SIKU chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwataka
Watanzania kujiandaa na uvamizi wa kigaidi, vijana 11 wenye umri kati ya miaka
18 na 39, wametiwa mbaroni mkoani Mtwara, wakidaiwa kuwa katika mafunzo ya
kijeshi msituni, yaliyotajwa kuwa ya kutisha na hatari.
Vijana hao wanadaiwa kukutwa katika mlima wa
Makolionga wilayani Nanyumbu, wakiwa katika maficho wakitumia CD zipatazo 25
zenye mafunzo mbali mbali. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen
alielezea tukio hilo kuwa si la kawaida na kutaja aina ya CD zilizokuwa
zikitumika.
Kwa mujibu wa Zelothe, CD hizo zilihusu Al -Shabaab,
mauaji ya Osama bin Laden, Zindukeni Zanzibar, kuandaa majeshi, mauaji ya Idd
Amin na Mogadishu sniper.
“Pamoja na CD hizo, watuhumiwa walikuwa na zana
nyingine na vyakula,” alisema.
Alitaja zana hizo ni DVD player moja, Solar panel moja
yenye wati 30, mapanga mawili, visu viwili, tochi moja na betri ya pikipiki
namba 12. Pia, wanatuhumiwa walikutwa na simu tano za viganjani, vyombo
mbalimbali vya chakula, jiko la mkaa, jiko la mafuta ya taa, taa ya chemli,
baiskeli tatu, ndoo nne za maji na vitabu vya dini ya Kiislamu.
Vitu vingine walivyokutwa navyo ni unga wa mahindi
kilogramu 50, mbaazi kiroba kimoja chenye kilogramu 50, mahindi viroba vitatu
sawa na kilogramu 150, virago vya kulalia na mfuko wa kijani, unaosadikiwa ni
wa kijeshi wenye nembo ya nanga ya meli yenye mistari kulia na kushoto na nyoka
katikati.
Kamanda Zelothe alitaja waliokamatwa kuwa ni Mohamed
Matete (39), mkazi wa kijiji cha Sengenye ambaye anadaiwa kuwa kiongozi wa
kundi hilo na Hassan Omary, maarufu kama Ajili (39), mkazi wa Nalunyu.
Wengine ambao wote ni wakazi wa Likokona ni Rashidi
Ismail (27), Abdallah Hamis (32), Salum Bakari maarufu Wadi (38), Ramadhan
Rajabu (26), Fadhil Rajabu (20), Abbas Muhdini (32), Ismaili Chande (18), Said
Mawazo (21) na Issa Abed mwenye umri wa miaka 21.
“Watuhumiwa hao wote tayari wamefikishwa mahakamani na
wakati huo Polisi mkoani hapa inaendelea na upelelezi wa kina kuhusu tukio hili
ambalo si la kawaida.
“Tunasaidiwa na Makao Makuu ya Polisi pamoja na
kushirikisha mikoa mingine kuwanasa watu wote ambao wanatajwa kuhusishwa na
tukio hilo la mafunzo ya kutisha na hatari,” alisema Zelothe katika taarifa
yake kwa vyombo vya habari.
Jeshi la Polisi limetoa rai kwa wananchi wote wenye
taarifa, inayohusu tukio la aina hiyo, watoe taarifa mapema iwezekanavyo ili
watu hao wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake.
-HABARILEO