muhtasari

Latest Article Get our latest posts by subscribing this site

WAZIRI NCHIMBI,KAMANDA KOVA WAWAKIMBIA KIBANDA NA DK.ULIMBOKA...

 
JESHI la Polisi limeonyesha wazi kuwa halina dhamira ya dhati ya kuwasaka na kuwatia nguvuni wahalifu waliowateka, kuwatesa na kuwaumiza vibaya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Absalom Kibanda, na Mwenyekiti wa Jumuia ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka.
Ni zaidi ya mwaka mmoja na miezi minne tangu Dk. Ulimboka atendewe unyama huo lakini hadi leo suala hilo limegeuzwa sinema na jeshi hilo kwa kumkamata mtu asiyehusika ambaye baadaye walilazimika kumwachia huru.
Hivi ndivyo imetokea pia kwa Kibanda ambaye ni Mahriri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006), kwani tangu ateswe na kung’olewa jicho, kucha, meno na kukatwa kidole, hakuna mtuhumiwa hata mmoja aliyekamatwa ikiwa ni zaidi ya miezi saba sasa.
Lakini jana Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, akiongozana na maofisa wengine wa jeshi hilo akiwemo Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, waliitisha mkutano na waandishi kuwataja ‘vibaka’ waliokamatwa wakihusishwa kumshambulia na kumwibia Dk. Sengondo Mvungi.
Dk. Mvungi ni mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambaye alivamiwa na majambazi hao takriban wiki mbili zilizopita na kukatwa mapanga na kuporwa kompyuta mpakato (laptop) na fedha.
Kwa sasa hali yake ni mbaya akiwa bado hajitambui na hivyo kulazimika kupelekwa nchini Afrika Kusini kujaribu kuokoa maisha yake.
Hatua ya Waziri Nchimbi kujitokeza jana kuzungumzia tukio hilo na kuonyesha juhudi za haraka za kuwanasa watuhumiwa, iliwasukuma waandishi wa habari kuhoji kulikoni matukio ya Ulimboka na Kibanda yamewekwa kiporo.
Kama kawaida yake, Kamishna Suleiman Kova alijibu kuwa kila tukio lina mazingira yake, hivyo tukio la Mvungi halifanani la Kibanda wala Dk. Ulimboka na kueleza kuwa mfumo wa suala hilo kiupelelezi unakwenda vizuri.
“Tukio la Mvungi na la kina Kibanda na Ulimboka mazingira yake ni tofauti; unapeleleza halafu unatuhumiwa wewe mwenyewe, ila watapatikana,” alisema Kova.
Katika taarifa yao hiyo, Dk. Nchimbi na Kova walisema kuwa wamekamatwa watuhumiwa wengine watatu zaidi wanaodaiwa kumvamia, kumjeruhi kwa mapanga na kumpora mali Dk. Mvungi.
Kova alisema kuwa operesheni ya kuwasaka waliomshambulia Dk.Mvungi imefanikiwa kwa asilimia zaidi ya 80 ambapo mpaka sasa wamekamatwa watu tisa wakiwa na vifaa walivyotendea uhalifu huo ambavyo ni mapanga matano, simu ya mkononi na kigoda.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Msigwa Kopelo, Chibango Magozi, Ahmed Ally, Zakaria Rafael (23) dereva wa boda boda, Manda Salowaa ( 40), Paulo Jailos (29), Juma Hamisi (29), Longishu Semaliki(29) muuza ugoro Vingunguti na Masunga Makenza (40).
Dk. Mvungi ambaye pia ni mshauri wa masuala ya kisheria wa Chama cha NCCR-Mageuzi alipatwa na mkasa huo usiku wa kuamkia Novemba 3, mwaka huu, akiwa nyumbani kwake Kibamba Msakuzi, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Baada ya kumjeruhi waliiba sh milioni moja, bastola, simu mbili za mkononi na kompyuta mpakato (laptop).
Utendaji huu wa jeshi la polisi unaacha mashaka makubwa hasa kwa matukio makubwa ya utekaji na utesaji ambayo ni mageni nchini, kwani uchunguzi wake wa kuwasaka watuhumiwa unalegalega.
Itakumbukwa kuwa mara tu baada ya tukio la Dk. Ulimboka Julai 26 mwaka jana, jeshi hilo liliunda kikosi kazi kilichowashirikisha wataalamu mbalimbali wa kanda maalumu na makao makuu.
Hadi sasa ripoti yake haikuwahi kutolewa hadharani kama Kova alivyojigamba wakati akiitangaza, badala yake hivi karibuni amekuwa akitupiana mpira na wakuu wake kuhusu ripoti hiyo.
Dk. Ulimboka kwa kiapo aliwataja watu aliowatuhumu kuhusika na tukio hilo, mmoja wao akiwa ni ofisa usalama wa taifa-Ikulu lakini hakuwahi kufanyiwa gwaride la utambuzi wala kuhojiwa na kamati hiyo ya uchunguzi.
Siku chache kabla ya Dk. Ulimboka kumtaja ofisa huyo, gazeti la MwanaHalisi lilichapisha habari iliyoeleza tukio zima lakini serikali ikalifungia kwa muda usiojulikana kwa kile kinachoitwa kosa la uchochezi.
Tukio hilo la Dk. Ulimboka limekuwa kama sinema kwani hata mtuhumiwa pekee raia wa Kenya, Joshua Mulundi, aliyekuwa amekamatwa na kuwekwa ndani kwa muda kadhaa na kufunguliwa kesi, ukamatwaji wake ulikuwa wa kutia mashaka.
Wakati vinywa vya wananchi vikiwa bado vinatafakari unyama huo, tasnia ya habari nayo iliingiliwa kwa kushambuliwa kiongozi wa wahariri katika tukio kama lilelile la Dk. Ulimboka.
Matukio haya ni kama ya kupangwa kutokana na kufanyika kwa ustadi wa hali ya juu na kwa muda mfupi tena bila wahusika kuchukua chochote kwa mteswaji.
Kama ilivyokuwa kwa Dk. Ulimboka, pia kwa Kibanda, iliundwa kamati ya uchunguzi iliyoongozwa na wataalam wakiwemo walewale walioshindwa kuwakamata watesaji wa Dk. Ulimboka.
Hadi leo hakuna mtuhumiwa hata mmoja ametiwa nguvumi na jeshi la polisi ambalo kila siku viongozi wake wamekuwa wakijinasibu kuwa na intelijensia ya hali ya juu inayobaini matukio ya kihalifu kabla ya kutokea, mathalani kuzuia maandamano na mikutano ya vyama kwa madai ya kuepusha vurugu.
-tanzania daima

