mbalimbali.
“Ukaaji wa sasa umezingatia masilahi ya nchi, utashi na matakwa ya wananchi. Watu wa CCM, CUF na Chadema ndiyo mnaharibu mkutano (Bunge),” alisema Dovutwa.
Dovutwa alisema vyama hivyo vinatofautiana katika masuala mbalimbali na misimamo yao ndiyo imetawala bunge hilo.
“Mnatulazimisha tuwasikilize nyie tu. Kwa hiyo Mwenyekiti usikubali, kikao hiki kizingatie masilahi mapana ya makundi mbalimbali,” aliongeza Dovutwa.
Baada ya kutamka hilo, mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Kupitia Kanuni, Amon Mpanju alisimama na kumtaka Kificho kulisaidia Bunge hilo kwenda na utaratibu aliowatangazia juzi wajumbe, ambao wanatakiwa kuwasilisha hoja zao kwenye kamati kisha kutolewa uamuzi.
“Naomba uamuzi ukishafanyika, kiti chako kisiruhusu mtu mwingine kuingilia maana mchakato hautafika mwisho. Nawaomba wajumbe wenzangu tusilete michango inayoweza kuleta hisia za mgawanyiko miongoni mwetu,” alisema Mpanju.
Mtatiro alisema hakupendezwa na mchango wa Dovutwa na kutahadharisha ukweli hauwezi kukwepeka kwa kuwa kuna watu wanaotoka katika makundi mbalimbali.
“Wakati wa kupiga kura tunahitaji theluthi mbili ya wajumbe wa Tanzania Bara na idadi kama hiyo kwa wajumbe kutoka Zanzibar kwa hiyo ili kurahisisha kazi hiyo, wajumbe kutoka Zanzibar wakae upande wao na wale wa Bara wakae upande wao,” alisema Mtatiro.
-mwananchi

KATIBA MPYA KUTUMIKA KATIKA UCHAGUZI MKUU UJAO...KATIBA YA TANGANYIKA YAPENDEKEZWA IPEWE MAANDALIZI YA MIAKA MINNE...


Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya, imeelekeza kipindi cha mpito ambacho pamoja na mambo mengine, kitaandaa mazingira ya Katiba hiyo kutumika kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. 
 
“Kufanya maandalizi na kuendesha Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kuzingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 2014 na kufanya maandalizi ya mambo yote muhimu kwa ajili ya utekelezaji bora wa masharti ya kikatiba yaliyomo kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 2014,” inasema sehemu ya rasimu hiyo.
 
Tume ya Mabadiliko ya Katiba pia imependekeza kipindi cha mpito cha miaka minne kuanzia tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba Mpya ili sheria zilizopo ziweze kubadilishwa.
 
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema jana kwamba katika kipindi hicho cha mpito utakuwa ni muda wa kutungwa kwa Katiba ya Tanganyika. 

Warioba alisema pia katika kipindi hicho, utakuwa ni muda wa mgawanyo wa rasilimali baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali za nchi washirika.
 
“Katika kipindi hicho pia utakuwa ni muda wa kufanya maandalizi na kuendesha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa kuzingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 2014,” alisema.
 
Warioba alisema katika kipindi hicho, Katiba ya Zanzibar itafanyiwa marekebisho ili kuwiana na masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 2014.
 
Sehemu ya Rasimu ya Katiba ya Muungano, imependekeza kuwa maoni yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, yanaweza kutumika kutengeneza Katiba ya Tanganyika.

>>Mwananchi

MAANDAMANO YA VYAMA VYA UPINZANI YASITISHWA...KWANINI SOMA UJIONEE...


Viongozi Wakuu wa vyama vya siasa nchini Tanzania, NCCR-Mageuzi, CHADEMA na CUF wametangaza kusitisha mpango wa maandamano uliokuwa umepangwa kufanyika siku ya Alhamisi, Oktoba 10, 2013 katika maeneo ya mikoa ya Unguja, Dar es Salaam, Mbeya, Kigoma, Dodoma, Tanga, Mwanza na Arusha kwa lengo la kudai upatikanaji wa muafaka wa mchakato wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yatakayowezesha kuundwa kwa Katiba Mpya inayokubalika na wananchi.

Mwenyekiti wa CUF akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake katika ofisi za Makao Makuu ya NCCR-Mageuzi jijini Dar es Salam, Profesa Ibrahim Lipumba amesema sababu kubwa ya kusitisha mikutano iliyopangwa inatokana na kuitambua nia ya Rais Kikwete aliyoionesha katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi, ambapo alibainisha wazi kuwa atakutana na viongozi wa vyama hivyo  kuzungumzia suala hilo la Muswada wa Katiba.
 

Kutokana na nia hiyo, alisema vyama hivyo havina budi kusubiri mazungumzo na Rais Kikete yatakayotoa dira ya kitakachoendelea katika lengo la kupata katiba shirikishi na inayokubalika na raia wengi.

“Tumesikia kupitia vyombo vya habari ambavyo navyo vimenukuu taarifa kutoka Ikulu, inayobainisha kuwa Rais Jakaya Kikwete amepanga kukutana na viongozi wa upinzani kati ya Oktoba 13 na 15 ili kujadili na kupata muafaka wa suala hili la Katiba. 


"Tunaamini kuwa taarifa hizi ni sahihi kabisa, hivyo tumeamua kusitisha maandamano yetu, yaliyolenga kushinikiza nguvu ya umma kuungana nasi katika kudai mchakato wa kuipata Katiba shirikishi, na kushinikiza Rais kutosaini kabisa muswada huo wa sheria  kwa kuwa una upungufu,” alisema Profesa Lipumba.

Viongozi hao pia wamesema wapo tayari kusubiri kukutana na Rais katika tarehe itakayopangwa na kuafikiwa.

“Pamoja na kuahirisha maandamano haya, tunapendekeza huo mkutano ulioahidiwa na Rais, ufanyike mapema ili mchakato wa Katiba unaosuasua kwa sasa uendelee kwa ufanisi,” alisema Lipumba.

Ikiwa mazungumzo hayo hayatafanikiwa, viongozi hao wameahidi kurejesha ratiba ya maandamano na mikutano.

Popular Post

 
Support : OBAMA | OBAMA | OBAMA
Copyright © 2013. DiraYaLeo - All Rights Reserved
Template Created by Barakaeli Aremu Published by Dira Ya Leo
Proudly powered by Blogger