MGOMO wa malori na mabasi kupinga Sheria ya Barabara inayowataka
wasiongeze mizigo kupita kiwango cha mwisho cha uzito, umeingia katika sura
nyingine ambapo baadhi ya wasemaji wa wamiliki, wamewasingizia viongozi kuwa
wamelegeza msimamo.
Msimamo wa Serikali kwa mujibu wa Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, ni
kuzingatia sheria ambayo inataka magari hayo yasizidishe mzigo kupita kiwango
cha juu kilichowekwa kisheria cha tani 56 kwa kila lori.
Wamiliki wa malori kupitia Chama cha Wamiliki wa Malori (TATOA), wanashinikiza
Serikali irejee katika makubaliano ya mwaka 2006, ambapo waliruhusiwa kwa
barua, kuendelea na safari bila kutozwa faini, kama mzigo utazidi tani 56,
lakini si kwa zaidi ya asilimia tano.
Jana asubuhi, taarifa zilizotangazwa kupitia vyombo mbalimbali vya
habari na kusambaa, zilidai kuwa Dk Magufuli angezungumza katika ukumbi wa
Idara ya Habari (Maelezo), kuhusu mabadiliko ya msimamo huo.
Taarifa hizo zilisababisha ukumbi huo kujaa waandishi wakimtarajia Dk
Magufuli, lakini wakaambulia kukutana na wamiliki wa malori.
Wamiliki
Wakizungumza katika mkutano huo, wamiliki hao walidai hawajagoma na
hawana sababu ya kugoma, badala yake wameegesha magari yao hadi hapo
watakapopatiwa suluhu ya Sheria ya Barabara inayosababisha kuondolewa ruhusa ya
kuzidisha mzigo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana Dar es Salaam, wamiliki hao
walidai wao ni wafanyabiashara waliochukua mikopo katika mabenki mbalimbali na
hawana sababu ya kugoma, bali wamepaki ili wasiharibu barabara.
Mmoja wa wamiliki hao, Davis Mosha alisema walipata barua inayohusu
kuondolewa kiwango hicho cha ziada ya mizigo juu ya kiwango cha kisheria,
lakini jambo lililowashangaza ni kukosa muda wa kujadiliana na mamlaka
zilizohusika kutoa maamuzi hayo.
“Sisi hatujagoma, na wala hatutagoma, tumepaki ili tusiharibu barabara
kwani tungepakia tungezidisha foleni barabarani…tunataka kufikisha kilio chetu
kwa Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli ili suluhu ipatikane,” alisema Mosha na
kuongeza wangeendelea kusafirisha mizigo na malori hayo, kungekuwa na msongamano
mkubwa.
Alisema wao kama wasafirishaji ni wadau wakubwa katika kulinda
miundombinu hiyo na hawako kwa ajili ya kubishana ila wanahitaji sheria
kufuatwa.
Alisema kwa sasa mafuta hayaendi mikoani jambo ambalo linaweza
kusababisha mgongano na kuiomba Serikali kutoa uamuzi haraka kuhusu sheria
hiyo.
Mahakamani vipi?
Kuhusu kwenda mahakamami kama hawakuridhika na uamuzi huo wa Serikali,
alisema kuwa wao ni wastaarabu wanaotoa huduma katika jamii na hawakutaka
kukurupuka kwenda mahakamani kudai haki yao ila bado wanaiheshimu Serikali yao.
Alisema haoni sababu ya kwenda mahakamani kwa kuwa bado wanasubiri
Serikali itoe majibu kwani kuendelea kubishana wataonekana kutokuwa na nidhamu.
Mmiliki mwingine, Ibrahim Ismail kutoka Usangu Logistic, alisema
wamepata usumbufu mkubwa na tatizo kubwa ni mizani kutokuwa na viwango vilivyo
sawa.
Faisal Edha kutoka Overland Logistic, alisema asilimia hiyo haipo
Tanzania peke yake, bali pia ipo katika nchi wanachama wa Jumuiya za Afrika
Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC).
Magufuli alikimbia?
Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Martin Ntemo alipoulizwa na gazeti hili
kama Dk Magufuli alikuwa na mkutano wowote na waandishi wa habari leo, alisema
hakukuwa na mkutano wa aina hiyo.
Badala yake alisema Wizara haijabadilisha msimamo na Dk Magufuli, ametoa
pongezi kwa kampuni za usafirishaji ambazo zimekuwa zikiendelea na usafirishaji
na hazijawahi kuzidisha uzito kwa miaka 10.
Alisema kampuni hizo zimekuwa mfano wa kuigwa kwa kuheshimu sheria na
taratibu za usafirishaji hapa nchini kwa kujaza uzito unaotakiwa na chini ya
hapo kiwango kilichowekwa na sheria.
“Uchambuzi uliofanyika kwa kuangalia kipindi cha miaka 10, tumebaini
kampuni ambazo hazina rekodi ya kuzidisha mizigo wakati wote magari yao
yanapopimwa katika vituo vya mizani ya barabarani,” alisema na kuongeza kuwa
kampuni za aina hiyo ni za kupongezwa kutokana na uzalendo na kuzingatia weledi
katika uendeshaji wa shughuli zao za usafirishaji.
Magufuli alitaja kampuni hizo kuwa ni Dar Express, Cargo Star, Hood Bus,
Coca-Cola, BM Coach, Bakhresa (AZAM Transport), Kampuni ya Bia Tanzania (TBL),
Golden Coach, Kanji Lanji Bus, Taqwa, Consolidate Logistic, Lamada na BP ambayo
sasa inaendeshwa na Puma.
Magufuli alisema Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ilitangaza upya
nafasi za kazi katika mizani na kuwabadilisha wafanyakazi takribani 400, sawa
na asilimia 85, hatua ambayo imedhibiti mianya ya kupitisha mizigo kinyume na
taratibu na kukata mawasiliano kati ya wasafirishaji na watendaji hao.-habarileo