Arusha. Mbunge wa Arusha,
Godbless Lema, ameendelea kushikilia madai yake kuwa polisi wanahusika
na tukio la bomu lililolipuka katika mkutano wa kampeni ya chama hicho
Viwanja vya Soweto Arusha na kusababisha vifo vya watu wanne.
Lema alitoa madai hayo juzi alipohutubia mkutano wahadhara Viwanja vya Shule ya Msingi Ngarenaro.
Alidai Rais Jakaya Kikwete amegoma kuunda tume
huru ya kimahakama kuchunguza tukio hilo, ili kunusuru polisi na aibu
ya kushiriki uhalifu na mauaji ya raia wasio na hatia.
“Mauaji ya Soweto yalipangwa na kutekelezwa na
polisi, RPC (Kamanda wa Polisi) wa Arusha anajua mpango mzima ndiyo
maana Rais hataki kuunda tume kama Chadema tulivyomuomba, ili
tuwasilishe ushahidi wa video kuonyesha jinsi walivyohusika,” alisema
Lema
Alisema ushindi wa Chadema kata nne za Elerai,
Kimandolu, Themi na Kaloleni ni dalili njema za ushindi kwa nafasi zote
kuanzia udiwani, ubunge na urais Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Naye Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani
Golugwa, alitaka polisi kukitambua na kukiheshimu Chadema na viongozi
wake, kwa sababu ni chama kilichoundwa na kuongozwa kwa kuzingatia
katiba na sheria za nchi.
“Hatutakubali kuonewa, kunyanyaswa wala kupuuzwa kwa sababu iwayo yote,” alisema Golugwa.
Alishukuru ulinzi wa Mungu mlipuko wa bomu, ushindi na walitangaza kuanza vikao vya katiba leo.