·
SERIKALI kupitia wakala wa Serikali Mtandao (EGA) imefanya mapinduzi
makubwa ya kuboresha huduma zake kwa kuanzisha tovuti mpya itakayokuwa dirisha
huru la kila mwananchi kuihoji wakati wowote na kupata majawabu ya haraka ya
kero zao katika sekta yoyote ya umma nchini.
Sambamba na hilo, kila kijiji na mtaa kote nchini kunaandaliwa utaratibu
wa kuanzishwa kituo cha teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) sambamba
na kuweka mfumo rahisi wa mawasiliano ya simu zisizo na mtandao wa intaneti ili
kuwezesha wakazi wa vijijini kuwasiliana na serikali moja kwa moja.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue aliyasema hayo jana
alipozungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za EGA mara baada ya kufanya
ziara ya kawaida ya kikazi kujionea utendaji kazi wa wakala huo katika kipindi
cha mwaka mmoja tangu ulipoanzishwa.
Wakala huo ulianzishwa Julai mwaka jana (2012). Ingawa hakueleza ni lini
hasa tovuti hiyo itazinduliwa rasmi, Balozi Sefue alisema muda mfupi ujao
itazinduliwa na kwa sasa ipo katika hatua za mwisho za kukamilishwa.
Alisema maboresho makubwa yanatokana na kuwepo kwa Mkongo wa Taifa
unaowezesha huduma moja kutolewa kwa watu wengi kwa wakati mmoja.
Ofisa Mkuu Mtendaji wa EGA, Dk Jabiri Bakari aliwaambia waandishi kuwa
hivi sasa tovuti hiyo iitwayo www.tanzania.go.tz ipo hewani na mwananchi
anaweza kuingia na kupata taarifa muhimu za serikali ambazo awali hakuwa na
uwezo wa kuzipata ili kujibu maswali ya kero zinazomkabili katika eneo lake.
Akitoa mfano wa namna ya utatuzi wa kero, Balozi Sefue alisema, ikiwa
wakulima katika eneo fulani mazao yao yamevamiwa na ugonjwa usiojulikana,
wanaweza kupiga picha sehemu iliyodhurika na kuituma kwenye mtandao na kisha
watapata jibu la aina gani ya dawa watumie kumaliza tatizo bila kuhitaji
mtaalamu kufika walipo.
Hata hivyo, Balozi Sefue alikiri kuwepo kwa changamoto kadhaa za
matumizi ya Tehama, ikiwemo wizi wa nyaraka za siri za serikali, uhalifu wa
mtandao lakini alisema serikali haiwezi kukwepa kutumia teknolojia hiyo, ila
cha msingi ni kuweka utaratibu na sheria zitakazowezesha utekelezaji wake.
“Kama mnavyofahamu Tanzania imeingia katika mpango wa Shughuli za
Serikali kwa Uwazi (Open Government Partnership-OGP), mambo yote ya utendaji wa
serikali kwa umma yasio siri, yaweze kupatikana, na mifumo hii ikikamilika,
kila mwananchi asiogope kutumia kwa uhuru, mfano kuhoji miradi ya maji, kilimo,
umeme, kila kitu kitaelezwa na kujibiwa,” alisema Balozi Sefue.
-habarileo