MATAPELI WAKAMATWA NA KITAMBULISHO CHA USALAMA WA TAIFA KATIKA HARAKATI ZA KUTAKA KUMTAPELI MWANAFUNZI...


 Kava ya nje ya Kitambulisho hicho kinaonekana namna hii.
Watu wawili wanaotuhumiwa kuwa ni wezi a.k.a Wapigaji/Matapeli wamekamatwa usiku huu kwenye hoteli ya Picolo,Kawe jijini Dar es Salaam.

Watu hao ambao wamekamatwa ni Bw. Takula Mayenga mkazi wa Mbezi Temboni na Bw. Juma Hamis ambaye ni mkazi wa Tabata wakiwa na nyaraka tofauti ikiwemo kitambulisho kinachotaja kuwa ni cha Idara ya Usalama wa Taifa, kadi za benki pamoja na simu zaidi ya kumi,wakiwa katika harakati za kumtapeli mwanadada mmoja aliejitambulisha kwa jina la Rebecca ambaye ni Mwanafunzi wa Chuo cha Biashara cha CBE,Mkazi wa Mbezi Beach jijini Dar es Salaa .

Akisimulia tukio dada huyo ambaye alipatwa na tukio hilo la kutapeliwa Ijumaa ya wiki iliyopita alisema kuwa, ilikuwa ni Ijumaa iliyopita wakiwa wamekaa katika fukwe wakipunga upepo ndipo alipokuja tapeli huyo na kukaa nao na baadae aliwawekea madawa ya kulevya na kuondoka na dada huyo kwenda kumtupa baharini.
 Watuhumiwa hao wakiwa chini ya Ulinzi wa Polisi.
 Kitambulisho hicho kinavyoonekana kwa nyuma.
 Mtuhumiwa wa Uwizi aliejitambulisha kwa jina la Juma Hamis huku akiwa na Kitambulisho cha Kazi cha Idara ya Usalama wa Taifa chenye jina la Kenedy Magige.
kwa picha zaidi bofya soma zaidi
 Mtuhumiwa mwenza wa Tukio hilo la Wizi,aliejitambulisha kwa jina la Takula Manyenga mwenye umri wa Miaka 28,akidhibitiwa kwa kufungwa kamba mara baada ya kukamatwa Usiku huu kwenye Hoteli ya Picolo,Kawe jijini Dar es Salaam.
 Watuhumiwa wote wawili wakipakiwa ndani ya Gari la Polisi kutoka katika Kituo cha Kawe,Jijini Dar es Salaam.
 Askari Polisi wakiwa eneo la tukuo kuhakikisha Usalama unapatikana eneo hilo.
 Askari Polisi wakiwa na Watuhumiwa hao wakati wakiendelea na Ukaguzi ndani ya Gari hilo aina ya Toyota Prado lenye nambari za Usajili T 445 BCY.
 Askari Polisi wakiendelea na Ukaguzi ndani ya Gari hilo,ambapo ndani ya Gari hilo kulikutwa na Simu zaidi ya kumi ambazo zilichukuliwa na Polisi hao.
 Gari walilokuwa wakilitumia Watuhumiwa hao.
 
 Ulinzi mkali kwa watuhumiwa hao.
Msafara wa kuelekea kituoni.
Picha kwa hisani ya Michuzi Blog

MTUHUMIWA UGAIDI KENYA ALIPITIA ARUSHA…



 
  • Shambulio hilo ni la pili kufanyika kwenye maeneo mawili tofauti ndani ya saa 24, baada ya lingine lililofanyika kwenye Mji wa Wajir, muda mfupi baada ya taarifa za kudhibitiwa kwa watu wanaodhaniwa kuwa magaidi walioshambulia jengo la kibiashara la Westgate mjini Nairobi.

