- Ni kauli iliyotolewa wakati wa mkutano wa hadhara uliovishirikisha vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi
Waziri wa Sheria na Katiba Mathias Chikawe
ametakiwa ajiuzulu kwa kutoa taarifa za uongo kwamba Zanzibar
ilishirikishwa kabla ya Muswada wa Mabadiliko ya Katiba kuwasilishwa
bungeni na kupitishwa na Bunge Septemba mwaka huu.
Msimamo huo ulitolewa na Waziri wa Sheria na
Katiba Zanzibar, Aboubakary Khamis Bakari wakati akihutubia mkutano wa
hadhara uliovishirikishwa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi
uliofanyika Uwanja wa Kibandamaiti mjini Unguja jana.
Aboubakari alisema kwamba Zanzibar ilipokea
taarifa ya awali ya mabadiliko kuhusu vifungu vinne vya Muswada wa
Mabadiliko ya Katiba na kutakiwa Zanzibar itoe maoni na mapendekezo
yake, jambo ambalo alisema lilifanyika kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili
wa Rais Zanzibar na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Hata hivyo, alisema vifungu vya mabadiliko ghafla
viliongezwa kutoka vinne hadi 12 bila ya Zanzibar kupewa nafasi ya
kujadili vifungu vinane ambavyo vina umuhimu mkubwa katika kupata katiba
bora.
“Waziri nimesoma naye Chuo Kikuu mwaka 1972, Chikawe kwa hili amesema uongo vinginevyo ajiuzulu, hafai,” alisema Aboubakari.
Alisema kabla ya kufanyika Waziri akifuatana na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Bunge, William
Lukuvi walifika Zanzibar na kutaka wajadili vifungu hivyo kwa siku moja
jambo ambalo alipinga kulitekeleza.
“Baada ya kuanza kupiga kelele, wenzetu walikuja
Zanzibar wakitaka tujadili mabadiliko ya mswada,nikawaambia siwezi
kujadili masilahi ya nchi kijuujuu, huko ni kuiuza nchi, siko tayari
kufanya hilo,” alisema.
Aboubakari alisema marekebisho yaliyofanyika
katika muswada huo na kutoa nafasi kujadili na kupitisha mabadiliko ya
Katiba kwa kutumia wingi wa kura ni sawa na wazimu.
Alisema mabadiliko yoyote ya Katiba yanapaswa
kutumia theluthi mbili toka pande mbili za Muungano, utaratibu ambao
ndiyo umekuwa ukitumika na nchi mbalimbali zenye mfumo kama wa Tanzania.
Mwananchi ilipomtafuta Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe
kujibu tuhuma hizo alisema Aboubakari ameudanganya umma mchana kweupe
kwa vile yeye na Waziri Lukuvi walifika Zanzibar kupeleka rasimu ya
muswada na si kujadili na kupokea mapendekezo papo kwa hapo.
Chikawe alisema kwamba walipokabidhi muswada pia
walimtaarifu siku ya kuwasilishwa muswada huo katika kikao cha Bunge na
kuwataka kutoa maoni na mapendekezo kwa wakati mwafaka kabla ya
kujadiliwa na kamati ya Katiba ya Sheria ya Bunge.
Alisema kwamba nyongeza ya marekebisho ya vifungu
vinane yalitokana na mapendekezo ya wabunge katika kamati na michango ya
wabunge ndani ya Bunge katika utaratibu unaoruhusiwa kisheria.
“Baada ya kamati ya Bunge kukaa, Mbunge Halima
Mdee wa Chadema ndiye aliyependekeza kutumika kwa utaratibu wa wingi wa
kura katika kupitisha mabadiliko hayo ya Katiba kama hatua ya theluthi
mbili itashindwa kufikia mwafaka,” alisema Chikawe.
-mwananchi
-mwananchi