muhtasari

Home » , » Mitambo ya Symbion yazua jambo Arusha...

Mitambo ya Symbion yazua jambo Arusha...


Mitambo ya Symbion, Njiro Arusha

WAKATI wakazi wengi wa Arusha wakiendelea kupata huduma ya umeme unaozalishwa na Mitambo ya Kampuni ya Symbion (T) Ltd, afya za wakazi wenzao zaidi ya 300 wanaoishi eneo la Njiro nje kidogo ya Jiji la Arusha ziko hatarini, kutokana na kuathiriwa kwa moshi wa mitambo ya kampuni hiyo ya Marekani.
Wakazi hao zaidi ya 300 kutoka vitalu B, C na D wamekuwa wakilalamikia mitambo hiyo kwa muda mrefu na malalamiko hayo yamekwishawasilishwa katika ngazi mbalimbali za kiserikali lakini hadi sasa hakuna hatua za dhahiri zilizochukuliwa.
Symbion Power wamefunga majenereta 30 yanayotumia mafuta mazito kufua umeme ambao umeingizwa katika Gridi ya Taifa na kelele zinazotokana na jenereta hizo zimekuwa kero kwa wanafunzi wa chuo cha uhasibu ambao hosteli zao zipo jirani na eneo hilo.
Wakazi hao wanadai mitambo hiyo ya kuzalisha umeme wa megawati 66 imekuwa ikisababisha kelele nyingi, mtikisiko unaosababisha nyufa katika nyumba zao pamoja na moshi mweusi wenye kemikali zinazodaiwa kusababisha maradhi ya kifua.
Malalamiko na athari za kiafya
Mmoja wa wakazi ambao afya zao zimeathirika anatajwa kuwa ni Eline Zelothe, ambaye amelazimika kwenda kutibiwa nchini India na kufanyiwa upasuaji wa kichwa kuondoa utando wa moshi huo katika sehemu ya ubongo wake.
Akizungumza na Raia Mwema mwishoni mwa wiki iliyopita Zelothe ambaye ni mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Mkoa wa Arusha, anadai kuanza kupata matatizo ya kuumwa kichwa na kushindwa kupumua tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
"Nilitibiwa katika hospitali mbalimbali hapa nchini lakini sikupata ahueni na kutokana na hali kuwa mbaya niliomba rufaa ya kupelekwa India na Septemba 12, mwaka huu, nilifanyiwa upasuaji wa kichwa kuondoa utando wa moshi katika sehemu ya ubongo,"
"Madaktari waliniambia kuwa nimeathirika kichwani kutokana na uchafu wa moshi wenye kemikali, kwa kweli nashukuru Mungu ndugu zangu wamenisadia kunipeleka huko (India), vinginevyo sijui kama ningepona," anasema Zelothe.
Hadi sasa Zelothe ambaye alirejea nchini mwishoni mwa wiki iliyopita, bado hajapata eneo jingine la kuhamia na anaishi katika makazi yake ya awali ingawa madaktari wamemshauri kuhama eneo hilo.
Mkazi mwingine, Dominck Kabyemera, alisema hatua ya Symbion Power kupewa eneo hilo ambalo awali lilikuwa kituo cha Shirika la Umeme nchini (TANESCO), ni ukiukwaji wa sheria ya mipango miji na kuingilia uhuru wa makazi ya watu.
"Ujenzi wa mitambo hiyo mikubwa  unakwenda kinyume cha sheria za nchi kwa kuwa eneo hilo limetengwa kwa makazi ya watu, si eneo la kujenga viwanda au mitambo ya aina hiyo ambayo sasa inawanyima haki wananchi wanaoishi hapa kufurahia maisha," alieleza Kabyemera.
Alisema mitambo ya kuzalisha megawati 66 za umeme ni mradi mkubwa unaohitaji kufanyiwa tathmini ya mazingira (EIA) lakini Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) hawakufanya tathmini yoyote wakati wa kuanzisha mradi huo katika eneo hilo.
