RIPOTI ya Wiki imegundua kuwa, fedha ni hatari kwa afya ya binadamu kwani huweza kusababisha madhara makubwa.
Katika
uchunguzi, ilibainika kuwa fedha za noti na zile za sarafu huweza
kukusanya na kusambaza vimelea vya magonjwa hatari kutoka kwa mtu mmoja
kwenda kwa mwingine.
Kuhakikisha ukweli wa jambo hilo, Ripoti ya Wiki ilifanya mahojiano
na mtaalam wa magonjwa mbalimbali, Dk. Richard Marise na kusema kuwa
tafiti mbalimbali duniani zimeripoti kuhusu vimelea vinavyoweza
kusafirishwa kupitia fedha ambavyo ni Staphylococcus Aureus,
Escherichiacoli,Fecal Bacteria na sumu nyingine.
“Tafiti nyingi zilizofanywa katika nchi zilizoendelea, zimegundua
kuwa vimelea hatarishi kwenye fedha hasa za noti ambapo vingi hutokana
na uchafu utokao kwa mwanadamu mwenyewe kwa mfano; kinyesi, mkojo na
jasho.
“Vimelea hivyo kwa pamoja husababisha magonjwa kama boils (magonjwa
ya ngozi) pneumonia, toxic shock syndrome (homa za sumu mwilini),
diarrhea (kuharisha), gum diseases (magonjwa ya fizi), homa za vipindi
na meningitis (uvumbi wa bongo) ambao kama hakuna matibabu huweza
kusababisha kifo,” alisema Dk. Richard.
Akifafanua jinsi fedha zinavyoweza kusafirisha magonjwa, daktari huyo
alisema fedha huweza kushikwa na mtu asiyeosha mikono yake kwa maji
safi na sabuni baada ya kutoka kujisaidia, kisha hela hiyo huweza kutua
mikononi mwa mtu mwingine ambaye huacha jasho lake na kuongeza vimelea
vya magonjwa mengine juu yake.
Mzunguko huo unaweza ukawa mkubwa kufikia hatua ya vimelea kusambaa
kwa mamilioni ya watu hivyo kuifanya jamii kuwa katika hatari zaidi ya
maambukizi ya ugonjwa husika.
Dk. Richard alikazia kuwa, maambukizi hutokea kama mtu aliyeshika
hela hizo atagusa sehemu zenye unyevunyevu kwenye mwili wake kwa mfano
jicho, mdomo na pua ambapo vimelea hivyo vitapata nafasi ya kuingia
ndani ya mwili.
Katika mazingira ya kawaida, fedha zenyewe huhifadhiwa katika
mazingira hatarishi ambapo kuna mifano ya watu kuhifadhi fedha ndani ya
nguo za ndani au kwenye matiti (akina mama zaidi).
Fedha pia huweza kudondoka kwenye uchafu wa aina mbalimbali na kuokotwa kisha ikatumika tena.
Imeelezwa
kuwa, ukiachilia mbali kubeba vimelea vya magonjwa, fedha zinaweza
kubeba sumu na madawa ya kulevya juu yake ikiwa itapitia kwenye mikono
ya mtu aliyeshika vitu hivyo.
“Ni vyema ukatumia fedha kwa uangalifu, usiweke hela mdomoni na
ukumbuke kuosha mikono yako kila mara kwa maji na sabuni ili kujikinga
na maambukizi,” alitahadharisha Dk. Richard.