KWA mara nyingine Mahakama Kuu, imetupilia mbali mashtaka ya
ugaidi yaliyofunguliwa dhidi ya viongozi na wananchama wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Jana, Mahakama Kuu Kanda ya Tabora iliwafutia shtaka la ugaidi
wanachama watano wa CHADEMA ikisema kosa lao ni la jinai na halipaswi
kuitwa la ugaidi.
Katika uamuzi wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Simon Lukelelwa,
aliwaonya waendesha mashtaka kuacha tabia ya kutumia maneno makali ya
ugaidi katika kesi za jinai, hatua aliyosema inaogofya wageni
wanaotarajia kuja Tanzania.
“Suala hili la ugaidi kwa siku za hivi karibuni limeshika kasi,
linazungumzwa kwa mapana ndani na nje ya nchi, lakini inavyoonyesha
mazungumzo hayo hayajaeleweka undani wa madhara yake. Nchi ikiwa
imekithiri kwa ugaidi kama inavyodaiwa vitu vingi vingeathirika, uchumi,
utalii na mambo mengine.
“Ni vizuri mambo haya yakapewa nafasi yake na kwa umakini mkubwa,
yasije yakaleta madhara kwa nchi pasipo ulazima wowote. Hata neno ugaidi
tafsiri yake haijajulikana vizuri, kila mtu anatafsiri zake. Mtu
unayemuona ni gaidi, anaweza kuwa mpigania uhuru kwa mwingine,” alisema
Jaji Lukelelwa.
Hii ni mara ya pili kwa Mahakama Kuu kufuta mashtaka kama hayo kwa
viongozi wa CHADEMA ambapo Mei 8, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Dar
es Salaam ilimfutia mashtaka matatu ya ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na
Usalama wa chama hicho, Wilfred Lwakatare.
Jaji Lawrance Kaduri alitoa uamuzi huo akisema ulitokana na
kukubaliana na hoja ya mawakili wa Lwakatare, Tundu Lissu, Peter
Kibatara na Mabere Marando.
Makada hao wa CHADEMA waliofutiwa shtaka hilo la ugaidi jana mkoani
Tabora ni Henry John Kilewo, ambaye ni Katibu wa CHADEMA Wilaya ya
Kinondoni, Evodius Justinian, Oscar Kaijage, Rajabu Daniel na Seif
Magesa Kabuta.
Vijana hao walipandishwa kizimbani katika mahakama ya wilaya ya Igunga
na kusomewa mashtaka mawili, moja la ugaidi na lingine la jinai.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mawakili wao, Peter Kibatala na
Profesa Abdallah Safari walipambana kuwanusuru na mashtaka hayo.
Mawakili hao walihoji uhalali wa mashtaka hayo, wakidai kuwa hakuna
vigezo vya kutosha kuonyesha kuwa kuna ugaidi, huku pia wakihoji
utaratibu wa kuwafungulia mashtaka katika mahakama hiyo badala ya kule
walikokamatiwa.
Hivyo, waliiomba Mahakama Kuu ama iwafutie mashtaka hayo au iamuru
kila mshtakiwa arudishwe na kushtakiwa katika mahakama za mahali
walikokamatiwa.
Katika uamuzi wake, Jaji Lukelelwa aliongeza kuwa sheria za makosa ya
jinai zipo wazi na zinaelekeza na kufafanua makosa na mashtaka
yanayoweza kufunguliwa kwa wananchi wanaokwenda kinyume cha sheria
zilizotungwa.
Jaji aliamru watuhumiwa hao warejeshwe wilaya ya Igunga walikotenda
makaosa yao na wafunguliwe shtaka la kufanya matendo ya kusababisha
madhara makubwa mwilini kwa kuzingatia sheria ya mwenendo wa makosa ya
jinai.
Aliongeza kuwa hakimu atakayesikiliza shauri hilo awape dhamana kwa
kutoa masharti atakayoona yeye yanalingana na shtaka linalowakabili
watuhumiwa.
Wakili wa washtakiwa hao, Peter Kibatala, akizungumza na waandishi wa
habari nje ya mahakama na kumshukuru jaji kwa kupitia marejeo yao
waliyoomba na kuyatolea maamuzi.
Awali wananchama hao watao wa CHADEMA kutoka mikoa mbalimbali hapa
nchini walikuwa wanatuhumiwa kwa makosa mawili likiwemo la ugaidi kwamba
walimteka na kummwagia tindikali raia mkazi wa mjini Igunga.
Katika shtaka la kwanza walishtakiwa chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi,
wakidaiwa kumteka kwa nia ya ugaidi Mussa Tesha huko Igunga, Tabora na
la pili wanashtakiwa chini ya Sheria ya Kanuni za Adhabu wakidaiwa
kumdhuru Tesha kwa kummwagia tindikali.
Walidaiwa kutenda makosa hayo mwaka 2011, wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga.
Upande wa mashtaka uliongozwa na wakili wa serikali, Juma Masanja,
akisaidiana na wakili mwingine wa serikali, Idelfonce Mukandara,
waliodai mashtaka hayo ni halali.
-TANZANIA DAIMA
|