BAADA ya kuisambaratisha Mtibwa Sugar katika Ligi Kuu ya Bara wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba imesema kikosi chake kipo kamili kambini kuikabiri JKT Mgambo hapo kesho.
Simba inatarajiwa kushuka kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kesho kuvaana na Mgambo ikiwa na kumbukumbu ya kuifunga Mtibwa Sugar mabao 2-0 katika uwanja huo.
Matokeo hayo yaliifanya Simba ifikishe pointi saba baada ya kucheza mechi tatu na kutoka sare moja kisha kushinda mechi mbili.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga ameuambia mtandao huu kwamba kikosi cha timu yake kipo tayari kwa mechi dhidi ya Mgambo na kocha Abdallah Kibadeni hana wasiwasi na kikosi chake.
“Timu iko vizuri kambini Bamba Beach kujiaindaa na mchezo dhidi ya Mgambo, kocha (Kibadeni) amesema kikosi kipo tayari kwa mchezo na hakuna kitu kitakachozuia ushindi hivyo nawaomba wapenzi wa Simba wajitokeze kwa wingi uwanjani kushuhudia timu yao ikipata pointi tatu nyingine.
“Unajua mechi dhidi ya Mtibwa ilikuwa ngumu sana kwetu maana mwaka jana kama unakumbuka walitufunga na sisi msimu huu tumeweza kulipa kisasi na sasa atakayekaa mbele yetu tutahakikisha tunamfunga ili kuweza kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa,” alisema Kamwaga.
Kamwaga amesema hadi sasa kikosi chake hakina majeruhi hata mmoja na wachezaji wote wapo tayari kwa mchezo. “Hatuna majeruhi hta mmoja na hata wale wenye majeraha madogo hawawezi kushindwa kujumuhishwa kikosini,” alisema Kamwaga.
Tangu mechi za msimu huu zianze Simba imekuwa ikiwategemea zaidi wachezaji wake wapya kama Issa Rashidi ‘Baba Ubaya’, Gilbert Kaze, Joseph Owino katika nafasi ya ulinzi huku katika kiungo ikiwategemea Twaha Ibrahim na Henry Joseph na kwa upande wa washambuliaji wapo Amisi Tamwe na Betram Mwombeki.
Msimu uliopita Simba ilishika nafasi ya tatu na kuziacha Yanga na Azam zikitwaa nafasi za juu ambapo Yanga ndiyo iliyotwaa ubingwa, hivyo Simba msimu huu imekosa nafasi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Mgambo inayocheza na Simba hapo kesho, yenyewe ina pointi tatu tu huku ikiwa nafasi ya tisa baada ya kucheza mechi tatu na kushinda moja huku ikifungwa mechi mbili.
MGAMBO YAIVIMBIA SIMBA
Licha ya timu yake kufungwa mechi mbili za Ligi Kuu ya Bara na kushinda mechi moja tu na kujikuta ikishika nafasi ya tisa ikiwa na pointi tatu tu, Kocha wa Mgambo, Mohamed Kampira amesema kamwe Simba isitarajie mteremko katika mchezo wa kesho.
Kampira ameuambia mtandao huu kwamba, timu yake ipo jijini Dar es Salaam tangu wikiendi iliyopita na wameshafanya mazoezi ya kutosha kuweza kuibuka na ushindi hapo kesho.
“Sitishwi na matokeo yaliyotokea huko nyuma wala ukubwa wa timu ninayopambana nayo (Simba), mimi kazi yangu nimeshaifanya na wachezaji wangu sasa wapo tayari kwa mchezo ninachosubiri ni muda ufike ili tucheze na Simba,” alisema Kampira.
Kampira alisema kikosi chake hakina majeruhi wa kutisha kwani wachezaji wote wanaweza kupambana katika mechi ya kesho. “Sina majeruhi wa kutisha kwani wapo wachache wanaosumbuliwa na majeraha madogo madogo ambayo yanaweza kuwafanya wacheze,” alisema Kampira.