Ng’ombe zaidi ya 80 wameuawa kikatili kwa kukatwakatwa na
wengine kuchinjwa baada ya mifugo kuingia katika mashamba ya wakulima wa vijiji
vya Kisara na Mbogo wilaya Mvomero mkoa wa Morogoro .
Mdodosaji wetu ameshuhudia mabaki ya nyama na ngozi za na ndama
wachanga waliondolewa katika matumbo ya ngombe waliochinjwa na
kisha nyama kuuzwa katika mabucha huku ngombe wengine wakiwa wamekatwa
miguu na kushindwa kutembea ambapo wamiliki wa ngombe hizo ambao ni wafugaji
wamelalamikia wakulima kuchukua hatua mkononi na kuomba serikali kuchukua
hatua.
Nao baadhi ya wakulima wa wilayani Mvomero walioshuhudia
tukio hilo wameonyesha kusikitishwa na tukio hilo huku wakiitaka serikali
kuhakikisha inapanga mipango mizuri ili kunusuru migogoro ya wakulima na
wafugaji kwa kutenga maeneo maalumu kwa shughuli za kilimo na ufugaji.
Nae mkuu wa wilaya ya Mvomero Antony Mtaka akizungumzia tukio
hilo amesema serikali ya wilaya imeanza kuchukua hatua kwa kushirikiana na
jeshi la polisi ili waliohusika na tukio hilo wachukuliwe hatua za kisheria
huku akiwataka wafugaji kutulia wasilipize kisasi.