Ni Shilogile wa Morogoro, yataka apishe tume huru kuchunguza tukio hilo, Moi wakwepa kuzungumzia risasi.
Dar es Salaam. Baraza Kuu la Waislamu Tanzania
(Bakwata), limelaani vikali tukio la polisi kumjeruhi Katibu wa Jumuiya
na Taasisi ya Kiislamu, Sheikh Issa Ponda na limetaka kuundwa kwa tume
huru kuchunguza tukio hilo huku likimtaka Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Morogoro, Faustine Shilogile kujiuzulu.
Ponda amelazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili
(Moi), akitibiwa majeraha yanayoaminika kuwa ya risasi aliyoyapata
Ijumaa iliyopita mkoani Morogoro.
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum
alisema baraza hilo limesikitishwa na tukio hilo na kusisitiza kwamba,
uchunguzi huru unahitajika ili kuhakikisha kuwa wahusika wote
wanakamatwa.
“Ieleweke kwamba Bakwata na Sheikh Ponda siyo
maadui. Tunatofautiana mawazo tu, linapotokea suala lisilo la haki za
binadamu lazima tuwe kitu kimoja,”... Sisi Bakwata Mkoa wa Dar es
Salaam, tumesikitishwa na tukio hilo, tunataka tume huru ya kuchunguza
kifaa kilichomjeruhi na kuwabaini wahusika ili wachukuliwe hatua za
kisheria. Polisi walitakiwa kutumia njia ya weledi katika kumkamata,
lakini siyo kumjeruhi kama ilivyotokea.”
Alisema Bakwata inamtaka Shilogile kujiuzulu mara
moja ili kupisha tume huru itakayoundwa kuchunguza kwa ufasaha juu ya
kujeruhiwa kwa Sheikh Ponda.
Alisema: “Hata kama Sheikh Ponda anatafutwa na
polisi, ungetumika weledi wa kumkamata siyo kumjeruhi. Tunaamini polisi
ina mbinu nyingi za kuwakamata wahalifu na Ponda kazunguka mikoa mingi
ikiwemo Zanzibar walishindwaje kumkamata!” alihoji Sheikh Salum.
Alisema ikithibitika kwamba Sheikh Ponda
alijeruhiwa kwa risasi au polisi walihusika, hatua kali zichukuliwe kwa
wahusika kwa sababu tukio hilo linahatarisha usalama wa nchi.
Kauli ya Sheikh Salum inafanana na ile iliyotolewa
na juzi na Amiri wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Tanzania, Sheikh
Yusuf Kundecha ambaye aliitaka Serikali kuunda tume huru kuchunguza
tukio hilo.
Hata hivyo, Polisi imeipa jukumu Kamati ya Haki
Jinai chini ya Naibu Kamishna wa Polisi, Isaya Mngulu kuanza kazi ya
kuchunguza tukio hilo.
Hatua ya polisi kuanza kuchunguza tukio hilo
imepingwa vikali na Sheikh Kundecha ambaye jana alisema haiyumkiniki
kushiriki kuchunguza tukio hilo wakati yenyewe inatuhumiwa kuhusika.
“Umeona wapi mtu anampiga mtu halafu huyohuyo
anaunda tume eti kuchunguza kipigo na aliyepiga anakuwa ndani ya tume...
hii ni sawa na Tume ya Mwangosi ambayo haikuja na majibu. Kinachotakiwa
ni kuundwa tume huru ikiwashirikisha Waislamu,” alisema.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso alisema
jana kuwa Kamati ya Haki Jinai imeshaanza kazi juzi ya kufuatilia tukio
hilo kazi kubwa ikiwa ni kuchunguza namna lilivyotokea ikiwa ni pamoja
na mazingira yake.
-MWANANCHI
-MWANANCHI