Kwa ufupi
- Kulingana na vyanzo vya habari, mfanyabiashara huyo alipigiwa simu na kukubaliana kukutana katikati ya mji wa Bomang’ombe na makutano ya Barabara ya Kia katika Barabara Kuu ya Hai kwenda Arusha.
Moshi. Mfanyabiashara tajiri wa Mirerani na
Jijini Arusha, Erasto Msuya, ameuawa kwa kupigwa risasi zaidi ya 20 kwa
kutumia bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG), jana mchana.
Erasto anayemiliki vitega uchumi kadhaa na anayeaminika kuwa miongoni mwa wafanyabiashara wa Mirerani wanaoongoza kwa utajiri,
aliuawa jana saa 7:00 mchana wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
“Eneo la tukio kumeokotwa maganda karibu 21 ya
risasi zinazoaminika ni za SMG, yaani mwili ni matobo kila sehemu kwa
kweli ameuawa kinyama sana,” alisema polisi mmoja wa Kituo cha
Bomang’ombe.
Kufuatia mauaji hayo yaliyotokea kati ya neo la
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) na mji wa Bomang’ombe,
mji huo ulifurika magari ya wachimbaji kutoka Moshi, Arusha na
Mererani.
Habari za uhakika zilieleza kuwa wauaji wake
walikuwa katika pikipiki na baada ya kumminia risasi hizo, walimpora
kibegi ambacho haikujulikana kama kilikuwa na madini ama mamilioni ya
fedha.
Kulingana na vyanzo vya habari, mfanyabiashara
huyo alipigiwa simu na kukubaliana kukutana katikati ya mji wa
Bomang’ombe na makutano ya Barabara ya Kia katika Barabara Kuu ya Hai
kwenda Arusha.
RPC Kilimanjaro afafanua alivyouawa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz
alisema kuwa mfanyabiashara huyo aliuawa saa 7:00 mchana eneo la
Mjohoroni kati ya mji wa Bomang’ombe na makutano ya barabara ya Kia.
“Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa Eransto
alikuwa akitokea Moshi kuelekea Arusha, na alipofika hilo eneo la
Mjohoroni alichepuka na kwenda meta 300 nje ya barabara,” alisema.
Kamanda Boaz alisema alipofika eneo hilo,
alikutana na vijana wawili waliokuwa na pikipiki ambao waliingia ndani
ya gari kwa lengo la kufanya mazungumzo yanayodhaniwa ni ya kibiashara.
Hata hivyo, muda mfupi tu Erasto alishuka kwenye
gari lake na kuanza kukimbia na ndipo mmoja kati ya wale vijana alishuka
kwenye gari la Erasto na kuanza kumminia risasi nyingi.
chanzo:mwananchi
chanzo:mwananchi