Rais aliyechaguliwa tena kutawala kwa muhula mwingine nchini
Zimbabwe Robert Mugabe, amewaambia wapinzani wake kwenye uchaguzi uliokamilika
hivi karubini kuwa ikiwa hawajapendezwa na matokeo ya uchaguzi basi
'wajinyonge'.
Mugabe aliongeza
kuwa hawezi kurudi kwenye serikali ya muungano iliyoafikiwa kutokana na vurugu
zilizofuata uchaguzi mkuu wa mwaka 2008.
Mugabe aliyatoa
matamshi yake makali kwenye sherehe za kuadhimisha siku ya mashuja waliopigania
uhuru wa Zimbabwe.
Morgan Tsvangirai,
anayeongoza chama cha upinzani MDC, alisusia sherehe hizo ambapo Mugabe alitoa
hotuba yake ya kwanza tangu kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 31 mwezi
Julai.
MDC kimewasilisha
malalamiko yake mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu hali ambayo
imesababisha kucheleweshwa kuapishwa kwa Mugabe. Alishinda uchaguzi huo kwa
asilimia sitini ya kuza zote. Hata hivyo majaji wengi wanasemekana kumuunga
mkono Mugabe kwa hivyo huenda kesi ya MDC ikatupiliwa mbali.
Chama cha Mugabe
Zanu-PF kilishinda wingi wa viti vya bunge kikipata zaidi ya thuluthi mbili
ikiwa ni viti 160 ya viti kati ya 210 vya bunge zima.
Sherehe za
kuadhimisha siku ya mashujaa Zimbabwe, ni sherehe za kujivunia kwa wazimbabwe
wakati ambapo nchi hiyo ilijipatia uhuru wake miaka ya sabini.
Hii leo Mugabe
ameitoa hotuba yake ya kwanza katika eneo la kumbukumbu la vita hivyo na ambako
baadhi ya wapigania uhuru wamezikwa.
Hotuba za Mugabe
zinasifika zaidi kwa siasa zake kali za kizalendo, na ambazo zaidi hulenga
mkoloni wake wa zamani Uingereza na pia anatarajiwa kujipiga kifua kufuatia
ushindi wake mkubwa katika uchaguzi mkuu uliopita mwezi jana.
Chama cha MDC
kinasusia sherehe hizo katika kile kinachosema ilikuwa wizi mkubwa wa kura
uliofanywa na chama cha Zanu-PF, kwa hivyo sherehe hii bila shaka itazongwa na
siasa.
Mugabe bado
hajaapishwa kwa muhula wake wa saba akitawala Zimbabwe, kwa sababu ya kesi ya
MDC mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi huo.
MDC kilisema kina
ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa wizi wa kura ulitokea na kwamba kulikuwa na
visa vingine vilivyohujumu matokeo ya uchaguzi huo ikiwemo, rushwa , dhuluma na
kuvurugwa kwa daftari la wapiga kura.