Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
- Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ametangaza kuuawa kwa magaidi watano na kwamba watuhumiwa 11 wanashikiliwa.
- Hata hivyo, taarifa zaidi zilieleza kwamba ghorofa tatu za jengo la Westgate ziliporomoka huku kukiwa na miili ambayo ilikuwa haijaokolewa.
Nairobi. Wakati jengo la
ghorofa tatu lililovamiwa na magaidi likiripotiwa kuanguka jana na kuua
watu sita, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema mwanamke mmoja raia wa
Uingereza na Wamarekani wawili au watatu wanashukiwa kuongoza shambulizi
la kigaidi lililofanywa katika jengo la biashara eneo la Westgate,
Nairobi, Jumamosi iliyopita.
Akilihutubia taifa la Kenya jana, Rais Kenyatta
alisema hakuna ushahidi wa kuwahusisha watu hao na tukio hilo moja kwa
moja lakini uchunguzi unaendelea.
“Wataalamu wa mambo ya upelelezi wanaendelea
kuchunguza juu ya ushiriki wa watu hawa na wakiwabaini, basi tutachukua
hatua kali,” alisema Rais Kenyatta.
Tangu kutokea kwa shambulizi hilo, vyombo
mbalimbali vya habari vilimtaja mwanamke wa Uingereza, Samantha
Lewthwaite kuwa ndiye aliyeongoza shambulizi hilo.
Pia jina lake lilitajwa na Kundi la Al-Shabaab kupitia katika mtandao wa mawasiliano wa kijamii wa Twitter.
Hata hivyo, maelezo ya Rais Kenyatta yanapingana
na ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi hiyo, Joseph ole Lenku ambaye
alikaririwa na vyombo vya habari jana akidai kuwa hakukuwa na mwanamke
miongoni mwa magaidi hao, bali baadhi yao walivaa nguo za kike.
Rais Kenyatta alisema magaidi watano walikuwa wameuawa katika operesheni hiyo ya kulikomboa jengo hilo.
Pia alibainisha kuwa watu kumi na moja walikuwa wanashikiliwa na polisi wakishukiwa kushiriki katika shambulio hilo.
Magaidi wanaoaminika kuwa wafuasi wa Kundi la
Al-Shabaab walivamia jengo hilo na kufanya shambulizi lililosababisha
vifo vya zaidi ya watu 60 na 175 kujeruhiwa, Jumamosi iliyopita.
Rais Kenyatta aliapa kuwa Serikali yake imepania kuwashinda magaidi na kuhakikisha inawafikisha kwenye mikono ya sheria.
Ghorofa kuanguka
Pia Rais Kenyatta alitangaza kuwa maofisa sita wa
usalama walifariki dunia jana jioni baada ya kuangukiwa na ukuta baada
ya kudondoka kwa ghorofa tatu za jengo ambalo magaidi wamejichimbia.
-mwananchi
-mwananchi