VYAMA vitatu vya CHADEMA, CUF na NCCR Mageuzi vimeamua
kuunganisha nguvu ili kunusuru mchakato wa Katiba unaoendelea kwa kile
walichodai kuwa CCM inataka kuhodhi mchakato huo.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,
viongozi wakuu wa vyama hivyo, Freeman Mbowe (CHADEMA), Prof. Ibrahim
Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR-Mageuzi, walisema wametafakari na
kujadili mustakabali wa taifa.
Walisema kuwa tangu kupitishwa kinyemela mwa muswada wa marekebisho ya
mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013, kumekuwa na taarifa za upotoshwaji
kwa umma juu ya kile kilichotokea bungneni.
Kwa mujibu wa viongozi hao, mchakato wa Katiba mpya unahitaji
uvumilivu, stahamala, hekima, kuheshimiana na kamwe usitawaliwe kwa
mizengwe na nia mbaya, ubabe, mabavu, kejeli na dharau hasa kutoka kwa
watawala na wadau wengine.
“Kufanya vile kutasababisha kulitumbukiza taifa letu katika mipasuko, migogoro na machafuko,” walisema.
Walisema kuwa nguvu ya pamoja ya wananchi, wadau wote na Watanzania
wenye kuitakia mema nchi yetu zinapaswa kuunganishwa kuunusuru mchakato
wa Katiba mpya uliotekwa na kuhodhiwa na CCM na serikali yake.
Katika kuhakikisha wananchi wanafahamu kile kilichotokea bungeni kwa
wapinznai kususia muswada huo uliochakachuliwa kwa kuchomekwa vifungu
visivyo na manufaa, viongozi hao wameanza utaratibu wa kukutana na
makundi mbalimbali ya wadau na wananchi.
Kwa jana viongozi hao walikutana na wahariri wa habari na ndani ya
wiki hii watakutana na makundi mengine ya viongozi wa dini, asasi za
kijamii, wanazuoni na wananchi wengine.
Waliuchambua muswada uliopitishwa kinyemela hivi karibuni na wabunge
wa CCM wakisema ulikuwa na kasoro nyingi za wazi na kwamba Serikali ya
Muungano iliidanganya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
“Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haikushirikishwa katika kuandaa
muswada uliopelekwa bungeni wa sheria ya mabadiliko ya Katiba,”
walisema.
Pia waligusia hatua ya wabunge wa CCM kuridhia muswada huo unaoainisha
kuwa baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba
kukabidhi rasimu kwa Bunge Maalumu la Katiba inafutwa.
Viongozi hao walipendekeza kuwa tume hiyo haipaswi kufutwa hadi hapo
mchakato utakapofikia hatua ya kura ya maoni ili kuipa nafasi ya
kulisaidia Bunge Maalum la Katiba kufafanua baadhi ya vifungu
vitakavyokuwa na utata kwenye rasimu.
“Huu si mpambano baina ya CCM na wapinzani na katika hili hakuna
mshindi wala mshindwa bali unatafutwa muafaka wa pamoja katika taifa
lililoparaganyika,” walisema katika tamko lao.
Wenyeviti hao waliongeza kuwa Mei mwaka huu, Serikali ya Muungano
ilipeleka muswada wa sheria ya mabadiliko ya Katiba uliokuwa na vifungu
sita.
Kwamba serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliujadili na kupeleka
mapendekezo yao ya rasimu ya muswada huo. Lakini muswada uliopelekwa
bungeni hivi karibuni uliongezwa vifungu vingi ambavyo havikuwepo katika
rasimu iliyopelekewa Zanzibar.
Walitolea mfano kifungu cha 26 cha sheria mama kurekebishwa kuruhusu
iwapo theluthi mbili za kila upande hazikupatikana, hivyo kufanya
utaratibu wa kupitisha hoja kuwa wa wingi wa kawaida (simple majority).
Vilevile walimuonya Rais Jakaya Kikwete kutousaini muswada huo kuwa
sheria, kwani marekebisho yaliyofanyika na utaratibu uliotumika
kuyapitisha ni kinyume na dhamira na dhima ya majadiliano aliyofanya na
vyama hivyo na wadau mwaka 2011 na 2012.
Kutokana na hali hivyo, vyama hivyo vimeazimia kufanya mkutano mkubwa
jijini Dar es Salaam Septemba 21 mwaka huu, katika viwanja vya Jangwani
ili kupeleka ujumbe kwa wananchi kunusuru mchakato usiendelee kuhodhiwa
na kutekwa na CCM.
Waliziomba asasi za kiraia, taasisi za dini, vyama vingine vya siasa,
taasisi zingine za elimu ya juu, vyama vya wafanyakazi, jumuiya za
wakulima, wafugaji, nyinginezo na wananchi kwa ujumla kuweka pembeni
tofauti zao na kuunga mkono hoja yao.
-
|