Posted by Unknown
Posted on Wednesday, August 14, 2013
Mwenyekiti wa Chama cha demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amesema
amenusurika kuuawa katika matukio matatu yanayotokana na harakati zake
za kisiasa.
Akihutubia umati mkubwa wa wananchi katika mji wa
Meatu mkoani Simiu jana, Mbowe alisema hata kama atauawa hatasikitika na
kwamba Watanzania wasimlilie.
Mbele ya umati huo akiwemo mbunge
wa Maswa, John Shibuda, Mbowe alisema kuna watu ndani na nje ya CHADEMA
ambao wamekuwa wakifanya kila mbinu kuwaangamiza viongozi na makada wa
chama hicho.
Mbowe alisema viongozi wa CHADEMA akiwemo yeye
mwenyewe wamekumbana na misukosuko mingi, ikiwemo yenye kuhatarisha
maisha yao kutoka kwa wanasiasa wasioipenda nchi, lakini kwa neema ya
Mungu wamenusurika.
“Leo hii hata kama nikiuawa, naomba
Watanzania msinililie. Mbele ya jeneza langu, nizikeni huku mkisema
Bwana Alitoa na Bwana Ametwaaa, Jina Lake Lihimidiwe.
“Leo CHADEMA sio ya Slaa wala ya Mbowe bali ya Watanzania iliyojengwa kwa misukosuko mingi na mkono wa Mungu.
“Mmeshuhudia namna viongozi wake walivyonusurika kuuawa na kufungwa, na watu kufunguliwa na kesi mbalimbali.
“Kwa hiyo yeyote awe kiongozi wa CHADEMA au watawala anayetamani kuibomoa chadema hataweza kamwe,” alisema.
Kiongozi huyo alisema wale wote wanaofanya hivyo, wajue kuwa wanapambana na mkono wa Mungu na wamelenga kuwaumiza Watanzania.
“CHADEMA
ina baraka za Mungu na ndio maana imeshinda na kupita katika majaribu
mengi ya watawala ambao wameshindwa kuifuta au kuibomoa,” alisema.
Mbowe
na viongozi wengine wa CHADEMA wako katika ziara ya mikutano ya
mabaraza ya wazi kujadili rasimu ya Katiba mpya ambayo itaendeshwa nchi
nzima kwa nia ya kukusanya maoni ya Watanzania.