Mwanafunzi wa darasa la tano wa shule ya msingi Pandani kisiwani Pemba, Asha Hamad Khalfan (13), ameathirika macho na kichwa baada ya kudaiwa kupewa dawa aina tatu tofauti na mwalimu wake ikiwemo ya kichocho, matende na malaria bila kanuni za matibabu kuzingatiwa.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili, baba wa mwanafunzi huyo Hamad Khalfan, alisema :
“Alianza kupata homa kali mara baada ya kunyweshwa
dawa hizo zikiwemo dawa za mabusha na matende, kichocho na malaria. Kwa
mujibu wa maelezo yake, alipewa na mwalimu wake shuleni.”
Hamad alisema kinachomshangaza ni mtoto wake kupewa dawa hizo na mwalimu wake badala ya mtaalamu wa afya na tiba.
Alisema kwamba mtoto wake amevimba macho na sehemu
ya kichwa kulegea na kuwa mithili ya kichwa cha mtoto mchanga na
alilazwa katika Hospitali ya Wete kwa siku 12 kabla ya kuhamishiwa
katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja baada ya hali yake kuzidi kuwa
mbaya.
Katibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja mjini
Unguja, Hassan Makame alithibitisha kumpokelewa mgonjwa huyo, alikanusha
kukupewa dawa aina tatu kwa wakati mmoja .
Waziri wa Afya wa SMZ Juma Duni Haji alisema kwa
mujibu wa kanuni za afya, dawa za aina yoyote ikiwemo ya chanjo hutakiwa
kutolewa na Ofisa wa Afya mhusika.