Wakuu wa Utaliana wameopoa maiti 6 za wahamiaji kutoka pwani inayopendwa na watalii, Catania, katika kisiwa cha Sicily.
Inaarifiwa kuwa mashua hiyo ndogo yenye injini ilinasa kwenye mchanga, mita 15 tu kutoka ufukweni; baadhi ya abiria walizama kwa sababu ya kutojua kuogelea.
Inaarifiwa kuwa Wasyria na Wamisri ndio kati ya mamia ya watu waliowasili Utaliana katika siku chache zilizopita.
Bandari ya Catania, mji wa pili kwa ukubwa kisiwani Sicily, ilikuwa kwenye mtafaruku wakati uokozi unaendelea.
Meli kubwa ya watalii zaidi ya 12,000 ilikuwa imetia nanga hapo piya.
Wakuu wa Utaliana walishughulika zaidi na familia za wakimbizi waliochoka, ambao wanasema waliondoka Mashariki ya Kati wiki mbili zilizopita na walibadilisha mashua njiani.
Mabasi ya watalii yalipishana njia na magari ya waokozi na ya kubeba wagonjwa.
Kwa vile bahari imekuwa shuwari katika siku za karibuni, kwa hivo wakimbizi zaidi wamewasili katika visiwa vya Utaliana vya Sicily na Lampedusa kutoka Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.
Hilo ndilo wimbi kubwa kabisa la wakimbizi kutoka Syria kufika katika kisiwa hicho kwenye bahari ya Mediterranean.
Magengi yanayopanga safari hizo za wakimbizi wanapata faida kubwa, na wanawabwaga wakimbizi hao mara moja wakishaona walinzi wa pwani wa Utaliana au Malta.