muhtasari

Home » , , , » DR.SILAA AINANGA CCM NI KULEE MAREKANI...

DR.SILAA AINANGA CCM NI KULEE MAREKANI...






ZIARA ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa nchini Merekani imezidi kuwa gumzo kutokana na mapokezi makubwa anayoyapata katika maeneo mbalimbali, huku akiinanga Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa ina ukubwa wa Baraza la Mawaziri lisilokuwa na tija.
Dk. Slaa ambaye yuko Marekani kwa siku kadhaa katika ziara yake iliyoandaliwa na umoja wa vyuo vikubwa nchini humo ya kujifunza mambo mbalimbali, juzi aliingia katika jimbo la Alabama na kupokelewa na wakuu wa jimbo hilo akiwemo Gavana Robert J. Bentley pamoja na Waziri wa Biashara.
Alabama ambayo uchumi wake ulitegemea kilimo kwa asilimia 90 ni moja ya majimbo yaliyokuwa nyuma sana kiuchumi na kimaendeleo siku za nyuma, lakini miaka 25 iliyopita, viongozi wake walibuni mikakatati ya kuibadilisha.
Kwa sasa jimbo hilo ndilo moja ya majimbo yenye viwanda vikubwa vya magari kama Honda, Mercedes Benz, Airbus, Hyundai, Raytheon, Space Station, Wallgreens na mengineyo, na uchumi wake unakua kwa kasi kubwa.
Kupitia kaulimbiu yake ya “Vision Tanzania” Dk. Slaa alipata nafasi ya kukutana na viongozi wa jimbo hilo ili aweze kujifunza mbinu ambayo ataweza kuwarudishia Watanzania ili nao waondokane na umasikini.
Kwa mujibu wa taarifa za mitandao ya kijamii, gavana wa jimbo hilo pamoja na mawaziri wake, wako tayari kushirikiana na Tanzania kwenye mambo ya biashara, hasa miundombinu ikiwemo bandari na ujenzi wa madaraja na bandari.
Katika ziara yake jimboni humo, Dk. Slaa na mkewe Josephine walipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo bandari kubwa.
Katibu mkuu huyo, alisema kuwa alichojifunza ni kwamba, serikali inaweza kuwa na ufanisi hata ikiwa na baraza dogo la mawaziri.
Kwamba Jimbo la Alabama lina mawaziri sita tu, huku Serikali ya CCM ikiwapa walipakodi wa Tanzania mawaziri zaidi ya 50 wasiokuwa na kazi.
“Mawaziri wengi wana matumizi makubwa huku wakina mama wakijifungua sakafuni, walimu wakinyimwa haki zao, polisi na wanajeshi wakiishi hali duni na wanafunzi wakisoma chini ya miembe. CCM ni janga kubwa lililowakumba Watanzania,” alinukuliwa Dk. Slaa.
Katika ziara hiyo, Dk. Slaa alipata nafasi ya kutembelea Chuo Kikuu cha Auburn ambacho ni moja ya vyuo vikuu vikubwa zaidi vya utafiti duniani.
Auburn inafanya shughuli zake nchini Kenya, Uganda, Senegal na kwingineko barani Afrika. Nchini Kenya, Auburn inawasaidia wakulima mbalimbali hasa wafugaji wa samaki kutumia teknolojia ya kisasa inayowawezesha kusafirisha samaki wengi kwenda Ulaya.
Katika Kenya na Uganda, utafiti wao umetoa zaidi ya ajira 7,000.
Kwamba watafiti hao walipoulizwa kwa nini walikwepa Tanzania, walidai kuwa ni vigumu sana kufanya kazi  wakitaja kuzuiwa na vitendo vya ufisadi ingawa wangekuja na fedha zao kutoka Benki ya Dunia na Shirika la Kimarekani la Misaada (USAID) ambayo inadhamini miradi yao sehemu nyingi barani Afrika ikiwemo Kenya na Uganda.
Taarifa hiyo ilidai kuwa viongozi wa chuo hicho wako tayari kurudi Tanzania ikiwa mazingira ya kazi yatabadilika hasa kukiwepo na serikali mbadala, ambayo Dk. Slaa amewahakikishia kwamba CHADEMA iko tayari kufanya nao kazi.
Kwamba viongozi wa Auburn wako tayari kusaidia vyuo vya Tanzania kama kile cha Kilimo cha Sokoine mkoani Morogoro kwa kuwafundisha walimu na pia kubadilishana nao teknolojia za kisasa za kilimo pamoja na kuwafundisha wakulima wa aina zote na hata walaji mbalimbali.
Dk. Slaa alifika pia katika moja ya bandari kubwa nchini Marekani ya Mobile Alabama ambako alipokelewa na Mkurugenzi wa Shirika la Bandari ya Alabama.
Akiwa hapo alielezwa kuwa shirika hilo linapitisha makontena 100 kwa saa moja na mizigo inayozidi tani milioni 30 kwa mwaka na kuipa bandari hiyo inayojitegemea kiasi cha dola za Kimarekani milioni 152 kwa mwaka ambazo ni faida.
Shirika hilo la bandari lina wafanyakazi 600 tu, lakini limeweza kutoa ajira ambazo siyo za moja kwa moja 280,000.
Akieleza kile alichojifunza bandarini hapo, Dk. Slaa alisema kuwa mashirika ya umma yanaweza kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa pasipo uingiliaji wa kisiasa.
Dk. Slaa pia alijifunza kwamba kama jimbo dogo kama Alabama linaweza kupitisha tani milioni 30 kwa mwaka, basi Tanzania inaweza kupitisha tani milioni 100 kwa mwaka kutokana na jiografia yake.
Alisema kuwa anaamini kwamba bandari ya Tanzania inaweza kuajiri vijana 350,000 chini ya utawala wa CHADEMA.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, anaamini kwamba mashirika ya umma kama bandari hayana ufanisi kwa sababu waendeshaji wake wanateuliwa kiurafiki na kindugu bila ya kuzingatia uwezo wa mtu.
“China ya utawala wa CHADEMA haya yote yatafikia kikomo kwa manufaa ya Watanzania wanaoumia na umasikini,” alisema.
Pia Dk. Slaa alikutana na viongozi wa juu wawili wa Baraza la Biashara la Alabama katika chakula cha jioni kilichoandaliwa kwa ajili yake na taasisi hiyo.
Mwenyekiti wa baraza hilo, ameahidi kuhamasisha makampuni makubwa kwenye jimbo la Alabama kumsaidia Dk. Slaa na CHADEMA kunyanyua uchumi wa Tanzania kwa kuwekeza kwenye sekta mbalimbali za uchumi kama kilimo, elimu, viwanda, miundombinu na nishati.
-Tanzania daima

Popular Post

 
Support : OBAMA | OBAMA | OBAMA
Copyright © 2013. DiraYaLeo - All Rights Reserved
Template Created by Barakaeli Aremu Published by Dira Ya Leo
Proudly powered by Blogger