Na Raymond Kaminyoge na Kelvin Matandiko
(email the author)
Dar es Salaam. Wanafunzi wa vyuo vikuu wa Chama
cha Mapinduzi (CCM), wameishangaa Tume ya Kurekebisha Katiba kwa
kuyaondoa Maziwa Tanganyika, Victoria na Nyasa kama sehemu ya Jamhuri ya
Muungano kwenye rasimu ya Katiba.
Mwanasheria na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama
cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Kilimanjaro, Evod Mmanda alisema katika
rasimu hiyo haitaji maziwa hayo kama sehemu ya Muungano.Mmanda alisema
hayo kwenye kongamano lililoandaliwa na Vyuo Vikuu mkoa wa CCM.
Rasimu hiyo iliyopo ibara ya pili inasema, “Eneo
la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara ikijumuisha sehemu
yake ya bahari na eneo lote la Zanzibar ikijumuisha sehemu yake ya
bahari,” alisema Mmanda.
“Rasimu hii inaondoa maziwa tuliyonayo nadhani
yataenda katika nchi jirani kwa sababu hayajaonyeshwa kama sehemu ya
Muungano,” alisema.
Alisema watanzania wanatakiwa kupitia vipengele
vyote vilivyopo kwenye rasimu hiyo ili kuweza kupata katiba inayofaa.
Wanafunzi wengi waliohudhuria kongamano hilo walipendekeza Muungano wa
Serikali mbili tofauti na rasimu hiyo inayopendekeza Muungano wa
serikali tatu.
“Hakuna haja ya kuwa na Serikali tatu wakati
tumeshindwa kuisimamia serikali mbili, sasa hivi tujikite kuwa na
muungano wa Serikali moja,” alisema John Magoti, Mwanafunzi wa Chuo
Kikuu cha Mwalimu Nyerere.
Alipendekeza wagombea wa ubunge kuwa na umri wa miaka 18 badala ya 25 kama inavyopendekezwa na rasimu hiyo.
“Kama mwenye miaka 18 anaruhusiwa kupiga kura, iweje kugombea iwe miaka 25, huku ni kuwanyima haki vijana,” alisema.
Naye Justine Mkude wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, alisema kwa kuwa na serikali tatu kutakuwa na gharama kubwa za uendeshaji.
“Tutatue kero zilizopo katika muungano na si kuongeza mzigo mwingine,” alisema.
Mlezi wa Mkoa wa Vyuo Vikuu wa CCM, Januari
Makamba alitaka vijana wasomi kugombea nafasi mbalimbali ya uongozi na
kwamba wasiwaachie wababaishaji.
“Ni lazima nchi hii iongozwe na vijana wasomi tusiwaachie wababaishaji hatutafika kule tunakokwenda,” alisema Makamba.
-MWANANCHI
-MWANANCHI