Nairobi. Wakati Serikali ya Kenya imeliomba Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) kumkamata Mwingereza Samantha Lewthwaite (pichani), taarifa zinadai kuwa mwanamke huyo alipitia mpaka wa Namanga, Arusha kwenda Nairobi ambako anahusishwa na tukio la ugaidi.
Lewthwaite, ambaye ni maarufu kwa jina la ‘Mjane mweupe’ inaaminika anashirikiana na kundi la magaidi la Al-Shabab la Somalia.
Kundi hilo ndilo linaaminika lilihusika na mashambulizi kwenye jengo la Westgate jijini Nairobi, wikiendi iliyopita.
Hata hivyo, taarifa ya Interpol ilisema kuwa alikuwa anatakiwa kujibu mashtaka ya kumiliki mabomu na kupanga njama za ugaidi Desemba 2011.
Interpol haikuhusisha maombi hayo ya Serikali ya Kenya na mashambulizi ya Nairobi.
Pia Lewthwaite inasemekana aliingia nchini humo kwa kutumia mpaka wa Tanzania.
Baadhi ya vyombo vya habari vya Afrika ya Kusini, vinasema mwanamke huyo alitumia pasi ya kusafiri ya nchi hiyo kuingia Kenya kwa kutumia mpaka wa Namanga uliopo mkoani Arusha.
Taarifa hizo zinasema mwanamke huyo alitumia mpaka wa Lunga Lunga na Namanga kati ya Februari na Agosti mwaka 2011 akitumia jina la Webb.
Habari hizo zinaeleza kuwa, awali mwanamke huyo alikuwa anaishi Afrika Kusini ambako aliweza kukopeshwa fedha benki na kuweza kupanga sehemu ya kuishi.
Wakati huohuo, watu wanaodhaniwa kuwa magaidi wamefanya shambulio kwenye Kituo cha Polisi mjini Mandera na kuua askari wawili, kujeruhi watatu kisha kuchoma zaidi ya magari 11 jana asubuhi.
Shambulio hilo ni la pili kufanyika kwenye maeneo mawili tofauti ndani ya saa 24, baada ya lingine lililofanyika kwenye Mji wa Wajir, muda mfupi baada ya taarifa za kudhibitiwa kwa watu wanaodhaniwa kuwa magaidi walioshambulia jengo la kibiashara la Westgate mjini Nairobi.
Shambulio hilo limefanyika wakati kikosi maalumu cha wataalamu wa mabaki ya mabomu wa Kenya na wale wa kimataifa kikianza kufanya upekuzi wa jengo hilo, ili kubaini wahusika halisi wa shambulio hilo na aina ya silaha zilizotumiwa.
-MWANANCHI.

Wakuu wa usalama kuhojiwa Kenya...


Sehemu ya jengo la Westgate iliyoporomoka
Maafisa wakuu wa ujasusi wametakiwa kufika mbele ya kamati ya ulinzi ya bunge ili kuhojiwa kuhusu mashambulizi ya kigaidi dhidi ya jumba la Westgate mjini Nairobi.
Taarifa kwenye vyombo vya habari nchini humo zinaonyesha kuwa hali ya kulaumiana imeanza kuibuka huku mashirika ya usalama yakinyosheana kidole.
Watu 67 waliuawa kwenye shambulizi hilo huku zaidi ya miamoja sabini na tano wakipata majeraha mabaya. Shirika la Red Cross nalo linasema kuwa watu 61 wangali hawajulikani waliko.
Wataalamu wa uchunguzi wa mauaji wangali wanafanya uchunguzi wao wakitafuta miili na dalili za kilichosababisha shambulizi hilo.
Kamati ya bunge inataka maafisa wanaohusika na maswala ya usalama waweze kuwajibishwa.
Kundi la kigaidi la nchini Somalia, al-Shabab limedai kufanya mashambulizi hayo yaliyodumu siku nne kama hatua ya kulipiza kisasi kwa Kenya kujihusisha nchini Somalia kijeshi.
Hii leo ni siku ya tatu ya maombolezi kwa wathiriwa wa shambulizi hilo wakiwemo raia na wanajeshi.
Rais Uhuru Kenyatta amehudhuria mazishi ya mpwa wake na mchumba wake mjini Nairobi ambapo aliwahutubia waumini.

Walipuuza onyo?

Hatua ya kuwataka maafisa hao wa usalama kufika mbele ya tume ya bunge siku ya Jumatatu, inakuja kutokana na wasiwasi miongoni mwa wakenya kuhusu kiwango cha maafisa hao kujiandaa kwa tukio lolote la kigaidi sawa na lililotokea Westgate.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari mmoja wa maafisa waliotakiwa kufika mbele ya kamati hiyo ni mkuu wa shirika la ujasusi Michael Gichangi, anayesema alitoa taarifa za ujasusi kuhusu shambulizi hilo kwa polisi.
Lakini, afisaa mmoja mkuu katika idara ya polisi alikana kuwa taarifa hiyo ilitolewa kwa polisi.
-BBC

MAKUNDI YA KIGAIDI YAPANGA KUVAMIA FAINALI ZA MISS WORLD 2013 AMBAYO YAMEPANGWA KUFANYIKA NCHINI INDONESIA...

