TAARIFA YA SAMSON MWIGAMBA KWA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU WARAKA WA MKAKATI WA MABADILIKO 2013
Jumatano, 27 Novemba 2013
Jana
katika taarifa kwa waandishi wa habari, Mhe. Tundu Lissu na Mhe. John
Mnyika waliudanganya umma kuhusu waraka unaohusu Mkakati wa Mabadiliko
2013. Katika maelezo yao waheshimiwa hawa, pamoja na mambo mengine,
walidai kuwa waraka uliosambazwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari ni
feki. Ukweli ni kwamba:
Ninathibitisha kwamba waraka uliosambazwa
kwenye vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii ni sahihi
neno kwa neno kama nilivyousoma katika magazeti ya HabariLeo, Jamhuri na
Rai, pamoja na nakala iliyopo Jamii Forum.
Ili kuthibitisha kwamba
waraka ule ndio wenyewe, nawatumieni ‘soft copy’ kutoka kwenye kompyuta
mpakato (laptop) yangu ambako ndiko
ulikoibwa na viongozi wa chama baada ya kunipora kwa nguvu laptop yangu
Oktoba 25 na kukaa nayo hadi jioni ya Oktoba 28.
Naomba kila mtu asome
neno kwa neno waraka ninaowapa leo halafu afananishe na ule uliopo
kwenye magazeti na kwenye mtandao ili mjiridhishe kama kweli sio
wenyewe. Kama Lissu na wenzake wana mpango wa kuuchakachua waraka huu
wamekwama!
Waraka huu si wa uhaini wala mapinduzi wala usaliti
kama inavyodaiwa na akina Lissu. Huu ni waraka wa kusaka ushindi katika
uchaguzi halali ndani ya chama ambao ulikuwa ufanyike Desemba 2013, na
ambao sasa umesogezwa mbele.
Napenda ijulikane kwamba wakati wa
uchaguzi si jambo la ajabu kuwa kwa wanachama kuwaunga mkono wagombea
tofauti. Nimekuwa karibu na Mwenyekiti Mbowe kwa miaka mingi na ninajua
kwamba yeye naye anao mkakati tena unaohusisha mbinu haramu za
kuhakikisha anammaliza Zitto na yeye kupita bila kupingwa kwenye
uchaguzi huo. Wanaoshiriki mkakati wake ni pamoja na Lema, Lissu na
wakurugenzi kadhaa waliopo makao makuu.
Waraka huu ulipaswa kuwa
siri ndani ya watu watatu tu (M1, M2 na M3) na haikutarajiwa kwamba
ungevuja kwa jamii.
Bahati mbaya viongozi wa chama baada ya kuunasa
waraka huu kutoka kwenye komputa yangu mpakato (laptop), na baada ya
kikao cha Kamati Kuu, waliamua, kwa jazba na bila kutumia busara ya
kiuongozi, kuusambaza waraka huo kwenye vyombo vya habari kwa lengo la
kuwakomoa na kuwadhalilisha waandaji.
Sasa baaada ya kugundua madhara ya
waraka huo machoni pa jamii wameamua kuukana. Ni ajabu kwamba wanaukana
waraka ambao waliusambaza wenyewe.
Nasisitiza kwamba mambo
yaliyopo kwenye waraka ni bayana na dhahiri. Sibahatishi kwa sababu mimi
nimefanya kazi makao makuu kama Mhasibu Mkuu hadi Mwezi Aprili 2012.
Ni
kwa kutambua uozo uliopo katika uongozi wa chama makao makuu niliona
umuhimu wa kubadilisha uongozi kwa njia za kidemokrasia ili tukiokoe
chama na hatukuwa na nia wala sababu za kuanika haya yote kwenye umma.
Kwa sababu za chuki na kukosa busara za kiuongozi huyo anayeitwa
Mwanasheria Mkuu akawashauri viongozi wetu kijinga wauanike waraka mbele
ya macho ya watanzania.
Wangekuwa na akili na busara baada ya yote haya kutokea wangejiuzulu au kuitisha uchaguzi mara moja.
Tunatambua
kwamba viongozi wetu wanamchukia Mheshimiwa Zitto Kabwe kwa siku nyingi
sana na wametamani kumfukuza siku nyingi.
Hata hivyo, ninawashauri
watafute sababu nzuri za kumfukuza uongozi na hata uanachama kwa sababu
yeye hahusiki na waraka wetu wa Mkakati wa Mabadiliko 2013 hata chembe,
pamoja na kwamba yeye ndiye alikuwa na bado ndiye mlengwa mkuu, kama
atakubali.
Samson Mwigamba (M3)
Arusha
Samson Mwigamba (M3)
Arusha