Serikali imeendelea kuwasisitizia wazazi na wanafunzi
shuleni kuwa wanafunzi wote 136,000 waliofeli kidato cha pili mwaka jana
na kutakiwa kurudia darasa hilo wanapaswa kufanya hivyo bila
kushurutishwa.Imesema wasijidanganye kuwa watafanya mitihani ya kumaliza
kidato cha nne mwakani kwani namba zao hazipo.
Pia wanafunzi hao wasije wakarubuniwa na baadhi ya
walimu wakuu wa sekondari nchini kuwa licha ya kufeli kwao wanaweza
kuendelea na kidato cha tatu mwaka huu kwani hawataweza kufanya mitihani
ya Taifa ya kidato cha nne mwakani kama wanavyodhani kutokana na namba
na majina yao tayari zimeondolewa katika orodha hiyo ya mwakani.
Tahadhari hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo wakati akifungua mafunzo ya
Waratibu Elimu kata Kitaifa yanayoendeshwa na Wakala wa Maendeleo ya
Uongozi wa Elimu (ADEM) huko wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Mulugo alisema ana taarifa ya kuwapo kwa baadhi ya
wanafunzi kati ya hao 136,000 ambao wameshawishiwa na wakuu wa shule
pamoja na wazazi wao kadhaa kuendelea na kidato cha tatu kwa matumaini
ya kuwa watafanya mitihani ya kumaliza kidato cha nne mwaka ujao imani
ambayo Waziri alisema itakuja kuwaliza baadaye maana kundi hilo halina
nafasi ya kuhitimu mwakani.
Kutokana na hali hiyo Naibu Waziri Mulugo
aliwaagiza waratibu elimu kata nchini wafuatilie mara moja wanafunzi
wote wa kidao cha pili waliofeli kama wamekariri darasa hilo.
Alisema wanafunzi waliokaidi na kuendelea kidato
cha tatu mwaka huu watoe taarifa mapema ili hatua za kisheria
zichukuliwe dhidi yao na walimu waliohusika na udanganyifu huo.
“Waratibu elimu kata mtakapo toka hapa kwenye
mafunzo, nawaagiza sasa mkaanze na hili la kuwakufuatilia wanafunzi
waliofeli kidato cha pili mwaka jana. kama wote wamerudia darasa au wanaendelea na kidato cha tatu,”alisema Mulugo.
Awali Ofisa Taaluma wa Mkoa wa Dar es Salaam
Benadeta Thomas alisema mafunzo hayo yanaendeshwa katika mikoa 11 nchini
na ni utekelezaji wa mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari ngazi za
kat.