 
Hali ya usalama katika kisiwa cha Bali nchini Indonesia ambako shindano la Miss World 2013 litafanyika Jumamosi hii, imeendelea kuwa hatiani kutokana na vitisho kutoka kwa wanaharakati wa dini ya Kiislamu wanaotishia kulishambulia.
000_hkg8989120.si Wanawake wa Kiislamu wakiandamana dhidi ya shindano ka Miss World huko Banda Aceh, kwenye kisiwa cha Kaskazini cha Sumatra, September 14, 2013

Kutokana na Indonesia kuwa nchi yenye Waislamu wengi duniani, waandaaji wa shindano hilo walilazimika kulihamisha kutoka kwenye mji mkuu, Jakarta hadi kisiwani Bali. 

Lakini hata hivyo mambo hayajapoa bado na wanaharakati hao wamepanga kufanya maandamano mengine Jumamosi na kuvunja vizuizi vya ulinzi mkali kwenye shindano hilo.
1375084_10151957434219974_1998112413_n
Zaidi ya asilimia 90 ya watu milioni 240 wa nchini humo ni waislamu.
 
Waislamu wanapinga shindano hilo kufanyika nchini mwao na wakiliita shindano hilo kama la ngono na umal*ya. Pamoja na waandaaji wa shindano hilo ambao makazi yao ni Uingereza kuahidi kulioandoa shindano la bikini na washiriki kuvaa nguo zinazoziba mwili, waandamanaji hao hawakuridhika na kuendelea kuwataka walipeleke kwingine.
1377298_10151957436454974_1137514725_n
Mapema mwaka huu, mamia wa wanaharakati wa kundi la Islamic Defenders Front walijaribu kuvamia kisiwani Bali lakini polisi walikabiliana na kundi hilo na kulizuia kupanda ferry ya kwenda kisiwani humo.
 
Balozi za Marekani, Uingereza na Australia tayari zimeonya kuwa wanaharakati hao wanaweza kulishambulia shindano hilo na kukumbushia tukio la Jihad la ulipuaji wa bomu mwaka 2012 lililosababisha vifo vya watu 200.
 
Mwaka jana, Lady Gaga aliahirisha concert yake mjini Jakarta baada ya kuzuka maandamano kama hayo kuipinga na kumuita ‘mjumbe wa shetani’ anayevaa sidiria na chupi tu. 

Islamic Defenders Front walitishia kumzuia Lady Gaga asishuke kutoka kwenye ndege na wangeuchoma ukumbi ambako diva huyo wa “Poker Face” angetumbuiza.
 
Zaidi ya warembo 129 duniani watashiriki kwenye fainali ya Miss World 2013 ambapo Tanzania inawakilishwa na Brigitte Alfred. Zaidi ya walinzi 700 watakuwa wakifanya doria kwenye eneo la tukio kuhakikisha usalama wa washiriki na wageni.

MAANDAMANO YA CHADEMA, CUF NA NCCR YAPIGWA MARUFUKU JIJINI DAR ES SALAAM...

Jeshi la Polisi Jijini Dar es Salaam limepiga marufuku maandamano ya umoja wa vyama vya CUF, NCCR na CHADEMA siku ya Jumamosi yaliyokuwa yamepangwa  kuanzia Tazara hadi Jangwani na Mwenge hadi Jangwani na sehemu mbalimbali ...

Taarifa  iliyotolewa  na kamanda Kova  kupitia  ITV   imeeleza  kuwa  Polisi wamechunguza na kugundua kwamba  maandamano  hayo  yataleta usumbufu kwa watu wengine na kwamba kwa kuwa lengo ni kufika Jangwani basi Viongozi wa vyama hivyo wawaambie wafuasi wao waende Jangwani bila Maandamano.

TEC yataka Kamishna wa Polisi Z’bar afukuzwe kazi...


Padri Joseph Magamba wa Kanisa Katoliki Parokia ya Machui Zanzibar aliyemwagiwa tindikali akisaidiwa kushuka kwenye ndege na Padri Thomas Assenga(kushoto) wa Kanisa la Mtakatifu Joseph Zanzibar baada ya kuwasili kwenye uwanja wa Julius Nyerere Dar es Salaam jana kuelekea katika hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.Picha na Fidelis Felix 

