Hatima ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, na wenzake waliovuliwa nyadhifa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), itajulikana Ijumaa wiki hii wakati Kamati Kuu ya chama hicho itakapokutana kuzungumzia sakata hilo na kutoa maamuzi ya mwisho.
Afisa Uhusiano wa Chadema, Tumaini Makene, alisema jana kuwa chama kimewaandikia barua ya kuitwa mbele ya kikao ili wasikilizwe.
Mbali
na Zitto aliyevuliwa unaibu katibu mkuu na Naibu Kiongozi wa Kambi ya
Upinzani, wengine waliovuliwa nafasi zao ni aliyekuwa Mwenyekiti wa
Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk.
Kitila Mkumbo, Novemba 22, mwaka huu kwa tuhuma za kukisaliti chama.
“Chama
kimewaandikia barua hiyo baada ya kuwa kimeshawaandikia barua ya
kuwajulisha kuwa kimeshapokea maelezo yao ya maandishi kuhusu tuhuma 11
walizotuhumiwa nazo. Kwa hiyo wametakiwa kufika kwenye kikao cha Kamati
Kuu Januari 3, mwakani (Ijumaa) ,” alisema.
Makene
alisema wameitwa ili wasikilizwe kutoka midomoni mwao kuhusu tuhuma
zinazowakabili na kwamba hilo limefanyika kwa mujibu wa kanuni ya
uendeshaji chama, katika kifungu cha 6.5.2 (b) na 6.5.2 (d).
Alisema
kifungu hicho kinaelekeza kwamba Kamati Kuu inaweza kuchukua hatua za
dharura bila kuzingatia utaratibu wa (b) na (c) kama itaona maslahi ya
chama kwa ujumla yako hatarini.
“Lakini
katika kuchukua hatua hizo za dharura, mwanachama au kiongozi
anayelalamikiwa atalazimika kuitwa kwenye kikao husika. Hivyo chama
baada ya kupokea maelezo yao ya maandishi sasa wameitwa wajieleze kwa
mdomo. Kila kitu kinakwenda kwa utaratibu hapa,” alisema.
Makene
alisema tangu mwanzo chama kiliweka utaratibu kwa kuzingatia katiba,
kanuni, maadili, taratibu na miongozo ya chama, ndiyo maana ya taasisi.
CHANZO:
NIPASHE