MBUNGE wa Karagwe, Gozbert Blandes (CCM), ameshindwa kufanya
mkutano wa hadhara katika mji wa Kayanga, wilayani humo baada ya kukosa
wananchi wa kuwahutubia.
Blandes alipanga kufanya mkutano wa hadhara mjini Kayanga Jumamosi ya
Agosti 3, mwaka huu, lakini alilazimika kuuahirisha baada ya mahudhurio
ya wananchi kuwa hafifu.
Dalili za mkutano huo kutofanikiwa zilianza kuonekana siku moja kabla
wakati mtu aliyekuwa akitangaza taarifa za kuwepo kwa mkutano huo
kusema: “Wale waliokuwa wakisema Blandes hawezi kufanya mkutano Kayanga
waje wajionee.”
Kauli hiyo iliashiria kuwepo shaka kwa waandaaji wenyewe kuhusu kufanikiwa kwa mkutano huo.
Akitoa taarifa za kuahirishwa kwa mkutano huo, Katibu wa CCM wilayani
humo, Anatory Nshange, alidai kuwa Blandes asingefanya mkutano kutokana
na kuwepo kwa shughuli ya bomoa bomoa ya nyumba mbili za wananchi katika
eneo la Mgakorongo mjini hapa.
Hata hivyo, katibu huyo hakueleza uhusiano wa mkutano wa mbunge na
bomoa bomoa, hasa ikizingatiwa kuwa nyumba zilizobomolewa ni za
wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadena).
“Ndugu wananchi wa Kayanga, leo tulipanga kufanya mkutano wa mbunge
wetu hapa mjini Kayanga, lakini tumeamua kuuahirisha kwa sababu
kumejitokeza bomoa bomoa kule Mgakorongo.
“Tunawaomba radhi sana kwa usumbufu wowote, lakini tunawaahidi tutaandaa mkutano mwingine na tutawataarifu,” alisema Nshange.
Uchunguzi wa Tanzania Daima umebaini kuwa kuahirishwa kwa mkutano huo
kunatokana na kukosekana watu hali iliyosababishwa na mgogoro wa kisiasa
ulioibuka baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kufuatia utata wa
matokeo yaliyompa ushindi Blandes.
Wananchi wengi wa jimbo la Karagwe wanaamini kuwa Blandes hakushinda
uchaguzi huo na kwamba alipora ushindi wa aliyekuwa mgombea wa CHADEMA
kwa kusaidiwa na Jeshi la Polisi wilayani humo.
“Huyu si mbunge wetu; mbunge wetu ni wa CHADEMA. Blandes alipata
ubunge kwa kutumia mitutu ya bunduki za polisi na mabomu ya machozi.
“Hatuwezi kwenda kumsikiliza mtu aliyeingia madarakani kwa njia za
mabavu kwani kukubali kumsikiliza ni sawa na kukubaliana na kuhalalisha
uporaji wa kura aliofanya mwaka 2010,” alisema mwananchi mmoja.
“Hatuwezi kwenda kumsikiliza mtu ambaye aliwaagiza polisi kutufyatulia
risasi za moto na kutupiga mabomu mwaka 2010. “Kwa nini tukamsikilize
mtu aliyekusudia kutuua? Akawahutubie hao polisi wake,” alieleza
mwananchi mwingine ambaye pia hakutaka kuandikwa jina gazetini.
Alipotafutwa mbunge huyo kuzungumzia sababu za kuahirishwa kwa mkutano
wake, alikanusha kupanga kufanya mkutano huo kama ilivyotangazwa na
viongozi wake wa chama.
“Siyo kweli! Sijapanga wala kuandaa mkutano Kayanga, kama hao viongozi
wa CCM wamesema kuwa nimepanga kuhutubia hapo hawakuwa wakweli.
“Labda wao walipanga na walitaka kupata watu kupitia kwangu. Naomba
uniamini mimi maana ubunge wangu hauna ubia na mtu yeyote,” alisem
Blandes na kudai kwa sasa yuko nchini Uganda.
chanzo:Tanzania daima