Dar es Salaam. Tukio la kumwagiwa tindikali  Padri wa Kanisa la Romani Katoliki Parokia ya Machui, Joseph Mwang’amba huko Zanzibar limechukua sura mpya baada ya  Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC) kumtaka Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa kufukuzwa kazi.
Makamu  Rais wa TEC, Askofu Severine Niwemugizi aliliambia gazeti hili jana kuwa anapaswa kuondolewa kwa sababu ya kukithiri kwa matukio hayo visiwani.
Askofu Niwemugizi alisema kamanda huyo anapaswa kuchukuliwa hatua kwa kuwa ameshindwa kukamata watu wanaofanya vitendo viovu dhidi ya viongozi wa dini.
Kwa upande wake Kamishna Mussa alisisitiza hawezi kujiuzulu na kwamba anayestahili kulaumiwa ni Mkurugugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa sababu kwa upande wake alishawakamata watuhumiwa wa matukio hayo.
“Kazi yangu mimi ni kupeleleza na kukamata watuhumiwa,ila kazi ya kushitaki watu ni ya DPP hivyo mimi siyo wa kulaumiwa’Alisema .
Hili ni tukio la nne la uhalifu dhidi ya viongozi wa dini huko Zanzibar baada ya kuuawa kwa Padri Evarist Mushi wakati Padri Ambrose Mkenda alipigwa risasi na Katibu wa Mufti, Sheikh Fadhili Soraga alimwagiwa tindikali.
  Katika hatua nyingine, Askofu Niwemugizi alisema kuwa matukio hayo kwa sasa yamekuwa wazi kwamba ni mpango wa kuangamiza Ukristo na Wakristo kwa ujumla katika Visiwa vya Zanzibar.
“Uchochezi umefanywa wa kuhamasisha chuki dhidi ya Ukristo unasikitisha. Tulikaa kama Wakristo tukaiambia Serikali mambo ambayo inaweza kufanya kukomesha vitendo hivi, lakini hadi sasa hakuna lililotekelezwa,” alisema na kuongeza: 
“Awali ilielezwa kwamba siyo sababu ya kidini,  watu wa Kikundi cha Uamsho ndiyo walioanzisha moto huo na wanauendeleza, hali inatisha zaidi kwamba hata jamii ya Wazanzibar haionyeshi nia ya kushiriki kukomesha ukatili huu, kama huyu Padri Mwang’amba amemwagiwa kwenye kituo cha intaneti ni eneo ambao lina watu mbona mhusika hajakamatwa? alihoji.
Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Kamati ya Haki na Maadili kwa Jamii kwa Viongozi wa Dini ya Kikristo, Mchungaji William Mwamalanga alisema kuwa Kamishna huyo wa Polisi anatakiwa kufukuzwa kazi kwa kuwa anaichafua Zanzibar kwa kushindwa kudhibiti matukio hayo ya uhalifu kwa makusudi, pia amejaa udini.
-mwananchi

ALEX MASSAWE KUTUA DAR RASMI...

MFANYABIASHARA maarufu nchini, Alex Massawe anatarajiwa kutua nchini mwishoni mwa mwezi huu na kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Tanzania. Mkuu wa Interpol, Tawi la Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav Babile, aliiambia MTANZANIA jana kuwa taratibu za kumrejesha Massawe nchini zimekamilika na hakuna vikwazo vitakavyosababisha asiletwe kujibu tuhuma zinazomkabili.

Kamishna Babile alisema tuhuma zinazomkabili Massawe alizitenda akiwa katika ardhi ya Tanzania, hivyo ni lazima ajibu tuhuma hizo katika ardhi ya Tanzania na si vinginevyo.

Alisema taarifa za kupandishwa kizimbani Massawe katika Mahakama ya Dubai, hazikuwa sahihi na kusisitiza hakuna mabadiliko katika taratibu zinazofanywa kumrejesha nchini ili aweze kujibu tuhuma zake.

“Process (mchakato) unaendelea vizuri, kamwe hakuna mabadiliko wala vikwazo, katika kipindi cha mwisho wa mwezi huu, anaweza kuwa nchini.

Babile alisema Serikali ya Dubai (UAE), haiwezi kumfungulia mashitaka Massawe, kwa makosa aliyoyafanya akiwa Tanzania.

“Hawezi kuhukumiwa kule, kwa sababu hawezi kufunguliwa mashitaka Uarabuni kwa makosa aliyoyafanya Tanzania,” alisema Babile.

Hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari (si MTANZANIA) viliripoti kuwa mfanyabiashara huyo amefikishwa katika mahakama ya Dubai, akikabiliwa na tuhuma za mauaji, baada ya Polisi wa Kimataifa (Interpol), kuiomba Serikali ya nchi hiyo kumkamata.

Massawe anayefanya biashara zake katika miji ya Arusha, Moshi na Dar es Salaam, alikamatwa kati ya Juni, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai, akitokea Afrika Kusini.

Akiwa Dubai, Massawe alikutwa na hati za kusafiria (Passport) tatu bandia zilizokuwa na majina tofauti, wakati alama zake za vidole zikitambua jina lake halisi.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imethibitisha kuwa taratibu za kumrejesha nchini, Alex Massawe zimekamilika na kuongeza taratibu hizo zinafanywa kwa karibu sana kati ya Jeshi la Polisi.

Msemaji wa wizara hiyo, Mkumbwa Ali aliiambia MTANZANIA juzi kuwa Massawe alitiwa mbaroni baada ya kufanyika taratibu za kipolisi wa Tanzania, kuwataarifu Interpol juu ya kutafutwa kwa mtuhumiwa huyo.

“Si kwamba unaofanyika ni utaratibu wa kumrejesha kwa makubaliano ya kubadilishana wafungwa au watuhumiwa, Tanzania hatuna utaratibu wa kubadilishana wafungwa na Dubai, hizi ni taratibu za kipolisi.

“Imetolewa taarifa na Polisi Tanzania kwamba, huyu ni Wanted (anatafutwa) na ikitolewa taarifa hizo mtuhumiwa anawekwa katika rekodi na kukamatwa,” alisema.

Massawe anatuhumiwa kufanya uhalifu mbalimbali, ikiwamo kughushi nyaraka mbalimbali na tayari Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imetoa hati ya kukamatwa na kurejeshwa nchini Massawe, ili kujibu mashitaka yake.
-MTANZANIA

JWTZ LATOA ONYO KALI KWA VYOMBO VYA HABARI VINAVYOANDIKA HABARI ZA UONGO KUHUSU MZOZO WA DRC...

JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limevitaka vyombo vya habari kuacha kuandika taarifa za mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), badala yake taarifa rasmi zitakuwa zikitolewa na jeshi hilo kila baada ya wiki mbili.


Katazo hilo limetolewa jana jijini Dar es Salaam na Meja Erick Komba wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya mgogoro huo.

Alisema hali hiyo inatokana na jeshi hilo kubaini kuwa baadhi ya vyombo vya habari nchini vinaandika habari za uchochezi zinazotaka kuziingiza vitani nchi ya Tanzania na Rwanda.

Meja Komba alisema hategemei kama kutakuwa na chombo chochote cha habari kitakachotoa habari kuhusu maendeleo ya mgogoro huo bila kupata taarifa rasmi kutoka jeshi hilo.

Alionya kuwa chombo chochote kitakachokwenda kinyume kitakuwa kina tatizo.
Meja Komba alisema wananchi wanapaswa kuelezwa kuwa kikosi cha Tanzania kilichoko DRC ni sehemu ya Brigedia ya SADC, iliyotoa mchango wake katika Jeshi la Umoja wa Mataifa (Monusco).

Alitaja majukumu ya kikosi hicho kuwa ni kuzuia waasi wa M23 na wengine kujitanua, kuvunja nguvu zao na kuyapokonya silaha makundi yote ya waasi.
“Kwa kuzingatia kuwa kikosi chetu kiko chini ya majeshi ya Monusco, inamaanisha kuwa operesheni hiyo ni ya Umoja wa Mataifa,” alisema.

Aliongeza kuwa Tanzania haikupeleka kikosi chake DRC kwa ajili ya kupigana na M23, pia ieleweke kuwa haina tatizo na Rwanda kuhusiana na operesheni hiyo ambapo Rwanda ilitoa ridhaa kikosi cha Tanzania kwenda DRC.

Meja Komba alisema Rwanda ni miongoni mwa wanachama wa nchi za Maziwa Makuu, ambayo imesaidia kwa kuruhusu kikosi cha Tanzania kupitisha vifaa na zana katika nchi yake kupeleka DRC.

“Tanzania inashiriki katika operesheni hiyo ya ulinzi wa amani nchini DRC kutokana na mgogoro kati ya serikali na waasi hususan kikundi cha M23,” alisema.
Mgogoro huo ulianza Aprili mwaka jana, ambapo kikundi cha M23 kilijitoa katika jeshi la serikali na kuanzisha mapigano yaliyosababisha hali ya usalama nchini DRC kuwa mbaya.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe Benard, amesema kuwa marais Jakaya Kikwete na Paul Kagame wa Rwanda wamemaliza tofauti zilizokuwa zimejitokeza kati yao hivi karibuni.
Marais hao walikutana na kufanya kikao cha faragha jijini Kampala nchini Uganda juzi baada ya mkutano wa viongozi wa nchi za Maziwa Makuu na baadaye kutoa taarifa kwa waandishi wa habari.

Kuzorota kwa mahusiano kati ya viongozi hao kulikuja kufuatia kauli ya Rais Kikwete ya kumtaka Rais Kagame kukaa meza moja na vikundi vya waasi wa nchi yake vilivyo nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ushauri ulioonekana kumkera Rais Kagame.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Membe alisema marais hao walitumia mazungumzo yao yaliyochukua muda wa saa moja kujadiliana na kueleweshana mambo mbalimbali yaliyosababisha kutoelewana.
“Baada ya mkutano huo ambao uliwapa fursa za kuchambua, kujadili na kurejesha mahusiano ya kihistoria kati ya nchi hizi mbili, marais wetu walitoka na nyuso za furaha,” alisema.

Moja ya maazimio ya kikao chao ni kuwa na vikao vingine kati ya Rwanda na Tanzania katika siku zijazo.

“Kwa kweli kikao kati ya Rais Kikwete na Rais Kagame kimeondoa majungu yote, kimekata fitina, uongo na maneno ya kuchombeza yaliyokuwa yakitawanywa na watu mbalimbali hapa nchini na hata kule Kigali,” alisema.

Mbali ya kikao hicho pia Rais Kikwete alifanya kikao kingine cha faragha na Rais wa Uganda Yoweri Museveni ambapo walipata muda wa kujadiliana kwa kina kuhusu mambo mbalimbali kuhusu nchi zao na mambo ya migogoro katika nchi za Maziwa Makuu.

Akizungumzia yale yaliyokubaliwa katika mkutano wa viongozi wa nchi za Maziwa Makuu, Membe alisema kuwa mkutano huo kwanza ulimruhusu Rais Museveni aendelee kusuluhisha vita ya serikali ya DRC na waasi.

Alisema kuwa viongozi hao walilaani mashambulizi ya M23 yaliyojeruhi na kumuua Meja Mshindo wa Tanzania aliyekuwa miongoni mwa askari walioko nchini Congo katika kusimamia amani chini ya Umoja wa Mataifa.

WAASI WA M23 WAANZA KUSALIMU AMRI BAADA YA KUPEWA KICHAPO KIKALI NA JWTZ ( MONUSCO)...


Waasi wa M23 Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamesema kuwa watasitisha mapigano, kufuatia makabiliano makali na wanajeshi wa serikali wanaoungwa mkono na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa ikiwemo  JWTZ.
 
