Nairobi. Imeelezwa kuwa magaidi waliovamia jengo kubwa la maduka la Westgate jijini
Nairobi, Kenya mwishoni mwa juma lililopita waliingia na magari matatu
aina ya Nissan na kumuua mlinzi mkuu wa eneo hilo, Morris Adembesa kwa
kumpiga risasi nane.
Akizungumzia tukio hilo kwenye Hospitali ya Aga Khan Nairobi,
mke wa mlinzi huyo, Eunice Kavesa alisema ameuona mwili wa mumewe na
kusema una matundu manane ya risasi alizopigwa na magaidi hao.
Alisema aliuawa baada ya walinzi wenzake kumwita getini ili kuzungumza na magaidi hao ambao walikuwa wamekataa kupekuliwa.
“Walikataa kukaguliwa ndipo walipomwita mume wangu ambaye ni mkuu wa
ulinzi hapo na alipofika tu wakammiminia risasi nane hapohapo,” alisema
mama huyo.
Alisema mume wake alihamishiwa katika kituo hicho akitokea Mombasa wiki moja iliyopita na siku mauti yalipomkuta ilikuwa ni siku yake ya nne tangu alipoanza kazi hapo.
“Ameniachia watoto wawili niliozaa naye na yuko mwingine, maisha
yatakuwa magumu kwa kuwa ninafanya kazi za kawaida tu na yeye ndiye
aliyekuwa akitunza familia,” alisema Eunice.
Wakati akisema hayo mashambulizi yalikuwa yakiendelea katika eneo hilo
la Westgate ambalo limezingirwa na vikosi mbalimbali vya usalama vya
ndani na nje ya Kenya. Jana ilikuwa siku ya tatu tangu magaidi hao walipoliteka jengo hilo na kuua watu 62 huku wakiwajeruhi 175
chanzo:mwananchi