KAMATI
ya Utendaji ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la
Ukonga imewafukuza uanachama wanachama wake wanane huku wawili wakipewa
onyo kali kwa tuhuma za kukihujumu.
Akizungumza na Tanzania Daima
Jumapili ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa CHADEMA
Jimbo la Ukonga, Jumaa Mwipopo, alisema kuwa kwa muda mrefu kulikuwa na
tuhuma za wanachama hao kukihujumu chama hicho kwa kufanya vikao vya
siri ili kuwarubuni wanachama na viongozi wa matawi kukihama.
Mwipopo alisema kuwa mikakati hiyo ilikuwa ikiratibiwa na Mchungaji Zabron Shilinde na Habibu Rajabu.
Alisema
kuwa Mchungaji Shilinde awali alikuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kata ya
Kitunda, lakini alivuliwa uongozi Aprili 10, 2012 kutokana na tuhuma
mbalimbali, ikiwamo kuchukua fedha za chama na kuzitumia bila
idhini
na kuchukua kadi za chama kwenye kata na matawi bila kujulikana
alikokuwa akizipeleka, tuhuma ambazo alikiri, hivyo kubaki kuwa
mwanachama wa kawaida.
Akimzungumzia Rajabu, Mwipopo alisema kabla ya kufukuzwa uanachama alikuwa Mwenyekiti wa Vijana wa Kata ya Kitunda.
Aidha,
Katibu huyo wa Jimbo la Ukonga alisema kuwa tuhuma zinazowakabili
Shilinde, Rajabu na wenzao sita ni kupokea fedha kutoka kwa viongozi wa
Chama Cha Mapinduazi (CCM) ili zitumike kuwashawishi viongozi na
wanachama wa matawi mbalimbali wa chama hicho kujiondoa CHADEMA na
kujiunga na CCM.
Mwipopo aliwataja
watuhumiwa wengine waliofukuzwa uanachama tangu Agosti, 15, 2013 ni
Joshua Kisoko - Mwenyekiti wa Tawi la Msingi Masesko, Esther Joshua
Kisoko - Katibu wa Kina Mama Kata ya Majohe, S. Ngazonga – mwanachama,
J. Shomary - mwanachama, Pili Said – mwanachama na Surema Amali-
mwanachama.
Vilevile aliwataja waliopewa onyo kali kuwa ni Lukasi Matindiko na Juma Ununzi, ambaye ni Mwenyekiti wa Tawi la Kwa Mpemba.
Mwipopo
alibainisha kuwa: “Baada ya Kamati ya Utendaji kujiridhisha na ushahidi
uliotolewa pamoja na kupitia mawasiliano yao, kutokana mkakati wao wa
kushawishi wanachama na viongozi wa CHADEMA kukihama chama, kuanzia
Agosti 15, 2013 si wanachama wetu tena na hawatakiwi kujihusisha na
shughuli za chama.”
Julius Kunyara,
-TANZANIA DAIMA.