Home »
» ASKARI 117 WA CHUO CHA TAALUMA NA MAFUNZO YA UPOLISI WATIMULIWA CHUONI HUKO MOSHI
Posted by Unknown
Posted on Wednesday, July 24, 2013
Wanafunzi 117 wa Polisi,
wamefukuzwa katika Chuo cha Taaluma na Mafunzo ya Polisi (MPA),
kilichopo Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Waliotupiwa virago
na kufutwa kwenye kozi hiyo ni wale waliopoteza sifa za kuendelea na
mafunzo ya kijeshi baada ya kukutwa na makosa ya utovu wa nidhamu, utoro
na matatizo ya kiafya.
Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Matanga
Mbushi, ambaye ni mkuu wa chuo hicho alisema katika mahojiano maalumu
kwamba, waliotimuliwa chuoni ni kati ya askari wanafunzi 3,189 waliokuwa
wamesajiliwa kuanza mafunzo ya kijeshi katika chuo hicho, Oktoba 25
mwaka jana.
Kati yao askari 115 ni wale wa Polisi na askari wawili
wanatoka katika Idara ya Uhamiaji iliyopo chini ya Wizara ya Mambo ya
Ndani.
Kufukuzwa kwa wanafunzi hao , kuna akisi moja kwa moja jinsi
menejimenti ya chuo hicho ilivyojipanga upya kupunguza wimbi la baadhi
ya askari walioko kazini na ambao wanalipaka matope jeshi hilo kutokana
na kupotoka kimaadili kwa kutaka kujinufaisha kimaslahi.
Askari
hao walikuwa waungane na wenzao ambao wanatarajiwa kuhitimu mafunzo ya
awali ya polisi na uhamiaji, Julai 26 mwaka huu baada ya kupatiwa
mafunzo ya medani za kivita. Mgeni wa heshima atakayeshuhudia kuagwa kwa
askari 3,092 ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Kamishna
Mbushi alisema askari hao pamoja na mambo mengine wamepatiwa mafunzo
maalumu ya utunzaji wa amani ya nchi iliyopo, Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (ICT), Haki za Binadamu, Masuala ya mtambuka (Cross cutting
issues), Usimamizi wa majanga na Usimamizi wa kazi za Polisi.
Mafunzo
mengine ni pamoja na Polisi Jamii, Sheria ya ushahidi, Sheria ya
mwenendo wa makosa ya jinai, Upelelezi wa makosa ya jinai, Usalama
barabarani na stadi za kazi.
Taarifa za awali kutoka ndani ya
chuo hicho, zinaeleza kuwa mahafali hayo ya Polisi yatatanguliwa na
medani za kivita yatakayofanyika Julai 25 huko katika Kijiji cha
Kilele-Pori, Wilaya ya Siha.
CHANZO: HABARI LEO