IKULU imekanusha taarifa zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii jana
ikidai kuwa Rais Jakaya Kikwete ametia saini muswada wa sheria ya
marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya Katiba ambao ulipitishwa na Bunge.
Taarifa iliyotolewa jana jioni na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu, ilieleza mambo manne kufafanua hatua za muswada huo kusainiwa na
Rais Kikwete utakapomfikia.
Ilisema kuwa Ofisi ya Rais, Ikulu, haijapokea muswada huo kwamba
inawezekana umekwishakutumwa kutoka bungeni lakini haujamfikia Rais, hivyo
kama haujamfikia hawezi akawa ameutia saini.
Pili, muswada huo ukimfikia inatarajiwa kuwa atautia saini kwa sababu
umepitia katika mchakato sahihi na halali wa kikatiba kwa maana ya
kufikishwa bungeni na serikali, kujadiliwa na hatimaye kupitishwa na Bunge.
Tatu, kama yapo marekebisho ambayo yanaonekana yanafaa kufanywa katika
sheria hiyo, basi yatafanywa na Bunge baada ya Rais kuwa ametimiza matakwa
ya kikatiba ya kutia saini muswada ambao umepitishwa na Bunge, ilisema
taarifa hiyo.
Katika sababu ya nne Ikulu ilisema kuwa hii haitakuwa mara ya kwanza kwa
sheria kupitishwa na Bunge, ikatiwa saini na Rais na baadaye kufanyiwa
marekebisho na Bunge baada ya kuonekana umuhimu wa kufanya marekebisho
hayo.
Katika hatua nyingine, Ikulu imeanza mawasiliano na viongozi wa vyama
vya siasa nchini vyenye hoja kuhusu muswada huo kwa nia ya kuandaa mkutano
kati yao na Rais Kikwete.
Taarifa ilisema kuwa mawasiliano hayo yalianza jana kufuatia maelekezo
ya Rais Kikwete kwa Ofisi ya Katibu wa Rais.
Kufuatia matukio yaliyotokea bungeni wakati wa kujadiliwa na kupitishwa
kwa muswada huo na kauli mbalimbali za wabunge wa vyama vya upinzani na
wadau wengine, Rais Kikwete alisema kuwa hoja na kauli za wanaopinga
muswada huo zinazungumzika kwa nia njema ya kutafuta mwafaka katika
mchakato wa kutafuta Katiba mpya.
Kwa mujibu wa maandalizi hayo, Ofisi ya Rais, Ikulu, inaangalia
uwezekano wa kuitisha mkutano huo Jumapili ya Oktoba 13 au Jumanne ya
Oktoba 15, mwaka huu, ilisema taarifa hiyo.
Hofu ya wengi
Kufuatia kuzagaa kwa taarifa hiyo, matumaini ya wengi yaliyeyuka baada
ya ratiba ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kutoonyesha jambo
hilo kama linarudi bungeni.
Wadau wengi walitumaini kuwa Rais Jakaya Kikwete asingeusaini muswada
huo, kufuatia kauli yake ya kuwataka viongozi wa vyama vya CHADEMA, CUF na
NCCR-Mageuzi waachane na maandamano ya kuupinga na badala yake waketi na
kujadiliana na serikali.
Akizungumza juzi na waandishi wa habari, Lissu ambaye ni mnadhimu wa
kambi ya upinzani bungeni, alisema kuwa busara ya Rais kutaka mjadala na
wapinzani ingeonekana jana kwenye ratiba ya kamati.
Alisema kama Rais hajausaini muswada huo, ratiba ya Kamati ya Bunge
ilipaswa kuonyesha kuwa sasa unarudishwa bungeni kufanyiwa marekebisho ya
kasoro zinazolalamikiwa.
Hata hivyo, jana ratiba hiyo iliyotolewa kwa wajumbe wa kamati hiyo,
haikuonyesha jambo lolote kuhusu muswada huo unaopigiwa kelele, jambo
lililozua hisia kuwa umeishatiwa saini na Rais.
Lissu alisema licha ya Rais Kikwete kusema jambo hilo linazungumzika,
sasa amemaanisha kuwa hana nia ya kutosaini muswada huo wenye mapungufu
mengi.
Katika ratiba ya kamati ambayo Tanzania Daima imefanikiwa kupata nakala
yake, wajumbe wake sasa wamepangiwa ratiba ya siku tatu kuanzia Oktoba 9
hadi 12 kwenda Zanzibar kukusanya maoni ya wadau kuhusu miswada ya sheria
ya kura za maoni 2013 na sheria ya mbadiliko ya sheria mbalimbali ya mwaka
2013.
Mbowe afunguka
Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe, amesema kuwa
Kikwete amemkosea Tundu Lissu kwa kumuita mwongo, mzushi, mfitini na
mzandiki na kwamba anapaswa kumwomba radhi.