Afisa mmoja wa Kundi hilo la M23 Museveni Sendugo, ameiambia BBC kuwa wanajeshi wake tayari wamerudi nyuma umbali wa kilomita tano kutoka eneo la mapigano.

Wengi wa wapiganaji wa M23 ni wanajeshi walioasi jeshi la serikali, wengi wao wakiwa wa kibila la Kitutsi sawa na uongozi wa Rwanda.
 
Serikali ya DRC na Umoja wa Mataifa zimeishutumu serikali ya Rwanda kwa kuwaunga mkono wapiganaji wa kundi hilo la M23, tuhuma ambazo zimekanushwa na utawala wa Kigali.

Awali, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametoa wito kwa rais wa Rwanda, kuwa mvumilivu huku uhasama kati yake na nchi jirani ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ukiendelea kutokota katika maeneo ya mipakani.

Bwana Ban, alizungumza na rais Paul Kagame baada ya serikali yake kuishutumu Congo, kwa kufanya shambulio katika ardhi yake makusudi na kumuua mama mmoja na kumjeruhi mtoto wake.
 
Msaidizi wa katibu huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa, amenukuliwa akiiambia Umoja wa Mataifa kuwa wapiganaji wa kundi la waasi wa M23, wameonekana wakirusha makombora wakilenga Rwanda.
 
Serikali ya DRC na Umoja wa Mataifa zimeshutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi hao wa M23, madai ambayo yamepingwa vikali ya utawala wa Kigali.
 
Wanajeshi wa Congo wakishirikiana na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa, wamekuwa wakifanya mashambulio dhidi ya waasi hao wa M23 karibu na mpaka wa Rwanda, tangu wiki iliyopita.

Waasi walengwa na UN

Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kutunza amani nchini DRC, Monusco, kiliimarishwa zaidi pale wanajeshi elfu tatu zaidi walipotumwa nchini humo kupambana na waasi hao.

Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Louise Mushikiwabo, amesema mabomu na makombora kumi na tatu yalirushwa katika ardhi yake siku ya Jumatano na mengine kumi siku ya Alhamisi.

Waziri huyo amedai kuwa kufikia sasa wanajeshi hao wa Congo wamefanya mashambulio thelathini na nne nchini Rwanda.
 
Amewashutumu wanajeshi wa DRC kwa kuwalenga raia wake na kusisitiza kuwa kwa sasa wanajiepusha kulipisa kisasi lakini hawatasita kujibu ikiwa uchokozi huo hautakoma.

Msemaji wa jeshi la Congo Kanali Olivier Hamuli ameiambia BBC kuwa jeshi lake haliwezi kurusha makombora kulenga maeneo yanayokaliwa na raia.
 
''Waasi ndio wanaoweza kufanya kitendo kama hicho, wapiganaji wa M23 na wala sio wanajeshi wake ndio waliokuwa katika eneo ambalo makombora hayo yalirushwa'' Alisema Kanali Hamuli.
 
Matamshi hayo yaliungwa mkono na msaidizi wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Mulet ambaye aliiambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa, wanajeshi wake nchini DRC walishuhudia wapiganaji wa M23, wakirusha makombora wakilenga Rwanda na wala sio wanajeshi wa Congo.
 
Takriban watu laki nane wamekimbia makwaoi nchini Congo tangu waasi hao wa M23 kuanzisha mashambulio katika eneo la Mashariki mwa Congo Aprili mwaka wa 20120.

-BBC

EAC YAINGILIA KATI MZOZO WA TANZANIA NA RWANDA...


Wakati Tanzania ikisema kuwa iko tayari kukaa meza moja na jirani yake Rwanda kumaliza hali ya uhasama iliyoanza kujitokeza katika siku za hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk Richard Sezibera amesema jitihada za kidipolomasia zinafanyika kutatua tofauti hizo za kimawazo. 
 
Bila kutaja taasisi wala wanaohusika katika jitihada hizo za kidiplomasia, Dk Sezibera aliwaambia waandishi wa habari jijini Arusha jana kuwa jitihada hizo zinafanyika kimya kimya bila kushirikisha vyombo vya habari “Migongano na tofauti za kimtazamo miongoni mwa viongozi wakuu wa nchi wanachama wa EAC ni jambo lisilo la afya kwa Jumuiya na linastahili kushughulikiwa kidiplomasia,” alisema Dk Sezibera.
 

Akizungumza kwa tahadhari kubwa kukwepa kuingia kwa undani kuhusu suala hilo, Katibu Mkuu huyo alisema inafaa kila linalowezekana lifanyike kutatua mgongano wowote unaotokea kati ya viongozi wakuu.
 

Mjini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe naye alisema katika mahojiano kuwa iwapo Rwanda itaomba kukutana na Tanzania kwa ajili ya kumaliza mzozo huo Serikali itakuwa tayari kutoa ushirikiano.
 

“Tanzania tunaona kuwa hii itakuwa njia ya busara zaidi kumaliza tofauti zetu kwa njia ya mazungumzo badala ya kuendelea kuishi kwa uhasama” alisema Membe na kwamba hali ya ujirani mwema na tofauti zetu tuzimalize kwa njia ya mazungumzo.”
 

