BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lenye wajibu wa
kutunga, kurekebisha na hata kufuta sheria linahusika moja kwa moja katika
kuyafungia magazeti ya Mwanahalisi, Mwananchi na Mtanzania. Ndiyo, kuanzia Bunge la Pius
Msekwa ambalo lilikuwa na wajibu wa kufuta sheria 40 mbovu (ikiwamo Sheria ya
Magazeti ya Mwaka 1976) zilizopendekezwa na iliyokuwa Tume ya Rais,
iliyoongozwa na Jaji Mkuu wa zamani, Francis Nyalali.
Kuendelea kuishi kwa sheria hiyo mbovu, maana yake ni kwamba
Bunge limeridhia na pale serikali inapoitumia sheria hiyo, Bunge haliwezi
kukwepa lawama na kimsingi, kila mbunge hawezi kukwepa lawama. Kwa kuzingatia
dhana ya kiutawala ya checks
and balances, Bunge limefeli kutumia madaraka yake kuhakikisha nchi
inabaki na sheria zinazokidhi mahitaji ya wakati.
Sikubaliani na wabunge wanaoitupia lawama serikali kwa sababu tu
imetekeleza sheria hii, wote wanahusika, serikali pamoja na kila mbunge hadi pale
sheria hii itakapofutwa. Unafiki wa baadhi ya wabunge hauwezi kukubalika,
unafiki wa kuvifurahia vyombo vya habari pale vinapokidhi malengo yao kisiasa
lakini kufunga midomo yao pale vyombo hivyo vinapofungiwa kwa sheria ambayo
wanaweza kuifuta.
Kwa mwenendo huu ya kufungia vyombo vya habari wakati wowote, ni
vigumu pia kukubaliana moja kwa moja na mawazo ya Rais wa 16 wa Marekani,
Kapteni Abraham Lincoln, kijana wa Mzee Thomas na Mama Nancy, kwamba namna
pekee ya kuelekea kufutwa kwa sheria mbaya ni kuitumia sheria hiyo mbaya
kikamilifu (The best way to get a bad law repealed is to enforce it
strictly). Kwamba sheria mbaya inapotumika ndipo wengi huweza kuichukia
zaidi na hivyo shinikizo la kutaka ifutwe kuzidi na hatimaye sheria husika
kufutwa, tukitumia msemo huo, tutazidi kuumia zaidi katika suala hili la sheria
ya magazeti ya mwaka 1976.
Ni vigumu kutumia mtazamo huo ili hatimaye Sheria ya Magazeti ya
Mwaka 1976 ifutwe, sheria ambayo inaigeuza serikali kuwa mlalamikaji mwenye
kupanga na kutangaza hukumu dhidi ya magazeti. Hii ni sheria kandamizi, kuzidi
kuitumia zaidi na zaidi kama ulivyo mtazamo wa Lincoln si uungwana.
Sheria hii imekwishasababisha madhara dhidi ya wanataaluma
kadhaa wa tasnia ya habari, achilia mbali wamiliki na makundi mengine ambayo
shughuli zao za kiuchumi zinaingiliana na uwepo wa magazeti nchini. Kwa miaka
kadhaa sasa, sheria hii ya magazeti ya mwaka 1976 imelalamikiwa na kupingwa. Hata
hivyo, kwa bahati mbaya mno, watunga sheria wetu ambao wanapaswa kuwa
wawakilishi wa Watanzania, kuanzia katika majimbo yao hadi ngazi ya kitaifa,
hawaoni ubaya wa sheria hii, wamebweteka, wamekaa kimya.
Je, wabunge wetu wanafurahia sheria hii? Kama hawafurahii
wamefanya nini kuipinga? Tukianzia katika Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria-
je, kamati hii inafanya kazi yake vizuri kwa niaba ya Bunge? Katika uhai wake,
kamati hii inaweza kujivunia kufanikisha ushauri wa aliyepata kuwa Jaji Mkuu wa
Tanzania, Francis Nyalali wa kufuta sheria takriban 40 kandamizi nchini?
