Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa,
Serikali imesalimu amri kwa kuamua kupunguza kodi ya barabara kwa malori yanayotoa bidhaa nchini Rwanda kuja nchini kutoka Dola za Marekani 500 hadi 152.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Serikali ya Rwanda kucharuka na kupandisha ushuru kwa malori yanayotoa bidhaa nchini kwenda Rwanda kutoka Dola za Marekani 152 ilizokuwa inatoza hadi 500 ili ziwe sawa na kiwango kilichokuwa kinatozwa na Tanzania.
Kutokana na uamuzi huo wa Rwanda, malori yaliyokuwa yanatokea Tanzania yalilazimika kukwama katika mpaka wa Rusumo kwa muda mrefu kabla ya Serikali ya Tanzania kufanya mazungumzo na serikali ya nchi hiyo na hatimaye wakapata muafaka.
Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, alisema jana kuwa Tanzania imekubaliana na Rwanda kutoza viwango sawa vya ushuru, ambavyo ni Dola za Marekani 152.
Dk. Mgimwa alisema malori yanayotoka nchini kwenda Rwanda ni kati ya 200 hadi 300 wakati yale yanayotoka Rwanda kuingia nchini ni kati ya 20 hadi 30, hivyo biashara hiyo ikikwama kutokana na mgogoro wa ushuru Tanzania ndiyo inayoweza kupata hasara.
Alisema sababu ya Tanzania kukubali kupunguza ushuru huo ni kutaka kunusuru uchumi wake kwa kuwa malori yanapokwama mpakani kunasababisha uchumi kukwama.
Waziri Mgimwa alisema awali walikuwa wanatoza ushuru mkubwa kuliko Rwanda kutokana na kuwa na sehemu ndefu ya barabara kutoka Dar es Salaam hadi Rwanda.Alisema kutoka Dar es Salaam hadi mpaka wa Rusumo ni kilomita 1,350, wakati kutoka katika mpaka huo hadi mji wa Kigali Rwanda hazifiki kilomita 300.
Alisema kwa kiasi kikubwa barabara za Tanzania ndizo zinatumika zaidi kuliko za Rwanda na kwamba, ushuru huo wa Dola za Marekani uliokuwa unatozwa awali ulikuwa sahihi.
Kuhusu wafadhili kuchangia katika bajeti ya serikali, Dk. Mgimwa alisema mwitikio wake ni mzuri na kwamba, kwa kiasi kikubwa fedha walizoahidi wamezitoa, ambazo zimeendelea kuisaidia serikali kutekeleza mipango yake ya maendeleo.
Akizungumzia deni la taifa, Dk. Mgimwa alisema kwa sasa limefikia Dola za Marekani bilioni 16.4, na kusisitiza kuwa bado nchi inaweza kukopa nje.
Alisema serikali inaendelea na jitihada za kulipa deni hilo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kukopesheka inapohitaji kufanya hivyo.
Kuhusu chenji ya rada kutumika kununulia madawati ya shule, Dk. Mgimwa alisema Sh. bilioni 76.4 zilipelekwa kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
CHANZO:
NIPASHE