RAIS Jakaya Kikwete amewataka watanzania kuchukua tahadhari dhidi ya
mashambulizi ya kigaidi yanayoweza kutokea hapa nchini kwa kuwa macho na kutoa
taarifa ya watu watakaowashuku katika maeneo yao ya kazi na makazi.
Hata hivyo, alisema Tanzania ilishaanza kuchukua tahadhari kwa
kuimarisha vyombo vyake vya usalama tangu mwaka 1998 lilipotokea shambulio
kwenye Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam na kuua watu 11 na kuongeza kuwa
serikali inaendelea kuchukua hatua za kujilinda na ugaidi, hasa katika maeneo
yenye mkusanyiko wa watu wengi.
“Pamoja na kujizatiti kwetu huko hatuwezi kusema kuwa tukio la kigaidi
halitaweza kutokea nchini. Uhakika huo hatuna kwani hata mataifa makubwa na
tajiri yamesham buliwa. Kilicho muhimu ni kuendelea kuchukua tahadhari na
wananchi kusaidia ili vyombo vyetu vifanikiwe zaidi,” alisema.
Rais ametoa hadhari hiyo siku chache baada ya kutokea shambulio la
kigaidi Septemba 21 mwaka huu, katika jengo la maduka ya kibiashara la Westgate
Nairobi, Kenya, ambapo watu zaidi ya 67 walipoteza maisha huku takribani watu
200 wakijeruhiwa.
Kikwete, ambaye akiwa nchini Marekani katika ziara ya kikazi alituma
salamu za rambirambi kwa Rais Uhuru Kenyatta kutokana na tukio hilo, alisema
jana katika hotuba yake kwa Taifa ya kila mwezi kuwa baada ya tukio hilo la
Kenya, hapa nchini watu wengi wameingiwa hofu kuhusu usalama wa nchi.
“Ni hofu ya msingi kwani Agosti 8 mwaka 1998 Ubalozi wa Marekani hapa
nchini ulishambuliwa na magaidi na ndugu zetu 11 wasio na hatia walipoteza
maisha. Napenda kuwafahamisha kuwa tangu shambulio la mwaka 1998, Serikali
imekuwa inajenga uwezo wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kupambana na
ugaidi katika nyanja mbalimbali,” alisema Rais Kikwete.
Alisema ni dhamira ya serikali kuendelea kujiimarisha bila kusita siku
hadi siku na kwamba Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), Polisi na Idara ya
Usalama wa Taifa wamekuwa na ushirikiano wa karibu kwa ajili hiyo, alisema
juhudi hizo ndizo zinazofanya nchi iwe salama hadi sasa.
Alisema, baada ya tukio la Kenya, vyombo vya ulinzi na usalama
vimeimarisha mikakati yao maradufu. Rais alitoa agizo kwa watu wote wenye
shughuli zinazokusanya watu wengi kama vile maduka, maofisi, mahoteli, migahawa
na nyinginezo kuweka kamera za ulinzi nje na ndani ya maeneo yao na kuangalia
uwezekano wa kuweka vifaa vya upekuzi (metal detectors and x-rays) hata kama
watu wakipiga kelele ya usumbufu, lengo likiwa kuwalinda na mali zao.
“Nawaomba muendelee kufanya shughuli zenu bila ya hofu ingawaje msiache
kuwa makini na kuchukua tahadhari. Watu watoe taarifa kwa vyombo vya usalama
wanapoona mtu au watu au kitu cha kutilia shaka.
Akifafanua kuhusu hilo, Rais alisisitiza kila mtu kuchukua hatua ya kuwa
mlinzi wa usalama wake, wa kila mtu, jamii na taifa kwa ujumla wakati maofisa
husika wa vyombo vya ulinzi na usalama wakiendelea kuelimisha umma kuhusu hatua
mbalimbali za tahadhari za kuchukua.
Rwanda
Kuhusu uhusiano na Rwanda, Kikwete alisema uhusiano baina ya Tanzania na
Rwanda uliokuwa katika sintofahamu, umerejea katika hali nzuri ya awali na
amewataka wanasiasa, watumishi wa umma, wanataaluma na wananchi kwa ujumla
kuuimarisha zaidi.
