MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa
Kilimanjaro, Philemon Ndesamburo, amesema anaafiki mkakati wa kuwafuta
kazi mawaziri wanaokataliwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwenda
mbali zaidi kwa kumtaka Rais Jakaya Kikwete avunje Baraza zima la
Mawaziri.
Ndesamburo, maarufu kama ‘Ndesapesa’ alitoa kauli hiyo jana akiunga
mkono kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM taifa, Nape Nauye,
aliyetaka Rais Kikwete awatimue baadhi ya mawaziri kwa kushindwa
kuwajibika.
Juzi Nape akiwa mjini Songea alimtaka Rais Kikwete kuwafuta kazi
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza,
Naibu wake, Adamu Malima na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk.
Shukuru Kawambwa ambaye ametajwa kuwa sehemu ya matatizo katika kila
wizara anayopewa kuiongoza.
Akizungumzia malalamiko ya CCM kulalamikia baadhi ya mawaziri
kutowajibika, Ndesamburo alisema kelele hizo huenda zikawa kama mchezo
wa kuigiza ili wananchi waone chama hicho kina nia ya kuwawajibisha
mawaziri wake.
“Madai ya CCM kutaka Rais Kikwete awafukuze kazi mawaziri wanne
wanaotajwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ni mazuri, lakini yanaweza
kuwa ‘geresha’ dhidi ya umma wa Watanzania.
“Mimi nasema kama CCM inawatakia mema wananchi wake, basi wamtake
Rais Kikwete avunje Baraza zima la Mawaziri, kwani wengi wamechoka,”
alisema Ndesamburo.
Akitolea mfano Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Ndesamburo
alisema ni mzigo kwa taifa kwani haina mpango wa dhati kwa wakulima
wanaotegemea jembe la mkono, wakati huo huo wakishinikizwa kuuza mazao
yao kwa bei ya chini kwa walanguzi.
Mbunge huyo aliwatahadharisha Watanzania kwamba kauli hiyo ya CCM
inaweza kuwa na nia ya kutafuta huruma ili kishinde kwenye uchaguzi wa
serikali za mitaa mwakani.
Alisema Rais Kikwete anapaswa asingojee fedheha nyingine
itakayotokana na shinikizo la wabunge ama watendaji wakuu wa CCM na
kasi ya CHADEMA katika kufanya uamuzi huo.
Alisema ni vema Rais Kikwete angewaondoa mawaziri hao mapema badala ya kusubiri upepo wa wabunge wake na nguvu ya CHADEMA.