Je, wabunge (wasio wajumbe wa kamati ya Katiba na Sheria)
wanajua mpango kazi wa kamati hii ambayo kwa bahati nzuri orodha ya sheria
mbovu zisizofaa kuendelea kuwapo nchini ilikwishawekwa hadharani na Jaji Mkuu
Nyalali?
Kuendelea kuwapo na kutumika kwa Sheria ya Magazeti ya Mwaka
1976 maana yake ni Bunge kushindwa kufanya kazi yake vizuri katika dhana ya checks and balances. Katika
nchi yenye mgawanyo wa mihimili mitatu yenye wajibu wa kusimamiana, Bunge
limefeli. Rafu zinazofanywa na serikali kupitia sheria hii dhidi ya magazeti
zinapaswa kudhibitiwa na Bunge lakini kwa bahati mbaya, Bunge limefeli katika
eneo hili mahsusi.
Bunge ndilo linalopaswa kusukuma kuondolewa kwa sheria ya
magazeti ya mwaka 1976, na kwa hiyo, hapa mchawi wa kwanza si yule
anayetekeleza sheria inayomfaidisha, bali mchawi namba moja ni yule mwenye
uwezo wa kuizuia na hata kufutilia mbali sheria husika. Mchawi huyo ni Bunge.
Kwa watu werevu, katika sakata hili wabunge ndiyo wa kung’ang’aniwa. Serikali
haiwezi kukubali kujipunguzia nguvu zake bila kushinikizwa na chombo sahihi
ambacho ni Bunge.
Kuendelea kuwapo kwa sheria hii ni ushuhuda mwingine wa namna
ambavyo Bunge kwa ujumla wake linavyosinzia katika kutimiza wajibu wake katika
dhana ya checks and
balances. Tumuulize Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu,
anaweka mchango gani kwa nafasi yake kama mbunge? Tumuulize, Naibu Spika, Job
Ndugai, anafurahia sheria hii. Tumuulize Spika Anne Makinda, Bunge linatimiza
wajibu wake ipasavyo kwa kuendelea kuwapo kwa sheria hii?
Kuendelea kuomba huruma ya serikali katika kuifuta sheria hii ni
sawa na kutekeleza makosa mengine. Serikali haiwezi kuwa na huruma kwa kiwango
hicho cha kujipunguzia mabavu yake. Lazima tubadili mwelekeo, na kwa kweli,
mwelekeo ni katika Bunge linalopaswa kutengeneza mfumo wa sheria unaohakikisha
uwapo wa mustakabali bora wa nchi.
Kila mwananchi mpenda haki amhoji mbunge wake kama anaridhika na
sheria hii, haitoshi kuendelea kulalamika katika vipindi vya televisheni au
mikutano ya hadhara dhidi ya serikali wakati, watu wanaotambulika kama
wawakilishi wetu wapo, tuwasukume wafanye kazi yao. Hatuwezi kuendelea kusubiri
magazeti zaidi yafungiwe ili ubaya wa sheria hii uzidi kuwa dhahiri, kama ambavyo
Lincoln anavyowaza.
Bila kujali makosa au usahihi wa magazeti yaliyofungiwa, tatizo
la msingi hapa limegawanyika katika maeneo makubwa mawili. Mosi, ni Sheria ya
Magazeti ya Mwaka 1976 na pili, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, ambao ndiyo wenye jukumu la kutunga sheria na hata kufuta sheria. Ili
Bunge lisiendelee kuwa tatizo na wabunge wasionekane tatizo, wafute sheria hii.
Ujumbe pekee unaojitokeza katika uamuzi huu wa Septemba 27,
mwaka 2013 wa kulifungia gazeti la Mwananchi siku 14 na gazeti la Mtanzania
siku 90 ni kwamba, Bunge limefeli katika kutimiza wajibu wake, hasa
ikizingatiwa kwamba, tukio hili lilitanguliwa na kifungo dhidi ya gazeti la
kila wiki la Mwanahalisi. Endapo Bunge lingetimiza wajibu wake, basi, sheria
hii ingefutwa.