muhtasari

Home » , » MATAPELI SASA KUPITIA MAKANISANI...

MATAPELI SASA KUPITIA MAKANISANI...



·  
KUMEIBUKA matapeli wanaotumia makanisa kuwaibia watu fedha kwa kuwadanganya kuwa fedha zao zitaombewa na kupata mara tatu zaidi ya kiwango walichonacho, pamoja na zawadi ya madini.
Aidha baadhi ya makanisa likiwemo Kanisa Katoliki na baadhi ya makanisa ya Pentekoste mkoani Pwani na jijini Dar es Salaam, yamejikuta yakitumiwa kwa utapeli huo na waliotapeliwa kuachwa wakilia nje ya milango ya makanisa hayo.
Mkoani Dar es Salaam, gazeti hili limebaini kuwepo kwa utapeli huo ambapo baadhi ya watu katika maeneo ya Buguruni walitapeliwa kwa nyakati tofauti katika kipindi cha miaka miwili sasa kwa kuelezwa na matapeli hao wanaodaiwa kuwa na dawa za kuwapumbaza akili, wawape fedha ili wakaziombee.
“Zaidi ya watu 20 walitapeliwa Dar es Salaam mwaka jana, wanafuatiliwa na matapeli wakitoka ama benki, au kwenye mitandao ya simu kutoa fedha, wanaingizwa mjini kuwa fedha zao zitayeyuka ikiwa hawataziombea. “Wanapelekwa mpaka kanisani na wanarubuniwa kwamba mchungaji ataziombea na mwenye fedha atapokea kutoka kwa Mungu, mara mbili ya fedha hizo baada ya siku kadhaa, kumbe ndio katapeliwa hivyo,” alieleza polisi mmoja wa kituo cha Buguruni ambaye hakutaka jina liandikwe gazetini kwa kuwa si msemaji.
Hivi karibuni, tukio kama hilo limebainika kuibuka kwa kasi mkoani Pwani, ambako watu takribani 10 wanaelezwa kutapeliwa fedha kati ya Sh 300,000 hadi milioni moja kila mmoja baada ya kutakiwa na matapeli kuwapatia fedha hizo ili wazipeleke kanisani kuombewa na baada ya siku moja, watapokea mara tatu na zawadi ya madini ya dhahabu (jiwe moja).
Inadaiwa makanisa kadhaa yamekumbwa na hili mkoani humo likiwemo Kanisa Katoliki ambapo katika Parokia ya Mtakatifu Don Bosco, Kibaha- Tumbi, zaidi ya watu wanne kati ya zaidi ya 10 wanaodaiwa kutapeliwa, walilizwa kupitia kanisa hilo.
Paroko Msaidizi wa Parokia hiyo, Padri Romwadi Mkandala akihubiri katika Misa ya kumuombea marehemu Sabina Nandi (92) katika Kijiji cha Boko-Timiza, Kibaha mkoani Pwani wiki moja iliyopita, alitoa tahadhari kwa waumini na wakazi wa Kibaha kuwa macho kutokana na kuibuka kwa utapeli huo.
“Tena kabla sijaendelea sana, jamani nyie watu mnaopenda fedha za bure bure, muwe macho, kuna matapeli wameibuka hapa Kibaha Tumbi, mtalizwa? Hivi kwa usawa huu nani akupe fedha za bure? “Kuna watu wanadanganya fedha zinaombewa na mapadri kanisani kwetu, nasema hakuna kitu kama hicho, watu wamelizwa karibia 10, narudia tena hakuna kanisa wala msikiti utaombea pesa zako ziongezeke mara tatu kimiujiza, huo ni uvivu na wengi mtatapeliwa msipokuwa macho,” alisema Padri Mkandala.
Akifafanua alisema hivi karibuni, watu wawili kila mmoja kwa wakati wake, walikutwa nje ya lango la kanisa hilo wakilia na kuhamaki baada ya kubaini kuwa wamelizwa kiasi kikubwa cha fedha na matapeli hao.
Wengine walishawahi kukutwa lakini hawakuwa tayari kujieleza kutapeliwa. Akielezea wanavyofanya, Padri Mkandala alisema kwa mujibu wa watu waliowahoji baada ya kuwakuta nje ya lango la kanisa wakilia, walieleza kuwa matapeli hao wanajipanga kuanzia katika vibanda vya kutolea fedha vya mitandao ya simu, ama katika benki na wakishajua kiasi cha fedha walichonacho huwafuatilia na kuanza kuwatapeli.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alipoulizwa kuhusu utapeli huo, alisema hakuna kesi iliyoripotiwa na kuelezea huenda wahusika wanaogopa kuripoti Polisi kutokana na mazingira ya kizembe ya kutapeliwa kwao.
“Tumejaribu kufuatilia matukio ya wiki chache zilizopita hapa kwetu, tumekosa kabisa matukio ya aina hiyo, huenda wahusika wanadai wameripoti kwetu lakini wanaogopa kuja maana ni uzembe gani huo wa kutapeliwa namna hiyo katika maisha ya leo, watu wanapenda fedha zisizo na jasho.

Popular Post

 
Support : OBAMA | OBAMA | OBAMA
Copyright © 2013. DiraYaLeo - All Rights Reserved
Template Created by Barakaeli Aremu Published by Dira Ya Leo
Proudly powered by Blogger