PAMOJA na nia njema ya Serikali ya kuhakikisha abiria wa treni ya Reli
ya Kati wanakuwa na uhakika wa kusafiri angalau mara mbili kwa wiki, imedhihirika
kuwa usafiri huo ni zaidi ya mateso kwa abiria wake.
Wengi wa abiria hao husafiri kati ya Dar es Salaam na mikoa ya Morogoro,
Dodoma, Singida, Tabora, Kigoma na hata Shinyanga na Mwanza.
Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni na gazeti hili umebaini kuwa, abiria
kwa sasa wamekuwa wanasafiri kwa mazoea na wengine kutokana na unafuu wa bei,
lakini si kwa kufurahia usafiri wa treni kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na uchakavu wa injini za treni
za abiria, ambazo hazina nguvu kiasi cha kuzifanya zisafiri kwa mwendo mdogo
hivyo mara kadhaa kuwa nje ya ratiba ya safari.
Mathalani, safari ya Dar es Salaam –Kigoma ambayo hupaswa kuchukua saa
zisizozidi 36, sasa abiria wake hulazimika kusafiri hadi saa 54. Pamoja na
uchakavu wa injini hizo ambazo vyanzo vyetu vinakiri ni `bora liende’ kutokana
na kutengenezwa zaidi ya miongo minne iliyopita, mabehewa ya abiria pia
yamechakaa.
Hali ni mbaya zaidi kwa abiria wa daraja la tatu ambao ndio wengi zaidi.
Katika madaraja yao, msongamano ni mkubwa mno, mathalani, behewa moja
linalopaswa kuchukua abiria 80 walioketi kwenye viti chakavu, huchukua hadi
abiria 200, huku wakiwa na mizigo iliyotapakaa kila sehemu.
Wapo wanaodiriki kulala chini ya viti, hivyo kuwazuia waliokaa kupata
fursa hata ya kukunja miguu. Ni nadra kwa mtu kuvuka kutoka behewa moja kwenda
jingine kutokana na msongamano, wengine wakikosa sehemu za kuweka mizigo na
hivyo kuishia kuibeba kichwani usiku na mchana.
Kwa wazoefu wa safari, pengine kwa kuijua adha hiyo, huwahi mapema
maeneo ya karibu na vyoo na kuijaza mizigo yao huku wenyewe wakipiga kambi
hapo.
Gazeti hili lililolazimika kufunga safari kutoka Dar es Salaam hadi
Kigoma ili kushuhudia adha na raha za usafiri wa treni kwa Reli ya Kati,
ulibaini kuwa hali ya msongamano ambayo si rafiki ni shubiri zaidi kutokana na
joto kali ndani ya mabehewa ambayo feni zake za juu zimechakaa kiasi cha
kutofanya kazi.
Tatizo la vyoo Aidha, kwa upande wa daraja la tatu, matumizi ya vyoo ni
anasa kwani hakuna huduma ya maji, hali inayochangia kuwapo kwa uchafuzi mkubwa
wa mazingira wakati wa usafiri.
Nafuu hupatikana katika vituo vikubwa, mfano Morogoro na Tabora ambayo
kutokana na treni kusimama kwa kati ya saa moja na mawili, abiria hukimbilia
kujisaidia au kuoga katika vyoo na mabafu ya kulipia katika maeneo hayo.
Kwa ujumla, safari kati ya Dar es Salaam na Kigoma ina vituo vikubwa na
vidogo jumla ya 85. Haishangazi kuona abiria walioshuka kwenye treni wakiwa
katika foleni za kulipia Sh 200 ili kuingia chooni, na wengine Sh 400 ili
kupata nafasi ya kuoga.
Kuna huduma ya sehemu ya kupiga mswaki, kunawa uso ambazo ni rahisi,
kwani mtejwa hutozwa Sh 100. Kwa abiria wa madaraja ya kwanza na pili, kwa
kiasi fulani wana nafuu ya vyoo vyao kuwa na maji, ingawa vinaandamwa na hali
ya uchafu.
Huko nako, kuoga ni mara chache kwani hali ya uchafu bado ipo. Hawa kwa
kuwa wana nafasi, wanaweza kupiga mswaki na kunawa uso bila ya kulazimika
kupanga foleni treni inapokuwa imesimama.
Tishio la wizi pamoja na mateso ya msongamano, ukosefu wa huduma kama za
vyoo na pia hali ya joto, mateso mengine kwa abiria yanatokana na tishio la
wizi.
Wakati wote, abiria huwa macho kwa hofu ya kuibiwa kutokana na kushamiri
kwa matukio ya aina hiyo. Mmoja wa maofisa wa Kikosi cha Polisi Reli ambaye
hakutaka kutajwa jina gazetini, aliliambia gazeti hili kuwa ni vyema kuchukua
tahadhari hasa unapokuwa daraja la tatu.
