muhtasari

Home » , , » Rwanda sasa waanza kuihujumu Tanzania ...

Rwanda sasa waanza kuihujumu Tanzania ...

Rais wa Rwanda, Paul Kagame
































 *Yatangaza kutotumia Bandari ya Dar es Salaam
*Serikali yasema haina muda wa malumbano

UHUSIANO wa Tanzania na Rwanda, umezidi kuingia doa, baada ya nchi hiyo kutangaza kutotumia Bandari ya Dar es Salaam, kuanzia Septemba Mosi, mwaka huu, kupitisha mizigo ya wafanyabiashara wake.
Uamuzi wa Rwanda umekuja huku kukiwa na mgogoro wa chini chini unaoendelea kufukuta, baada ya Rais Jakaya Kikwete kumshauri Rais Paul Kagame, kukaa meza moja na waasi wa kundi la FDLR, ambao wanadaiwa kuendesha mapigano nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Uamuzi huo, ulibainika mjini Dar es Salaam jana, wakati wa kikao cha pamoja kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, chini ya Mwenyekiti wake, Andrew Chenge na Umoja wa Wasafirishaji wa Mizigo kwa njia ya barabara Tanzania (TATOA).

Katika kikao hicho, TATOA ilieleza namna nchi za Rwanda na Uganda zilivyokusudia kuachana na mipango yao ya kupitisha mizigo yao katika Bandari ya Dar es Salaam.

Msemaji wa TATOA, Elias Lukumay, alisema kupanda kwa gharama za ushuru, kodi na nyinginezo, ni sababu kuu ya nchi hizo kujitoa kutumia bandari hiyo.

“Tunaelewa ufinyu wa bajeti ya Serikali, lakini sekta ya usafirishaji kwa sasa inaelemewa, baadhi ya vitu vilivyopanda na hivyo kuongeza gharama za uendeshaji ni leseni za barabarani, kodi ya mafuta, malipo ya bima, ghala la kuhifadhia mizigo, ada ya Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) na nyinginezo.

“Gharama kubwa za uendeshaji katika usafirishaji na kuweka gharama nyingi za ziada kutaathiri uchumi ambapo wateja wa nchi jirani watatafuta njia mbadala, wakati ilitugharimu kuwaleta kwetu na wengine watatafuta shughuli mbadala na kuachana na usafirishaji,” alisema.

Alisema mkutano wa maazimio hayo ulifanyika Julai 19, mwaka huu, nchini Rwanda, ambapo mjadala ulikuwa ni kutotumia Bandari ya Dar es Salaam kwa sababu Tanzania haina uamuzi wa haraka katika mambo yake kwa upande wa biashara.

“Kama TATOA, tulipata barua ya mwaliko wa mkutano huo, lakini hatukuhudhuria, sababu kubwa wenyewe wanasema hatueleweki na hatuna uamuzi wa haraka.

“Jambo hili pia, limechangiwa na mgogoro uliopo baina yetu na Rwanda, umechangia kwa kiasi kikubwa, kwani mkutano huo pia ulifanyika wakati Rais wa Marekani, Barrack Obama, akiwa nchini kwetu kwa ziara ya siku mbili,” alisema Lukumay.

Katika barua iliyoandikwa Julai 16, mwaka huu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Sekta Binafsi wa Rwanda, Hannington Namara na MTANZANIA kupata nakala yake, iliwataka wanachama wa usafirishaji katika nchi hizo kukutana ili kujadili utekelezaji wa ushuru wa pamoja wa orodha.

Sehemu ya barua hiyo ilisema: “Mkutano huo unarejea mazungumzo ya pande tatu yaliyofanyika mjini Kampala, Uganda, baina ya wakuu wa nchi za Rwanda, Uganda na Kenya, ambapo madhumuni yake ni kujadili kwa kina masuala yanayohusu biashara ya upakuaji na upakiaji mizigo kuendana na utekelezaji wa ushuru wa pamoja wa forodha.”

Moja ya uamuzi uliofikiwa katika mkutano huo ilikuwa kuimarisha eneo la ushuru wa pamoja wa forodha na utekelezaji wake, ambapo kodi zitakusanywa katika maeneo ya mipaka kama Mombasa, Mpondwe na Oluhura.

TATOA waliomba sekta ya usafirishaji ipunguziwe kodi, ihamasishwe na kuwezeshwa ili itoe mchango zaidi kwa pato la taifa kwa mamlaka husika kutenga maeneo ya maegesho na kusitisha ukamataji wa magari unaoendelea.
-MTANZANIA

Popular Post

 
Support : OBAMA | OBAMA | OBAMA
Copyright © 2013. DiraYaLeo - All Rights Reserved
Template Created by Barakaeli Aremu Published by Dira Ya Leo
Proudly powered by Blogger