SIKU moja baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kumfutia
kesi raia wa Kenya, Joshua Mulundi, ya kuteka na kujaribu kumuua
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, Jeshi la
Polisi limeanza sarakasi mpya za kutupiana mpira.
Wakati polisi wakikwepa kuwataja wahusika wa tukio hilo, wadau wamedai
kuwa vyombo vya dola vinamkumbatia mmoja wa maofisa wa usalama
aliyetajwa na Ulimboka kuhusika na utekaji huo.
Itakumbukwa kuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova, aliunda jopo la maaofisa kutoka kanda hiyo na makao makuu
kuchunguza tukio hilo na kutamba kuwa halitatokea tena.
Licha ya tambo hizo, hadi sasa jopo hilo halijawahi kutoa hadharani
ripoti ya kile walichokibaini hadi tukio jingine kama hilo likajirudia
Machi 6, mwaka huu, alipotekwa na kuteswa Mwenyekiti wa Jukwaa la
Wahariri nchini, Absalom Kibanda.
Watuhumiwa wa tukio la Kibanda pia hawajakamatwa pamoja na Kova kuunda jopo la uchunguzi.
Alipotafutwa jana kuzungumzia uamuzi wa DPP kumwachia huru Mulundi
kutokana na kutopatikana ushahidi wa kumtia hatiani kutenda kosa hilo,
Kova aligoma katakata kutaja kile kilichobainiwa na jopo la kamati yake
ya uchunguzi.
Badala yake Kamanda Kova alisema suala hilo lilikwisha kuondoka kwao
na kwamba yeyote anayetaka kujua undani wake ni vema akajaribu
kuwasiliana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai
(DCI), Robert Manumba.
Kova alisema masuala yote hayo ikiwamo watuhumiwa kudaiwa kujihusisha na vitendo vya ugaidi hayako kwake.
“Kwanza uliwahi kunisikia hata siku moja nikimuita mtuhumiwa gaidi,
sijawahi, mimi kazi yangu ni kukamata wahalifu mbalimbali wakiwamo wa
magari kama haya niliyowaonyesha baada ya kuibwa na majambazi wanaotumia
silaha,” alisema Kova.
Tanzania Daima lilimtafuta Kamishna Manumba ili kupata undani wa hatua
inayofuata baada ya mtuhumiwa pekee kuachiwa, lakini ofisa huyo naye
alikuwa na majibu ya kukwepa.
“Hivi baada ya kuachiwa kilitokea nini? Si umeona alikamatwa tena?”
alihoji Manumba ingawa alipobanwa kuwa hakukamatwa na kushtakiwa kwa
kosa la kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka, alisema sheria inasema kuwa mtu
yeyote anaposema uongo, moja kwa moja atakuwa ametenda kosa.
Aidha, alipotakiwa kutolea maelezo mtindo uliozuka wa watu
kubambikiziwa kesi za ugaidi, kamishna huyo hakutaka kusikiliza, zaidi
ya kusema: “Kwa heri,” kisha kukata simu yake.
Wadau wahoji
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, baadhi ya wadau hao
walionyesha hofu kwamba kwa sasa kuna hatari ya wananchi kubambikizwa
kesi za baadhi ya watu serikalini wanaofanya vitendo hivyo bila
kuchukuliwa hatua zozote.
Mkurugenzi wa zamani wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
(Tamwa), Ananilea Nkya, alieleza kusikitishwa na kitendo cha polisi
kutomtia hatiani ofisa wa Ikulu aliyetajwa kwa jina la Ramadhani
Ighondu, kuwa ndiye aliyeratibu tukio hilo la kumteka na kumtesa Dk.
Ulimboka.
“Kesi ya Dk. Ulimboka mbona ipo wazi, mtuhumiwa yupo wazi, alitajwa na
aliyeteswa, serikali ndiyo imemlinda. Kwa hali hii tunakuwa na hofu
kuwa vyombo vyetu vya usalama vinatesa watu na kuwalinda watesaji,”
alisema.
Aliongeza kuwa kwa sasa ni kama vile kuna vyombo vya ulinzi vya watu
wachache. Kwamba, Tanzania sasa si salama, hakuna utawala bora, haki za
binadamu hazizingatiwi wala hakuna demokrasia na uhuru wa mawazo.
Hili si jambo la kuchekea, ni suala la kulaaniwa na kuhuzunisha kwa
kila Mtanzania. Ni aibu sana tunapokuwa na serikali inayotesa watu
wake,” alisema.
Nkya aliongeza kuwa kwa hali hii Rais Jakaya Kikwete afafanue
hadharani kwa Watanzania kuhusu tukio hilo, vinginevyo haeleweki vizuri.
Naye Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisema uamuzi wa DPP kuwasilisha
mahakamani hati ya kutoendelea na mashtaka hayo ni ishara ya wazi kuwa
aliona hayana msingi.
Alisema kuwa mashtaka hayo yalifunguliwa kutumia kisingizio cha kesi
kuwa mahakamani ili kudhibiti vyombo vya habari visiandike habari za
uchunguzi kuhusu kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka.
Mnyika pia alifafanua kuwa ilikuwa ni njia ya kuzuia Bunge lisijadili
na kuihoji serikali. “Uamuzi huu wa DPP sasa umefungua mlango kwa vyombo
vya habari kuandika na wabunge kujadili, kwani mmoja wa watuhumiwa ni
ofisa wa Usalama wa Ikulu,” alisema.
Mbunge huyo alisisitiza kuwa kwa uamuzi huo, Inspekta Jenerali wa
Polisi, Said Mwema na Kamanda Kova wajitokeze waseme kuwa walilidanganya
taifa kwa mwaka mzima, na kwamba sasa wawaeleze Watanzania nani hasa
alimteka na kumtesa Dk. Ulimboka.
chanzo:MWANANCHI
|