HATIMAYE ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora,
kuhusu vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu na mauaji yaliyotokea
Arusha Januari 5, 2011 kwenye maandamano ya CHADEMA imevuja.
Licha ya ripoti hiyo kufichwa kwa kutosomwa hadharani kwenye vyombo
vya habari kutokana na kulishutumu moja kwa moja Jeshi la Polisi,
Tanzania Daima imefanikiwa kuinasa.
Maandamano hayo ya CHADEMA ya kupinga ukiukwaji wa kanuni na sheria
katika uchaguzi wa Meya ya Manispaa ya Arusha, Gaudence Lyimo, licha ya
kuruhusiwa na polisi awali baadaye yalipigwa marufuku na Mkuu wa Jeshi
hilo nchini, IGP Saidi Mwema.
Hata hivyo, CHADEMA walikataa kutii agizo hilo kutokana na taarifa ya
IGP kutowafikia kwa maandishi kama inavyoelekezwa kwa mujibu wa taratibu
za utendaji wa jeshi hilo.
Kufuatia vurugu hizo za polisi na wafuasi wa CHADEMA, watu watatu
waliuawa kwa kupigwa risasi, wengine zaidi yya 30 kujeruhiwa na wafuasi
zaidi ya 70 wakiwemo viongozi waandamizi wa chama ambao walifunguliwa
mashtaka mahakamani.
Kutokana na tukio hilo Tume ya Haki za Binadamu, iliunda tume
iliyochunguza suala hilo Januari 10 hadi 13 mwaka 2011, kwa kuwahoji
viongozi wa CHADEMA mkoa wa Arusha, Jeshi la Polisi, hospitalini
walipolazwa majeruhi na njiani walipoandamana wafuasi wa chama hicho.
Tume hiyo iliongozwa na Kamishna Joaquine De-Mello akiandamana na
ofisa uchunguzi, Philipo Sungu, kutoka idara ya elimu kwa umma na
mafunzo kufuatilia tukio hilo kwa muda wa siku tatu ili kupata picha
halisi.
Lengo kuu lilikuwa kubaini chanzo cha vurugu hiyo, uvunjwaji wa haki
za binadamu ambapo Januari 11, asubuhi tume hiyo ilianza kuonana na
madaktari na wagonjwa majeruhi waliolazwa katika hospitali mbili za
Mount Meru na Seliani.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ambayo gazeti hili linayo nakala yake,
taarifa zilizopatikana katika hospitali zilionyesha kupokelewa kwa
majeruhi 26 katika hospitali ya Mount Meru na wawili Seliani.
Majeruhi watatu walipoteza maisha wakati wakipatiwa matibabu ya awali
hapo hospitali ya Mount Meru, 22 walilazwa katika hospitali ya Mount
Meru na watatu walipatiwa matibabu na kuruhusiwa kuondoka hospitalini.
Ripoti ya madaktari ilithibitisha kuwa vifo hivyo vilitokana na
majeraha ya risasi za moto huku majeruhi wengine wakithibitisha kupigwa
risasi za moto huku wakionyesha majeraha hayo kwenye miili yao.
Licha ya ripoti kuonyesha vitendo hivyo vya uvunjifu wa haki za
binadamu uliofanywa na polisi, inasema kuwa maandamano ya CHADEMA na
mkutano yalikuwa halali na jeshi ndilo lilisababisha fujo hizo kwa
kutofuata sheria.
“Tanzania inajivunia Katiba inayoainisha vipengele mbalimbali
vinavyotambua na kulinda haki za msingi za binadamu, hivyo kama nchi
nyingine inawajibika kwa Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu la
mwaka 1948 (UDHR) ambalo ni mama wa matamko, makubaliano na mikataba ya
vizazi vyote vya haki,” inasema ripoti hiyo.
Kwamba Tanzania kama miongoni mwa nchi wanachama zilizoweka sahihi
na kuridhia mikataba hiyo zinawajibika moja kwa moja
“kuheshimu, kulinda, kutetea na kutekeleza” haki zilizoainishwa
kwenye mikataba husika.
