JOPO la majaji watatu wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, limekataa
pingamizi lililowekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kutaka kampuni za simu
zisiingie katika kesi ya kupinga tozo ya Sh 1,000 kwa mwezi kwa kila mmiliki wa
laini moja ya simu.
Uamuzi huo ulitolewa jana na majaji hao; Lawrence Kaduri, Aloysius
Mujuluzi na Salvatory Bongole, ambao sasa wameruhusu kampuni hizo za simu
kujiunga katika kesi hiyo zikiwa walalamikaji namba mbili mpaka sita.
Katika pingamizi la kutaka kampuni hizo za simu zisiruhusiwe kujiunga
katika kesi hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikuwa akidai kuwa hana uhakika
na mtu aliyeapa kwa niaba ya kampuni hizo kama alipewa mamlaka ya kufanya
hivyo.
Upande wa Serikali uliweka pingamizi hilo dhidi ya kampuni ya Mic
Tanzania yenye mtandao wa Tigo, Vodacom Tanzania, Airtel Tanzania, Zanzibar
Telecommunication Limited (Zantel) na Tanzania Telecommunication Company
Limited (TTCL).
Akisoma uamuzi huo, Jaji Bongole alisema hakuna hoja ya msingi ya
kupinga kampuni hizo kuingia katika kesi hiyo. Mawakili wa kampuni za simu
Fatma Karume na Beatus Malima, wameomba kufanya mabadiliko katika hati ya
madai, ambapo wametakiwa wayawasilishe Jumanne ijayo na kesi ya msingi ya
kupinga tozo hiyo ya laini za simu, itaendelea Oktoba 21, mwaka huu.
Kesi ya Msingi
Kesi ya msingi ilifunguliwa na Chama cha Kutetea Walaji, chini ya hati
ya dharura kuomba Mahakama itangaze kuwa Sheria iliyopitishwa na Bunge
inayotaka kila mmiliki wa laini moja ya simu ya mkononi kukatwa Sh 1,000 kila
mwezi, ni kandamizi.
Taasisi hiyo inadai kuwa watumiaji wengi wa simu za mkononi, hawana
uwezo wa kukatwa fedha hiyo kwa mwezi na kusisitiza kuwa sheria hiyo
ikitekelezwa, itaathiri watumiaji wa huduma hiyo nchini.
Kwa mujibu wa madai ya chama hicho, sheria hiyo inakiuka matakwa ya
Katiba ya nchi ya uhuru wa kupashana habari. Pia chama hicho kinataka Mahakama
imzuie Waziri wa Fedha kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA), kutoza kodi hiyo hadi
maombi yao yatakapotolewa uamuzi.
TRA waendelea kudai
Mwezi uliopita TRA iliandikia waraka kwa kampuni za simu nchini kuzitaka
zianze kukata kodi mpya ya laini mara moja.
Kodi hiyo mpya ilipitishwa wakati wa Bunge la Bajeti ya mwaka huu wa
fedha wa 2013/2014, ambapo TRA katika waraka huo, imetaka utekelezaji wake
uanze Julai 30, ili kusaidia shughuli za bajeti ya Serikali Kuu.
Kama kampuni hizo zikianza kutekeleza matakwa ya waraka huo, kila
Mtanzania anayemiliki laini moja ya simu, atakuwa akidaiwa Sh 3,000 mpaka
mwishoni mwa mwezi uliopita.
Mkurugenzi wa Elimu kwa Mteja, Huduma na Mapato wa TRA, Richard Kayombo,
alikiri TRA kutoa agizo hilo lakini hakutaka kuzungumnia zaidi kwa kuwa tayari
suala hilo liko mahakamani ambapo alisema si vema kuingilia uhuru wa mhimili
huo wa Dola.
“Sitaki kuzungumzia kiundani sana suala hili, lakini ukweli ni kwamba
kampuni hizi za simu zimeandikiwa waraka kuanza kulipa kodi na tumeandika kwa
ajili ya utekelezaji wa kodi hii mpya,” alisema Kayombo.