muhtasari

Home » » SUMAYE AWARUSHIA MAKOMBORA VIGOGO...

SUMAYE AWARUSHIA MAKOMBORA VIGOGO...

Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye.Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye amesema kuwa katiba nzuri ni lazima iambatane na Serikali adilifu inayojali masilahi ya umma na Rais anayeiongoza awe mchapakazi na anayejali masilahi ya umma na siyo masilahi yake, Sumaye alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akifunga baraza la katiba la Taasisi ya Vyuo Vikuu Tanzania (TAHLISO) iliyohusisha marais wote wa vyuo vikuu Tanzania na makamishna kutoka kanda saba za taasisi hiyo, lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Mzumbe Tawi la Mbeya.
Alisema kuwa dhahiri katiba nzuri ni jambo la msingi katika kutoa mwelekeo wa jumla wa jinsi nchi inavyoendesha mambo yake, yaani mfumo wake wa utawala, masilahi ya jamii, matumizi ya rasilimali zake na uhusiano wake.

Sumaye alifafanua kuwa pamoja na uzuri wake, katiba pekee haitatoa majawabu yanayotegemewa na wananchi kama utekelezaji na usimamizi wa shughuli hizo siyo makini. ” Kwani katiba ni mwanzo mzuri tu na ili matunda mazuri ya katiba nzuri yaonekane na yawafikie wadau yaani wananchi wote, ni lazima iwe na mlinzi na mtetezi shupavu na makini,” alisema.
“Ndivyo wanapoapa viapo vyao vya uaminifu wa nchi. Kwa hiyo katiba nzuri lazima iambatane na Serikali adilifu inayojali masilahi ya umma na rais anayeingoza awe mchapakazi na anayejali masilahi ya umma mpana na siyo masilahi yake binafsi ya watoto wake au ya marafiki zake.”
Alisema kuwa rais mwenyewe awe na uadilifu usiotiliwa shaka ya aina yoyote na apigane vita vya wazi dhidi ya rushwa, ufisadi, dawa za kelevya na maovu mengineyo katika jamii. ”Tukifanikiwa katika yote hayo basi tutakuwa tumevuna na kuyala matunda mema ya katiba nzuri,” alisema.
“Tukikosea katika yote au hata mojawapo tukawa na katiba mbovu Serikali nzuri au katiba nzuri lakini Serikali mbovu basi tutakuwa tumeharibikiwa na wala wananchi hawatapata matunda waliyotegemea,” alisema.
Kuhusu suala la rasimu ya Katiba Mpya, Sumaye alisema kuwa kuna eneo moja gumu ambalo ni la sura ya Muungano, ambapo rasimu imesema watu wengi wametaka kuwe na muungano wa Serikali tatu: “Mimi hoja yangu siyo idadi ya Serikali bali kwanza tujiulize maswali kadhaa na tuyapatie majibu ili tufanye uamuzi mzuri wa muundo utakaotufaa,” aliongeza.
Aliyataja maswali hayo kuwa ni pamoja na: Je, kwa nini tumefika hapo? Kama kuna masuala tumeshindwa kuyatatua katika muundo wa Serikali mbili, kuunda Serikali tatu ndiyo jawabu? Je, ni muundo upi utatikisa muungano wetu?
Suala la gharama za kuendesha Serikali tatu na vyombo vyake uchumi wetu unabeba kwa sasa? Tumetazama mbele zaidi ya wakati ulipo na kufanya tathmini ya kutosha?

Popular Post

 
Support : OBAMA | OBAMA | OBAMA
Copyright © 2013. DiraYaLeo - All Rights Reserved
Template Created by Barakaeli Aremu Published by Dira Ya Leo
Proudly powered by Blogger