Akifungua semina ya siku tatu ya mafunzo ya wakufunzi wa kanda za
CHADEMA jana jijini Dar es Salaam, Mbowe alimtahadharisha Rais Kikwete kuwa
makini na suala la Katiba kwani ni roho ya nchi.
Alisema Katiba ni sheria mama na suala linaloweza kulete mpasuko, hivyo
anapolizungumzia awe amejiridhisha kuliko kutegemea maneno ya kuambiwa,
kufahamishwa, kuelezwa na washauri wake ambao wamekuwa wakimshauri vibaya
na wakati mwingine kumdanganya.
Rais awe makini na kauli zake kabla ya kuzungumza na Watanzania na
atumie fursa hiyo kujiridhisha na katika suala la Katiba asifanye utani,
alisema.
Alisema kuwa katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi, Rais Kikwete
ametangaza uhasama binafsi na Lissu kutokana na hotuba aliyotoa bungeni.
Mbowe alisema Rais amemwonea Lissu na kwamba hata mkubwa akikosea huomba
radhi, hivyo katika hilo anapaswa amwombe Lissu radhi.
Lissu alikuwa akitimiza wajibu wa kibunge, alifanya hayo kwa mujibu wa
kanuni za Bunge na alikuwa anawakilisha maoni ya kambi ya upinzani.
Nashindwa kuelewa kwa nini Rais hakuelewa hili na maneno aliyotumia sio
maneno ambayo Rais anapaswa kuyatumia anapohutubia wananchi, alisema.
Aliongeza kuwa inashangaza kuona Rais Kikwete hana utamaduni wa kujisomea,
kwamba asingesema mjadala wa bungeni ulienda vizuri bila kusoma kumbukumbu
za Bunge (Hansard) au kuangalia mikanda iliyorekodiwa.
Amezingatia ushauri wa mawaziri wake, kukubali hata mambo ambayo
yamechomekwa katika muswada ulioletwa bungeni, alisema Mbowe.
Mapema akifungua semina hiyo, alisema CHADEMA imetambua vipaji
mbalimbali katika ngazi za uongozi, hivyo imegatua madaraka kupeleka kwenye
kanda badala ya mamlaka yote kutolewa na makao makuu.
Aliongeza kwamba mkakati uliopo sasa wa CHADEMA ni kuifanya kuwa ya
kidijitali (cha kisasa) katika maana kuwa wakufunzi wapya wataendesha chama
kitaalamu.
Wadau wanena
Wadau mbalimbali wamepokea kwa mitazamo tofauti hotuba ya mwisho wa
mwezi ya Rais Kikwete ambayo imeonyesha mgawanyiko juu ya mchakato wa Katiba
unapoelekea.
Wakizungumza na Tanzania Daima jana kwa nyakati tofauti, wadau hao
walisema kuwa tangu kuanza kwa mchakato huo umekuwa na dosari, hatua
inayoashiria kuwa kuna uwezekano wa kushindwa kuafikiana.
Mhadhiri wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Bashiru Ally, alisema kuwa ni wazi kuwa mchakato huo unaashiria kushindwa
kupatikana kwa muafaka.
Alisema kuwa mchakato huo umevamiwa na wanasiasa na wameuathiri hivyo
itakuwa ndoto kupata Katiba iliyo ya Watanzania.
Mjadala huu umeingia dosari tangu mwanzo kuanzia kutungwa kwa sheria
yenyewe na hata kuundwa kwa tume ambayo ina sura za mgawanyiko kwani wale
waliopo kila mmoja ana maslai yake binafsi na sio tume ya kitaifa,
alisema.
Mhadhiri huyo alisema kuwa Katiba inatungwa kwa kuketi chini na
kujadiliana na sio kama inavyotokea ambapo wanasiasa wamebadili muelekeo na
kuitana majina ya wanafiki na wazandiki, jambo ambalo linaashiria
kutokuamiana.
Naye mhadhiri mstaafu wa chuo hicho, Dk. Azavel Lwaitama, alisema kuwa
lugha aliyotumia Rais Kikwete inaonyesha kuwa ni wa kundi la Chama cha
Mapinduzi (CCM).
Alisema kuwa Rais ameonyesha nia ya kutaka kusaini muswada huo na hilo
linaashiria kuwa Katiba itakayopatikana itakuwa ni ya CCM.
Kama Rais Kikwete kaonyesha nia ya kutaka mchakato uendelee na asaini
huo mswada basi hakuna haja ya kukutana na wapinzani kama anavyotaka;
itakuwa ni sawa na kupoteza muda tu na wala haja ya kurudisha bungeni,
alisema.
Mkurugenzi wa Mawasiliano, Habari na Haki za Binadamu wa CUF Zanzibar,
Salum Bimani, alisema kuwa kama hotuba ya Rais Kikwete itaweza kutekelezwa
kuna uwezekano wa kupatikana kwa Katiba ya Watanzania
-tanzania daima
|
|
|