WAUMINI wa dini
ya Kiislamu waliokuwa katika ibada ya Swala ya Idd El Fitri katika
msikiti mkuu wa Ijumaa uliopo Wilayani Kyela mkoani Mbeya wamekumbwa na
taharuki baada ya Shekhe wao aliyekuwa akiongoza ibada kuvamiwa kibla
wakati akiendesha ibada na kujeruhiwa.
Tukio hilo la aina yake
limetokea majira ya asubuhi ambapo Shekhe huyo aliyetambuliwa kwa jina
la Nuhu Mwafilango alishambuliwa akiwa katikati ya sijida baada ya mtu
mmoja aliyedaiwa kuwa ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya kutwa ya
Kyela, Ally Mwangosi kuchoma Shekhe huyo na kitu chenye ncha kali.
Taarifa
kutoka msikitini hapo zinadai kuwa mara baada ya tukio hilo, Shekhe
alipiga kelele wa kuomba msaada na ndipo waumini waliokuwa wakiswali
msikitini hapo waliposhikwa na taharuki.
Mwenyekiti wa Baraza Kuu
la Waislamu Wilayani Kyela Bw. Daudi Mwenda alisema kuwa waumini
walimuokoa na kumkimbiza katika Hospitali ya Wilaya kwa ajili ya
kupatiwa matibabu.
Bw. Mwenda alisema kuwa Shekhe huyo ameumizwa
vibaya kichwani na kutokwa na damu nyingi. Waumini wawili waliojaribu
kumuokoa Shekhe huyo nao walijeruhiwa kwa kuchomwa na kisu ikiwa ni
pamoja na mweka hazina wa BAKWATA wilaya Ustadhi Khamis Hussein ambaye
alijeruhiwa kichwani na sikioni.
Nao baadhi ya waumini
waliokuwepo katika ibada hiyo walisema kuwa tukio hilo lilitokea wakati
waumini wote wakiwa wamesujudu, ndipo waliposikia kelele na vurugu.
Mmoja
wa waumini aliyejitambulisha kwa jina la Idd Hussein alisema kuwa
liliibuka kundi la watu waliomsaidia kijana huyo, na kuibua vurugu kubwa
iliyosababisha ibada ya swala ya Idd kuvunjika.
Akizungumzia
tukio hilo Katibu wa BAKWATA mkoa wa Mbeya Shekhe Juma Killah alisema
kuwa vurugu hizo zimetokea katika swala ya Idd na wahusika wa vurugu
hizo ni Waislamu ambao wanaipinga BAKWATA.
‘’Hiki
ni kikundi cha waislamu waliotoka Jijini Dar es salaam ambacho kimekuja huku na
kimesambaa katika wilaya zote za mkoa wa Mbeya.Kikundi hiki kinashawishi watu
kuipinga BAKWATA na kinafanya mambo ambayo BAKWATA hatukubaliani nayo,’’alisema Shekhe Killah.
Alisema
kuwa kikundi hicho kilikuwa kikimtuhumu Shekhe wa Wilaya kuwa ni
mshirikina na kwamba kutokana na hali hiyo hakupaswa kuongoza ibada
msikitini na badala yake wao ndio waliopaswa kuongoza ibada msikitini
hapo.
Kwa
upande wake Shekhe wa BAKWATA mkoa wa Mbeya Mohamed Mwansasu alisema
kuwa kitendo hicho kimeudhalilisha Uislamu na kwamba kilichofanywa na
kundi hilo la watu si mafundisho ya dini ya Kiislamu.
Hata hivyo Shekhe Mwansasu alienda mbali zaidi na kusema kuwa katika kikundi hicho wapo baadhi
ya waumini wanaodaiwa kuwa ni askari polisi ambapo inadaiwa kuwa katika
moja ya swala ya Ijumaa wiki iliyopita imamu aliyekuwa akiswalisha
alivutwa kanzu yake na kutakiwa kutoka eneo la kuongozea ibada ili
kuwapisha wao waendeshe ibada hiyo.
Kamanda
wa Polisi mkoa wa Mbeya Bw. Athumani Diwani amekiri kutokea kwa tukio
hilo ambapo alisema kuwa watu sita wanashikiliwa na Polisi kufuatia
vurugu hiyo iliyotokea majira ya saa 2:30 katika msikiti mkuu wa Ijumaa
wakati wa swala ya Idd el Fitri.
Kamanda
Diwani alisema kuwa kundi la waislamu wanaojiita kuwa ni wenye itikadi
kali walivamia msikitini wakati waumini wengine wakiwa wameinama
wakisujudu na kumvaa imamu kwa kumpiga kwa mateke na ngumi huku wakiwa
na nondo, mikasi na visu.
Alisema waumini hao walikuwa na madai kuwa hawamtaki Shekhe huyo na kwamba uwezo wake ni mdogo katika dini.
Alisema
kuwa Shekhe huyo aliokolewa na baadhi ya waislamu ambapo aliwataja
walioshikiliwa na polisi kuwa ni pamoja na Mashaka Kassim(30)Issa
Juma(37),Ahmed Kassim Magogo(35) Ibrahimu Shaaban(17) ambaye ni
mwanafunzi wa shule ya sekondari ya kutwa ya Kyela anayesoma kidato cha
Nne,Ambokile Mwangosi,(19)mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya
sekondari Kyela, Sadick Abdul(28).
Kamanda Diwani alisema kuwa taratibu zinafanyika ili watuhumiwa wafikishwe mahakamani.