muhtasari

Home » , » Taifa lavuliwa nguo

Taifa lavuliwa nguo



TUKIO la kumwagiwa tindikali kwa wasichana wawili raia wa Uingereza limeiweka Tanzania katika sura chafu baada ya kituo maarufu duniani cha runinga (CNN) kulitangaza kwa uzito mkubwa.
CNN kupitia kipindi chake cha Out Front imeonesha kuwa Tanzania sio salama tena na kwamba watu wanaotaka kutembelea nchini humo, lazima wachukue hatua za tahadhari.
Wasichana hao walimwagiwa tindikali juzi saa 1:15 usiku mtaa wa Shangani eneo la mji Mkongwe, Zanzibar.
Wasichana hao walifika visiwani humo wakijitolea kufundisha somo la Kiingereza katika shule ya msingi ya St. Monica inayomilikiwa na Kanisa la Angilikana Zanzibar.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumamosi mmoja wa Watanzania waishio nchini Norway alisema kuwa majira ya usiku kituo hicho kilitangaza kwa kina tukio la kutisha la wasichana hao kuvamiwa na kumwagiwa tindikali hatua ambayo imeiweka Tanzania katika sura mbaya duniani.
“Sio siri ndugu yangu matukio hayo kwa sasa yanatisha maana hata hapa nchini kwetu watu wanaotaka kutembelea huko wameanza kuchukua taadhali na kuna uwezekano wa kupungua kwa watalii baada ya tukio hili,” alisema.
Alisema kuwa pamoja na kuwepo kwa baadhi ya Wazungu walioolewa na Wazanzibari, akitolea mfano jirani yake (jina linahifadhiwa) alisema tukio hilo limepokelewa na raia wengi kwa hofu kubwa kiasi cha kumfanya jirani yake kugoma kuzuru Tanzania kwa kuwa ana hofu watoto aliozaa kudhuriwa.
Mbali na kituo hicho, baadhi ya magazeti ya Marekani na yale ya Uingereza yameiandika habari hiyo na kuipa uzito wa juu mno, hasa wengi wakishangazwa na ‘ukarimu’ wao wa kwenda kujitolea kufundisha Zanzibar huku wakiambulia kumwagiwa tindikali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, aliwataja mabinti hao waliojeruhiwa kuwa ni Katie Gee (18) na Kirstie Trup (18) ambao walifika Zanzibar wiki mbili zilizopita kwa mwaliko wa taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Arts in Tanzania.
Alisema raia hao wa Uingereza walipatwa na mkasa huo wakati wametoka kunywa kahawa katika Jaws Corner, mtaa wa Sokomhogo.
“Walimu hao walipofika makutano ya mitaa ya Shangani na Vuga wakielekea Hoteli ya Pagoda kwa ajili ya kupata chakula cha jioni ndipo vijana wawili wasiojulikana waliokuwa kwenye pikipiki aina ya Vespa waliwamwagia tindikali na kutokomea kusikojulikana,” alisema.
Mkadam alisema raia hao baada ya kumwagiwa tindikali walikimbilia baharini kunawa, lakini walipoona hali ni mbaya walipata msaada kutoka kwa raia wema ambao waliwachukua na kuwapeleka Hospitali ya Afya Medical iliyoko Vuga na baadaye kuhamishiwa hospitali ya Mnazi Mmoja iliyoko mjini Zanzibar.
Alisema Katie amejeruhiwa vibaya sehemu ya usoni wakati Kirstie amejeruhiwa kifuani na mgongoni. Wasichana hao kwa sasa wamelazwa katika Hospitali ya Agha Khan jijini Dar es Salaam na kuna uwezekano wa kusafirishwa leo kwenda Uingereza kwa matibabu zaidi.
source: TANZANIA DAIMA

Popular Post

 
Support : OBAMA | OBAMA | OBAMA
Copyright © 2013. DiraYaLeo - All Rights Reserved
Template Created by Barakaeli Aremu Published by Dira Ya Leo
Proudly powered by Blogger