Rais Jakaya Kikwete amezindua ujenzi wa barabara, huku akielezwa kuwa zaidi ya makandarasi 30 nchini ambao wanajenga barabara kwa fedha za ndani wako mbioni kugoma kuendelea na ujenzi huo kutokana na Wakala wa Barabara (Tanroads) kukosa fedha za kuwalipa kwa wakati.
Rais Kikwete yuko katika ziara ya kutembelea Mkoa
wa Simiyu aliouzindua jana na kusema ameunda mikoa mipya kwa ajili ya
kurahisisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo. Mikoa mingine
iliyoundwa ni; Njombe, Geita na Katavi.
Akizungumza mbele ya Rais Jakaya Kikwete, wakati
wa uwekaji wa jiwe la msingi la Ujenzi wa Barabara ya lami ya Bariadi
hadi Lamadi yenye urefu wa kilomita 71.8, Mtendaji Mkuu wa Tanroads,
Patrick Mfugale alisema ni muda mrefu sasa fedha zimekuwa zikichelewa
kufika kwa wakati kwao, hivyo kushindwa kuwalipa makandarasi na
wametishia kugoma kuendelea na kazi ya ujenzi.
Alisema kuchelewa kwa fedha hizo kunakwamisha
ujenzi wa barabara hizo ikiwa ni pamoja na kuitia hasara serikali
kutokana na kulazimika kulipa riba na fidia ya hasara kutokana na
kuchelewa kulipa kwa wakati.
Rais Kikwete alisema atafuatilia suala hilo ikiwa
ni pamoja na kuwahimiza wanaohusika na fedha kuhakikisha zinapatikana
haraka na hivyo kuwaondoa wasiwasi Waziri wa Ujenzi pamoja na
makandarasi.
Awali kabla ya kumkaribisha Rais Kikwete kuzungumza na wananchi, Waziri wa Ujenzi,John
Magufuli alieleza kuwa katika barabara hiyo yenye
urefu wa kilomita 71.8 Serikali imegharimia fedha zote kiasi cha Sh70.9
bilioni.
Alisema katika mradi huo, Serikal imelipa fidia ya
Sh795 milioni kwa wananchi ambao walifuatwa na barabara, lakini pia
imeweza kubomoa nyumba kwa wale ambao walijenga barabarani.
Azindua Benki ya Wananchi Simiyu
Katika ziara hiyo jana, Rais Kikwete alizindua
Benki ya Wananchi wa Simiyu na kuwataka wananchi kutunza fedha zao
katika benki hiyo kwa vile kufanya hivyo kutasaidia kupanga mipango ya
kiuchumi. Alisema benki ni kichocheo cha uchumi na kwamba ili iweze kuwa
na maana ni lazima wananchi waitumie benki hiyo kwa kuweka fedha na
kukopa.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Benki
hiyo, Mhandisi Christopher Sayi akitoa taarifa kwa Rais Kikwete alisema
benki hiyo itachochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa mkoa huo
kwa kutoa huduma za kifedha, mikopo yenye masharti nafuu na fursa ya
kuwekeza mitaji yao.
Alieleza kuwa mchakato wa kuanzisha benki hiyo
unaoratibiwa na kamati maalumu, umeisha kusanya mtaji wa Sh1.8bilioni na
kukamilisha taratibu za kibenki, na kwamba, wanatarajia kufungua
milango na kuanza kutoa huduma Februari mwakani.
-MWANANCHI
-MWANANCHI