Tunaweza kusema kwamba kujirudia kwa kasoro hizo ni
uthibitisho kwamba viongozi wa Serikali na vyama tawala katika nchi
nyingi za Afrika hawajawa na utashi wa kisiasa wa kuendesha na kusimamia
chaguzi huru na za haki na kuhakikisha kwamba nyanja za ushindani
zinakuwa sawa na linganifu kwa kila mshindani.
Uchaguzi Mkuu nchini Zimbabwe ulimalizika
Jumatano iliyopita, ambapo Rais Robert Mugabe wa Zanu-PF aliibuka
mshindi kwa kuzoa asilimia 61 ya kura, huku mpinzani wake, Morgan
Tsvangirai wa MDC akipata asilimia 34 ya kura. Kwa ushindi huo, Rais
Mugabe mwenye umri wa miaka 89 ataapishwa kuongoza tena nchi hiyo kwa
muhula wa saba mfululizo.
Hata hivyo, ushindi wa Rais Mugabe umelalamikiwa
na MDC, kwamba kulikuwa na rafu nyingi na wizi wa kura, hivyo chama
hicho kesho kitawasilisha pingamizi katika Mahakama Kuu kupinga ushindi
huo. Chama hicho pia kimesema kitawasilisha waraka wa upungufu wote
uliojitokeza kwa Jumuiya ya Kiuchumi ya Kusini mwa Afrika (SADC) na
kitaiomba jumuiya hiyo iitishe kikao cha dharura kuujadili.
Wakati waangalizi wa Uchaguzi kutoka Jumuiya ya
Afrika (AU) na SADC wakisema uchaguzi huo ulikuwa huru na haki, wenzao
wa Jumuiya ya Ulaya (EU) walisema uchaguzi huo ulikuwa na kasoro nyingi,
ikiwa ni pamoja na udhaifu katika mchakato wa upigaji kura na ukosefu
wa uwazi. Hata hivyo, waangalizi wa AU na SADC walisema kulikuwa na
hitilafu katika Daftari la Wapigakura, kwani baadhi ya wapigakura
hawakuruhusiwa kupiga kura wakati walikuwa na sifa za kufanya hivyo.
Sio nia yetu hata kidogo kuingia kwenye malumbano
na mijadala inayoendelea hivi sasa mahali pengi duniani kuhusu uchaguzi
huo. Wala hatuna mamlaka kisheria na kikatiba kusema uchaguzi huo
ulikuwa huru na haki ama ulikuwa kinyume chake. Hii ni kwa sababu wenye
mamlaka hiyo ni Wazimbabwe wenyewe na mamlaka zilizoko kisheria nchini
humo.
Hivyo, lengo letu ni kuona kama kuna somo lolote
ambalo nchi yetu itakuwa imejifunza kutokana na uchaguzi huo wa
Zimbabwe. Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba kasoro zilizojitokeza
katika uchaguzi huo na kuthibitishwa na waangalizi wa SADC, AU na EU ni
kasoro zilezile ambazo zimekuwa zikitokea katika chaguzi mbalimbali
katika nchi nyingi barani Afrika.
Tunaweza kusema kwamba kujirudia kwa kasoro hizo
ni uthibitisho kwamba viongozi wa Serikali na vyama tawala katika nchi
nyingi za Afrika hawajawa na utashi wa kisiasa wa kuendesha na kusimamia
chaguzi huru na za haki na kuhakikisha kwamba nyanja za ushindani
zinakuwa sawa na linganifu kwa kila mshindani.
Moja ya kasoro kubwa zinazojirudia ni tume za
uchaguzi kushindwa kuratibu na kuhakiki majina ya wapigakura katika
Daftari la Kudumu la Wapigakura. Kama tulivyoshuhudia hapa Tanzania
katika chaguzi zote zilizopita, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kwa
makusudi au kwa uzembe tu imekuwa ikishindwa kuhakikisha kwamba Daftari
hilo linahakikiwa mara kwa mara ili kila mwenye sifa ya kupiga kura
anapata haki hiyo.
Pamoja na kupigiwa kelele nyingi, Nec imeweka
pamba masikioni.Wapigakura wengi wananyimwa haki ya kupiga kura kutokana
na Daftari hilo kuwa na kumbukumbu na takwimu zilizopitwa na wakati.
Nec inazembea kuingiza majina mapya ya watu waliofikisha umri wa kupiga
kura na pia haifuti majina ya watu waliokufa. Tumebakiza wakati mfupi
kuingia kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Matokeo ya hali hiyo bila
shaka ni vurugu na uvunjifu wa amani. Nec isirudie makosa ya nyuma,
ipate somo la Uchaguzi wa Zimbabwe na kwingineko barani Afrika.