Rais alisema hatua ya kurejea kwa uhusiano huo ilifikiwa nchini Uganda
alipopata fursa ya kukutana na kuzungumza na Rais wa Rwanda, Paul Kagame
Septemba 5, mwaka huu mjini Kampala katika Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu na
kupata muda wa kuzungumza pamoja hali iliyopo.
Wahamiaji haramu
Akizungumzia uondokaji wa wahamiaji haramu kwa hiari nchini katika mikoa
ya Kigoma, Geita na Kagera na Operesheni ya Kimbunga, Kikwete alisema, alieleza
wazi hatua hiyo ya serikali kuwaondoa watu wanaoishi nchini kinyume cha
utaratibu kitaifa na kimataifa na anafurahi kuwa mambo hayo yamefanikiwa vizuri
na kuzipongeza Idara za serikali zilizohusika kusimamia hilo.
Hata hivyo, alionesha masikitiko yake kwa baadhi ya vyombo vya nje
vilivyopotosha kuwa Tanzania imewafukuza wakimbizi na kueleza kuwa hadi kufikia
Septemba 30 mwaka huu, wakimbizi 68,711 walikuwepo kwenye Kambi ya Nyarugusu,
mkoani Kigoma na kuongeza kuwa ingekuwa hivyo, Shirika la Umoja wa Mataifa la
Wakimbizi, lisingekaa kimya.
“Kumekuwepo na mafanikio ya kutia moyo. Kwa upande wa wahamiaji
wanaoishi nchini kinyume cha sheria watu wapatao 21,254 waliondoka kwa hiyari.
Hali kadhalika zaidi ya ng’ombe 8,000 waliondolewa na silaha 102
zilisalimishwa. Baada ya operesheni kuanza Septemba 6 hadi Septemba 20 mwaka
huu, wahamiaji haramu 12,828 walirejeshwa makwao na watuhumiwa 279 wa
unyang’anyi wa kutumia silaha walikamatwa,” alisema Kikwete.
Alisema madai kuwa Tanzania inawatesa watu walioishi kwa muda mrefu kwa
kuamua kuwaondoa, wakihoji siku zote serikali ilikuwa wapi, hayana tija kwa
kuwa walipewa nafasi ya kuomba uraia na kwamba kigezo cha kuishi muda mrefu
nchi ya kigeni sio kinga ya kupewa uraia ama kuwa raia.
Kikwete alisema hakuna mtu aliyeonewa kwa namna yoyote kwani wapo watu
waliokuwa na madaraka makubwa ilibidi waziachie nyadhifa zao na kuondoka kwa
kuwa ndivyo sheria za nchi na Katiba inavyotaka. Ziara ya Canada na Marekani .
Akiwa nchini Canada na Marekani katika ziara ya kikazi kati ya Septemba
17 na 28 mwaka huu, Kikwete katika hotuba hiyo alisema Chuo Kikuu cha Guelph,
Canada pamoja na kumtunukia Shahada ya Heshima ya Uzamivu kwa kutambua jitihada
za nchi katika kujiletea maendeleo kimekubali kushirikiana na Wizara
zinazohusika na Elimu, Kilimo na Mifugo kuboresha huduma.
“Pia wapo tayari kushirikiana pamoja na Chuo Kikuu cha Kilimo cha
Sokoine (SUA), Morogoro na Chuo Kikuu cha Dodoma. Nimewataka Mawaziri wa Wizara
hizo na viongozi wa vyuo hivyo kuchangamkia fursa hiyo bila kuchelewa,” alisema
Kikwete.
Kuhusu miradi ya umeme na barabara za vijijini zitakazogharamiwa na
serikali ya Marekani kupitia Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), maombi
yamepokewa vizuri na kinachosubiriwa ni miradi ipi itakubaliwa na Bodi ya MCC
ili fedha zitengwe na Bunge la Marekani kwa ajili hiyo.
Baraza Kuu
Alisema lengo kuu ya safari yake Marekani ilikuwa kuhudhuria Mkutano wa
68 wa Umoja wa Mataifa ambako pamoja na mambo mengine ni kuandaa ajenda ya
maendeleo baada ya mwaka 2015.