“Hali ni mbaya sana, usione ule msongamano, wengine wanafurahia kwa
sababu wapo kazini. Wanaibiana sana, ndiyo maana hata nyakati za usiku abiria
hawalali hovyo kila mmoja akimhofia mwenzake,” alisema na kudai hali huwa mbaya
nyakati za usiku kutokana na wezi wa vituo vya njiani kupanda juu ya mabehewa
na kukwapua mali za abiria.
Anavitaja vituo vya kati ya Kidete na Morogoro, Saranda na Tabora na
maeneo ya Uvinza hadi Kigoma kuwa ni tishio mno kwa staili hiyo ya wizi wa
kupanda juu ya mabehewa nyakati za usiku.
“Usiku lazima ufunge madirisha, ukishangaa utaibiwa kila kitu, kuanzia
simu, laptop (kompyuta ndogo) na hata mabegi kwa akinamama. Jamaa ni wepesi sana,”
anazidi kusimulia.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia mmoja wa wezi akinaswa baada
kuingia ndani ya treni kwa lengo la kuiba akitokea juu ya behewa, lakini
akajikuta akiangukia mikononi mwa polisi waliovaa kiraia.
Ilikuwa usiku wa saa 4:00 katika eneo la Nguruka, wilayani Uvinza,
Kigoma. “Unamwona huyu, ni miongoni mwa vijana hatari sana wanaosumbua abiria
nyakati za usiku. Wanatumia zaidi ushirikina ili wasinaswe, lakini safari hii
amefika. Tunakwenda naye mpaka Kigoma mjini akaozee polisi,” anasema ofisa
mwingine.
Na kweli, mpaka treni inafikia mwisho wa reli Kigoma baada ya safari ya
saa 54 kutoka Dar es Salaam, kijana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Ayoub,
alikuwa mikononi mwa polisi.
Baadhi ya abiria waliozungumza na gazeti hili wakiwa safarini walisema
kuwa kwa abiria wa Kigoma hawana njia nyingine ya kukabiliana na hali hiyo
kutokana na ukweli kwamba, ndio usafiri pekee nafuu na wa kuaminika kwenda ama
kutoka mkoani humo.
Ingawa kuna usafiri wa mabasi machache yanayofanya safari kati ya Dar es
Salaam na Kigoma, nauli zake ziko juu, kati ya Sh 65,000 na 75,000, wakati kwa
abiria wa treni hulazimika kulipa Sh 27,700 kusafiri umbali wa kilomita zaidi
ya 1,254 uliopo baina ya mikoa hiyo.
“Ni usafiri nafuu kwa walio wengi, ndiyo maana pamoja na hofu ya
kutofika kwa wakati na adha nyingine za safarini, inasaidia. Hata hivyo nadhani
Serikali inapaswa kutupia macho hali hii, ni mateso kwa kweli,” alisema Gilbert
Kaliza, mmoja wa wafanyabiashara anayetumia mara kwa mara usafiri huo
kusafirisha bidhaa zake.
Pamoja na adha hizo, hali ya reli si nzuri, kwani nayo imechoka kiasi
cha kuangusha mara kwa mara vichwa au injini za mabehewa ya mizigo, hali
inayosababisha treni za abiria kucheleweshwa mara kwa mara ili kupisha behewa
au kichwa cha treni kilichoanguka kiondolewe.
Mbali na adha hizo, pia inaponyesha mvua mabehewa yanavuja na watu
kujikuta wakiloana ambapo mfano wa karibu ni juzi treni ilivyokuwa ikitoka
Kigoma kuelekea Dar es Salaam ambapo watu walijikuta wakijikinga na mvua na
wengine wakiloana.
Vilevile usafiri huo umekuwa na kero ya kujaa kunguni ambapo kwenye
mabehewa ya daraja la pili ambayo yanatarajiwa kuwa na usafi yamejaa kunguni.
Masta Mkuu wa Shirika la Reli nchini (TRL) mkoani Kigoma, Ally Zunda
hakuwa tayari kuzungumzia lolote juu ya matatizo husika, akisema wasemaji wapo
makao makuu ya shirika jijini Dar es Salaam.
Alipotafutwa kwa njia ya simu, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe
na Meneja Uhusiano wa TRL. Midladj Maez hawakupatikana.
Hata hivyo, Serikali imekuwa ikisisitiza kuwa, inatafuta tiba ya kudumu
juu ya uchakavu wa injini, mabehewa na njia ya reli ili kuufanya usafiri wa
treni kuwa tegemeo la wengi zaidi mikoani inayotumia usafiri huo.-habarileo