"Hii ni kinyume cha Sheria ya Hifadhi ya Mazingira  ya Mwaka 2004, namba 191, ambayo inabainisha kuwa mradi au uwekezaji wa aina hiyo unapaswa kufanyiwa tathmini ya athari za kimazingira kabla ya kuanzishwa kwake,"  alisema na kuongeza; "Wahandisi wa Kampuni ya Symbion pia wameelekeza mkondo wa maji ya mvua katika makazi ya watu, na tumekuwa tukikumbwa na mafuriko katika msimu mvua"alisema.
Kwa mujibu wa Kabyemera, wakati wa ufungaji wa mitambo hiyo, kwa niaba ya wenzake, aliandika barua ya malalamiko kwa NEMC ambayo walijibu na kukiri kuwa ni kweli hakuna tathmini ya mazingira iliyofanywa na taasisi  hiyo.
Mkazi mwingine wa eneo hilo aliyeomba jina lihifadhiwe alisema ufungaji wa mitambo hiyo umeathiri kiuchumi wakazi wa eneo hilo.
"Katika eneo hili kuna watu wamewekeza katika ujenzi wa nyumba za kisasa za kupangisha lakini tangu kufungwa kwa mitambo hiyo, wapangaji wengi wamehama kutokana na kelele pamoja na moshi mwingi na hivyo kusababisha hasara kubwa kwa wamiliki wa nyumba," alisema mkazi hiyo.
Majibu ya NEMC, Mbunge na Meya
Raia Mwema imeona nakala ya majibu ya NEMC kwa wananchi hao yenye kumbukumbu namba NEMC/513/1/VOL1/148, ambamo taasisi hiyo inakiri kuwa ni kweli mradi huo haukufanyiwa tathmini ya athari za mazingira lakini Symbion walikuwa mbioni kufanya mchakato huo.
Lakini kwa upande wake Mbunge wa Arusha, Godbless Lema, alisema hatua ya mitambo hiyo kuwekwa katika makazi ya watu haikubaliki.
"Suala hilo ni la muda mrefu, zaidi ya mwaka moja na nusu wananchi wanalalamika na hakuna hatua zinazochukuliwa. Sielewi ni kwa nini wananchi hao walipe gharama ya kupoteza uhai wao ili wananchi wengine wa Arusha wapate umeme, jambo hili halikubaliki  lazima tuchukue hatua," alisema Lema ambaye hata hivyo hakuwa tayari kuweka wazi hatua anayotarajia kuchukua.
Naye Meya wa Jiji la Arusha, Gadance Lyimo, alikiri kufahamu tatizo hilo akisema; "Niliwahi kufika pale kwa kweli hali si nzuri, kuna kelele za majenereta na mtikisiko mkubwa na mimi sikuweza kuingilia jambo hilo kwa kuwa halijafikishwa ofisini kwangu na isingependeza kushughulikia jambo ambalo halifikishwi ofisini."
Menejimenti ya Kampuni ya Symbion Power (T) Ltd hawakupatikana kuelezea malalamiko ya wananchi hao na mmoja wa maofisa wa kampuni hiyo alikataa kutoa ushirikiano kwa mwandishi wetu.
Lakini Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Felchesmi Mramba, alikiri kuwepo kwa malalamiko ya wananchi hao dhidi ya mitambo hiyo ya Symbion Power.
"Tulikwishaandikia barua kuwa wafanye marekebisho (Symbion) ili kuondoa kelele na moshi unaoalalamikiwa na wananchi wanaoishi jirani na eneo hilo, tulidhani kuwa wametekeleza," alisema Mramba.
Mkurugenzi huyo alisema hata hivyo wananchi hao wanapswa kuwa wavumilivu kwa sasa kwa kuwa mkataba wa kampuni hiyo na TANESCO unamalizika Oktoba mwakani na mitambo hiyo itaondolewa haraka eneo hilo.
Kampuni ya Symbion Power (T) Ltd imeingia mkataba wa kufua umeme na kuuza kwa TANESCO na wameweka mitambo kama hiyo jijini Dar es Salaam.
-RAIA MWEMA

Popular Post

 
Support : OBAMA | OBAMA | OBAMA
Copyright © 2013. DiraYaLeo - All Rights Reserved
Template Created by Barakaeli Aremu Published by Dira Ya Leo
Proudly powered by Blogger