Ripoti hiyo inaongeza kuwa “kanuni za jumla za jeshi la polisi namba
403 kifungu cha kwanza inasema; Mtu yeyote ambaye anataka kuitisha,
kukusanya, kuandaa na mkutano wowote au maandamano katika eneo lolote
hadharani atapaswa kuwasilisha taarifa ya maandishi si chini ya saa 48
kabla ya wakati mkutano au maandamano kufanyika kwa ofisa wa polisi wa
wilaya husika.
Na pindi anapopelekea taarifa kwa maandishi kwa mkuu wa polisi wa
wilaya anaruhusiwa kuendelea kuandaa, kuitisha, kukusanya, kuunda, au
kuandaa mkutano au maandamano kama ilivyopangwa.
Ila mpaka atakapopata taarifa ya maandishi kutoka kwa Afisa Polisi wa
Wilaya husika kueleza sababu za kusitisha maandamano hayo.”
Ripoti hiyo inasema kuwa kwa mujibu wa sheria hiyo, polisi “Officer in
charge” wa eneo katika eneo hilo la Arusha mjini ni OCD wa Arusha Mjini
– ndiye aliyepaswa kutoa maelekezo ya kuzuia maandamano na si Kamanda
wa Polisi wa Mkoa au Inspekta Jenerali wa Polisi.
“Kwa mantiki hii, taarifa ya CHADEMA kwa polisi ilitosha kwa wao
kuendelea na mipango yao ya maandamano na mkutano kama inavyoelezwa
kisheria,” anasomeka taarifa hiyo.
Pia inaonyesha kuwa Sheria Na. tano (5) ya mwaka 1992 ya vyama vya
siasa kifungu cha 11 vifungu vidogo vya (4) na (6) na sheria Na. 1 ya
1939 ya polisi na huduma za mgambo kifungu 43.-(1), (2), zilikidhi pia
hitaji la CHADEMA kuendelea na mipango yao ya maandamano na mkutano wa
hadhara kama ilivyopangwa.
Kwamba Sheria Na.5, 1992 ya vyama vya siasa kifungu 11. — (8)
inasema: kama jeshi la polisi linasitisha maandamano au mkutano taarifa
hizo hutolewa kwa maandishi kueleza sababu, wala si kutumia televisheni,
kama ilivyojitokeza kwa tukio la Arusha.
“Hivyo CHADEMA walikuwa sahihi kwa kuwa hawakupata taarifa ya
kimaandishi licha ya polisi kudai kutoa barua hiyo lakini walishindwa
kuthibitisha madai yao mbele ya tume.
Ripoti hiyo pia inaongeza kuwa askari walifanya vitendo vya
unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya viongozi na waandamanaji hasa
wanawake bila kujali hali zao.
Kwa mfano wanatajwa mbunge wa viti maalum Lucy Owenya na mke wa Katibu
Mkuu wa CHADEMA, Josephine Mushumbusi, kuwa walipigwa na kujeruhiwa
vibaya sehemu mbalimbali za miili yao.
Kwamba viongozi wa CHADEMA na wananchi wengi walikamatwa na kuwekwa rumande katika kituo kikuu cha polisi kati mjini Arusha.
“Askari waliwapiga waandishi wa habari, waliwanyang’anya vifaa vyao
vya kazi na kufuta picha na kazi walizokuwa wanazifanya kwenye
maandamano. Askari na waandamanaji walisababisha uharibifu wa magari na
mali za umma na wananchi.
“Aidha walisababisha upotevu wa mali za wananchi zikiwemo simu mbili
za mkononi za Owenya na fedha tasilimu sh 2,700,000 za majeruhi Ally
Ogaga walizodai kunyang’anywa na askari, wakati Ofisi ya CCM Mkoa wa
Arusha ilivunjwa vioo kwa mawe na waandamanaji na nyumba ya mwananchi
Salum Ally iliungua kwa moto uliosababishwa na mlipuko wa bomu
lililoruka kutoka kwenye gari la polisi,” ilisomeka.
CHANZO:TANZANIA DAIMA