
Mbali na kuwatimua mawaziri hao, kamati imeiamuru wizara hiyo kusitisha mara moja matumizi ya viwango vipya vya alama za ufaulu kwa elimu ya sekondari vilivyotarajiwa kuanza kutumika mwaka huu, baada ya kubaini kwamba mchakato huo haufahamiki na Bodi ya Baraza la Mitihani Nchini.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Margaret Sitta, alisema hadi jana Bodi ya NECTA haikuwa imehusishwa wala kupewa fursa ya kujadili mabadiliko hayo, hivyo haiwezi kuruhusu kuendelea na viwango vipya vya ufaulu.
“Kamati imeona kwa kuwa wadau muhimu hawakufikiwa, tumeiambia kuwa kwa matokeo ya mwaka huu watumie alama zilizotumika miaka ya nyuma hadi tuhakikishe suala hili limeeleweka vyema na kufikia wadau wote,” alisema.
Margaret alisema kuwa kamati hiyo imebaini kuwa mchakato huo hadi sasa haujakamilika, hivyo ni vigumu kuendelea na matumizi ya alama hizo mpya za ufaulu.
Aliongeza kuwa watendaji wa wizara hiyo, wameshindwa kuwasilisha ripoti yote ya tume iliyoundwa na Waziri Mkuu Pinda mbele ya kamati na matokeo yake wameleta maelezo ambayo ni vigumu kwa kamati hiyo kuweza kujadili utekelezaji wake.
“Tunasisitiza kuwa wizara ituletee ripoti ili tuyafanyie kazi mapendelezo yaliyotolewa na tume; bila kutuletea hiyo ni vigumu kuweza kujadili.
“Tunaomba ripoti ya tume tupewe yote na wala isiwe nusu nusu ili kuiwezesha kamati kupitia na kubaini matatizo yanayoikabili sekta ya elimu kwa sasa na hapo tunaweza kuja na ufumbuzi,” alisema.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome akitangaza mapema mwezi huu, alisema uamuzi wa kubadilisha mfumo huo umechukuliwa kutokana na changamoto zilizojitokeza mwaka 2012.
Alama zilizokuwa zikitumiwa awali na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), katika kupanga matokeo hayo, kwa Kidato cha Nne ni A=80-100, B=65-79, C=50-64, D=35-49, F 0-34. Kwa upande wa Kidato cha Sita, A=80-100, B=75-79, C=65-74, D=55-64, E=45-54, S=40-44 na F= 0-39.
Alama mpya zilizotangazwa ni A=75-100, B+=60-74, B=50-59, C=40-49, D=30-39, E=20-29 na F=0-19. Alama hizo ni kwa kidato cha nne na sita.
Kwa utaratibu huo, A ilitafsiriwa kuwa ni ufaulu uliojipambanua, B+ ni ufaulu bora sana, B ufaulu mzuri sana, C ufaulu mzuri, D ufaulu hafifu, E ufaulu hafifu sana na F ufaulu usioridhisha.
Katika utaratibu huo, mtihani wa mwisho ulitarajiwa kuwa na alama 60 na alama 40 zitokane na alama za Maendeleo ya Mwanafunzi Shuleni (Continuous Assessment-CA).
Mwaka jana baada ya serikali kufuta matokeo ya mtihani wa Kidato cha Nne, Necta ilitumia CA ya 30 huku mtihani wa mwisho ukiwa na alama 70.