Waziri Membe alisema siyo jambo la busara kuacha mzozo huo ukakaamuliwa na mataifa ya nje ili hali nchi zenyewe bado zinafursa nzuri ya kukaa mezani na kujadiliana namna ya kutafutia ufumbuzi mzozo huo.
 

Uhusiano wa Tanzania na Rwanda unatajwa kuwa katika wakati mgumu kutokana na kauli za majibizano baina ya viongozi wa pande zote mbili. Hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete aliisihi Rwanda kutotoa kauli za kejeli kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kuhatarisha uhusiano uliodumu kwa muda mrefu .
 

Hata hivyo, Dk Sezibera alisema tofauti na migongano kati ya viongozi haiwezi kuathiri wala kuvunja Jumuiya ya sasa ya Afrika Mashariki kama ilivyotokea kwenye Jumuiya ya awali mwaka 1977 kutokana utofauti wa muundo na misingi ya Jumuiya ya sasa.
 

“Jambo lililo dhahiri ni kwamba tofauti za kimtazamo kati ya viongozi wa nchi wanachama (Kikwete na Kagame), haziwezi kuhatarisha uhai wa Jumuiya ya Afrika Mashairiki kwa sababu muungano huu umejengwa katika muundo na misingi imara tofauti na ule (jumuiya) wa zamani,” alisema Dk Sezibera

-Mwananch

MKUU WA FFU - ARUSHA NA POLISI WENGINE WATATU WAFUKUZWA KAZI ...


 Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Emmanuel Nchimbi amewavua madaraka Maafisa wanne wa Jeshi la Polisi nchini na kumsimamisha kazi mmoja ambaye atafunguliwa mashtaka ya kijeshi kutokana na kukiuka maadili na taratibu za jeshi hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Waziri Nchimbi amesema hatua hiyo ni katika kuendeleza vita ya kuhakikisha kuwa jeshi la polisi linakuwa na nidhamu, linatekeleza wajibu wake wa kutenda haki na kuwalinda raia na mali zao.

Alisema amewachukulia hatua Maafisa hao baada ya kuridhia maoni ya kamati aliyoiunda kufanya uchunguzi wa matukio yaliyolalamikiwa dhidi ya askari polisi katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro na Kigoma kati ya Desemba 2012 na Mei, 2013.

Waziri Nchimbi aliwataja waliovuliwa madaraka kuwa ni Mkuu wa kikosi cha kutuliza ghasia mkoani Arusha Mrakibu wa Polisi Ramadhan Giro, Mkuu wa Upelelezi wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro Inspekta Jamal Ramadhan, Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Dumila Inspekta Juma Mpamba na mkuu wa upelelezi wa wilaya ya 


Kasulu ASP Daniel Bendarugaho na kumsimamisha kazi Inspekta Isaack Manoni.

Alifafanua kuwa  Mrakibu wa Polisi Ramadhan Giro alivuliwa madaraka kwa kushindwa kusimamia kikamilifu askari na maafisa walio chini yake ambao walikamatwa wakisafirisha bangi yenye uzito wa kilogramu 540 kwa kutumia gari la polisi.

Alisema askari hao wawili waliokamatwa wakisafirisha bangi, walikuwa wakifanya kazi kwenye kituo cha Ngarananyuki na baada ya kukiri kosa walifukuzwa kazi mwezi Mei mwaka huu.

Alisema kwa upande wa Inspekta Jamal Ramadhan amevuliwa madaraka yake kwa kutochukua hatua stahiki baada ya kupata taarifa za mfanyabiashara wa Mvomero Samson Mwita kubambikiwa fuvu la kichwa cha binadamu na askari polisi watatu wakishirikiana na matapeli wawili.

“Katika tukio hilo Inspekta Isaack Manoni amesimamishwa kazi na atashtakiwa kijeshi kutokana na tuhuma za kumtorosha mtuhumiwa, Cpl. Edward aliyekuwa dereva wa gari la Polisi lililokamatwa na bangi kitendo ambacho kimelifedhehesha jeshi la polisi” alisema Waziri Nchimbi.

Alibainisha kuwa Inspekta Juma Mpamba amevuliwa madaraka hayo kwa kuonesha udhaifu katika utendaji wake wa kazi kwa kutosimamia kikamilifu askari walio chini yake kitendo kilichosababisha askari kujipangia kazi nje ya utaratibu na kumbambikiza mfanyabiasha huyo kesi kwa lengo la kujinufaisha kinyume na maadili ya kazi. Aliongeza kuwa askari waliohusika na tukio hilo wamefukuzwa kazi na kushtakiwa.

Waziri Nchimbi alisema ASP Daniel Bendarugaho amevuliwa madaraka kwa kutokuwa makini katika kufanya na kusimamia upelelezi wa kesi ya mauaji ya marehemu Gasper Mussa Sigwavumba aliyeuawa baada ya kupigwa na askari polisi wawili Desemba mwaka jana.

Alisema upelelezi mbovu uliofanywa chini ya usimamizi wa Mkuu huyo wa upelelezi ulisababisha kesi hiyo kuondolewa mahakamani. Aliongeza kuwa upelelezi wa kesi hiyo utaanza upya ili haki itendeke.

Popular Post

 
Support : OBAMA | OBAMA | OBAMA
Copyright © 2013. DiraYaLeo - All Rights Reserved
Template Created by Barakaeli Aremu Published by Dira Ya Leo
Proudly powered by Blogger