Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha
Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, alisema hayo wakati
alipozungumza na gazeti hili kuhusu kutafuta watumishi hewa, ambao
wanadaiwa wapo katika baadhi za wizara za SMZ.
Alisema utaratibu wa kuhakiki na kulipa
mishahara ya watumishi ofisini, umeanza kwa wafanyakazi wa Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Amali, pamoja na walimu wote wa shule za unguja na
Pemba.
“Wizara ya Fedha, Uchumi na Mipango ya
Maendeleo, imesikiliza kilio cha wawakilishi na sasa tumeanza kuhakiki
watumishi wote kwa kurudisha utaratibu wa zamani wa kupokea mishahara
ofisini na sio katika benki,” alisema.
Akifafanua zaidi, Mzee alisema Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, imepewa kazi ya kuhakiki watumishi wote wa SMZ.
Alisema Serikali imesimamisha utaratibu
wa watumishi wake waliokuwa wakipokea mishahara katika benki mbali mbali
kwa muda, ili kutoa nafasi ya uhakiki.
Mzee alisema mara baada ya kukamilika
kwa uhakiki wa watumishi hewa, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za
Serikali, atakagua watumishi wastaafu wanaopokea viinua mgongo ili
kutafuta wastaafu halali.
Alisema juhudi hizo zinazochukuliwa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, lengo lake ni kufichua watendaji
wanaojishughulisha na ubadhirifu wa mali za umma.
Kauli ya Mzee iliungwa mkono na
Mwenyekiti wa Kuchunguza Hesabu za Mashirika ya Serikali (PAC), Omar Ali
Shehe, wakati akiwasilisha maoni ya kamati hiyo.
Alisema uchunguzi umebainika kwamba
mashirika ya umma na vikosi vya Serikali upo ubadhirifu mkubwa
unaotokana na ukiukwaji wa taratibu za mahesabu.
Shehe aliitaka Serikali kufanya ukaguzi
wa mishahara ya watumishi wa Serikali katika Wizara ya Nchi Ofisi ya
Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambako viko vikosi vya SMZ.
“Tunaitaka Serikali mara baada ya
kumaliza kazi ya kuhakiki watumishi katika Wizara ya Elimu iendelee moja
kwa moja katika Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,”
alisema.
Mwishoni mwaka jana watumishi hewa
kadhaa walibainika katika Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi na vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.