Zikiwa zimesalia saa 24 kabla ya kumalizika kwa muda uliotolewa
na Rais Jakaya Kikwete kwa wahamiaji haramu kuondoka nchini au
kuhalalisha ukaazi wao na wenye silaha kuzisalimisha, makundi ya
wahamiaji hao, yameanza kuondoka kwa hiari.
Wastani wa wahamiaji haramu 150 wanaendelea
kujiandikisha kuvuka mpaka katika Kituo cha Rusumo, Ngara mkoani Kagera
kutekeleza agizo hilo.
Ofisa Uhamiaji wa Kituo cha Rusumo, Samweli
Mahirane alisema mpaka sasa Wanyarwanda 520 wameshaondoka katika maeneo
mbalimbali ndani na nje ya Ngara na kurejea makwao huku Mkuu wa Mkoa wa
Kagera, Fabian Massawe akisema silaha 17 za aina mbalimbali
zimesalimishwa.
Mahirane alisema wahamiaji hao wanatokea katika
vijiji vya Wilaya za Ngara, Karagwe, Kyerwa, Biharamulo na Geita pamoja
na Runzewe na wamekuwa wakiishi katika maeneo hayo bila vibali halali.
“Kuondoka kwa hiari kwa wahamiaji haramu,
kutahitimishwa Jumatatu Agosti 12 na baada ya tarehe hiyo, vyombo vya
dola vitaanza kufanya kazi kama agizo la Rais Kikwete lilivyoelekeza
katika Mikoa ya Kagera na Kigoma,” alisema.
Aliwahakikishia wahamiaji hao usalama katika
mataifa yao kwani hivi karibuni Serikali ya Rwanda ilikubali kuwapokea
hata walio na mifugo kwa masharti kuwa ndani ya kipindi kifupi
wataipunguza kwa kuiuza na kuboresha maisha yao.
“Rwanda wanahitaji mifugo michache, hivyo walio na
mingi wanatakiwa kuipunguza kwa kuuza na kujenga makazi bora ikiwa ni
pamoja na kuhifadhi ama kulinda mazingira ya nchi hiyo,” alisema
Mahirane.