muhtasari

Home » , » MBUNGE CCM ACHARUKA: PINDA MZIGO NAMBA WANI... • ASEMA ASIPOONDOLEWA CCM ITANG’OKA...

MBUNGE CCM ACHARUKA: PINDA MZIGO NAMBA WANI... • ASEMA ASIPOONDOLEWA CCM ITANG’OKA...

Kangi Lugola
SAKATA la mawaziri kuandamwa kwa kutowajibika limezidi kushika kasi ambapo safari hii, Rais Jakaya Kikwete ametakiwa kumfukuza kazi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa madai ya kuwa mchawi wa maendeleo ya nchi na mzigo namba moja.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia naye anadaiwa kuwa mzigo mwingine kwa taifa kutokana na kubariki ufisadi katika wizara yake.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) alipokuwa akichangia katika hoja mbalimbali kuhusu kamati tatu za Bunge zilizowasilishwa bungeni juzi.
Kamati zilizowasilisha hoja zao ni ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Kamati ya Bajeti na Kamati ya Hesabu za Serikali.
Lugola alisema kama Rais Kikwete asipowafukuza kazi Pinda na Ghasia, CCM itakuwa shakani kurejea madarakani katika uchaguzi mkuu mwaka 2015.
“Mimi nawashangaa wabunge wenzangu mnaosimama hapa na kutumia nguvu zenu nyingi kuishauri serikali… hii serikali inayoongozwa na chama changu haishauriki, kwa kipindi kirefu ina watu wasiojua majukumu yao.
“Ni ngumu kuishauri serikali kutokana na kuwa na mawaziri wasiojua majukumu yao, kwa kutojua wanachokifanya wameamua kutohudhuria vikao muhimu vya kujadili taarifa za kamati,” alisema.
Lugola alisema katika kikao cha jana, mawaziri sita na manaibu wawili ndio waliohudhuria, hivyo waliobaki kukosa fursa ya kusikiliza michango mbalimbali inayotolewa na wabunge.
“Mimi ni mbunge wa CCM, na pengine haya ninayotaka kuyasema yanaweza yasiwapendeze wabunge wenzangu wa CCM, lakini ndivyo nilivyo, ndivyo Mungu alivyoniumba, naomba wanisamehe. Nchi nyingine katika Bunge Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anapowasilisha taarifa, ndiyo wakati nchi nzima masikio ya watu yanakuwa bungeni, lakini kwetu ni tofauti,” alisema.
Wakati Lugola akichangia bungeni, walikuwepo mawaziri wanne tu na manaibu wawili, huku nafasi za mawaziri zikiwa wazi.
Waliokuwepo bungeni ni Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, Hawa Ghasia, Sofia Simba, Shamsi Vuai Nahodha, Mhandisi Charles Kitwanga na Janet Mbene.
“Lakini cha kushangaza kuanzia jana Waziri Mkuu ameenda kuhudhuria mahafali wakati jambo muhimu kama hili linazungumzwa bungeni. Hata hivyo pamoja na kuwa mheshimiwa spika jana (Juzi ) uliwatetea mawaziri kuwa walikuomba ruhusa, lakini mimi hainiingii akilini kuwa waliomba ruhusa mawaziri wote na kubaki mawaziri wanne na manaibu wawili,” alisema Lugola.
Alibainisha kuwa kwa busara za kawaida spika asingekubali kuwaruhusu mawaziri hao wakati kuna jambo la muhimu  linajadiliwa kwa mustakabali wa taifa na watu wake.
Lugola alisema TAMISEMI ina mtandao mkubwa wa utumiaji wa fedha ambao hauwezi kuwatenganisha Waziri Mkuu na Waziri Ghasia ambapo asilimia 70 ya fedha za bajeti hupelekwa huko.
Alisema kuwa licha ya wizara hiyo kutengewa fedha nyingi, bado serikali imekuwa ikisuasua kushughulikia masuala mbalimbali ya wananchi wa kipato cha chini.
Lugola aliwataka wabunge wasiendelee kuwasaliti Watanzania kwa kubariki ufisadi unaofanywa na viongozi wa TAMISEMI inayoongozwa na Waziri Mkuu, Pinda.
Alibainisha kuwa kwa sasa serikali haishauriki, na jambo hilo linaonekana wazi kwakuwa imeendelea kulipa mishahara hewa kwa waliofariki, huku Watanzania wakiteseka kwa umaskini.
Lugola aliongeza kuwa serikali imekuwa ikibariki ununuzi usiokuwa na nyaraka jambo ambalo ni wizi, lakini unalindwa na viongozi.
“Mchawi wetu katika maendeleo serikalini, tatizo kubwa ni Waziri Mkuu amekuwa mpole mno, hawajibiki…, matatizo yanatokea ndani ya nchi yupo wapi? Wananchi Mwibara umaskini unakithiri, fedha zinaliwa ambazo zingewapa madawati, watu wangepata madawati na maji, wangevua kwa uvuvi wa kisasa, Waziri Mkuu, jamani nakulilia huko wapi uwajibikaji wako ndani ya serikali?” alisema.
Naye Mbunge wa Musoma Mjini, Vicent Nyerere (CHADEMA), alisema serikali imeshindwa kufanya kazi, hivyo ni vema Watanzania wakafanya uamuzi wa kuiondoa madarakani kwa kutumia sanduku la kura.
Alisema kinachoonekana kwa Serikali ya CCM ni kubariki ufisadi kutokana na viongozi waliopo madarakani kushindwa kuwawajibisha wanaobainika kufanya ufisadi kwa sababu ya kulindana.
Nyerere alisema aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Moringe Sokoine, alikuwa na uwezo wa kuwawajibisha waliobainika kufanya ubadhirifu wa mali za umma.
“Hapa serikali mnaweza kujipima kuwa hata nyinyi wenyewe mmeishajikatia tamaa kutokana na kukosa huduma za kiafya na ndiyo maana hata alipotokea babu wa Loliondo viongozi wote mlikimbilia huko kwenda kupata kikombe,” alisema Nyerere.
Katika mjadala huo ambao umeibua hisia kali kwa wabunge, ambao kwa asilimia kubwa wamekuwa wakilalama kuwa TAMISEMI kuna ufisadi mkubwa ambao unafanyika huku serikali ikiwa imenyamaza kimya.
Katika mjadala huo wabunge walikuwa wakihoji sababu za watendaji wanaotuhumiwa kufanya ubadhirifu kuhamishwa vituo vyao vya kazi badala ya kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Mara kwa mara wabunge na viongozi wa CCM wamekuwa wakiwalalamikia mawaziri kwa kushindwa kuwajibika, hivyo kuisababisha serikali kuchukiwa na wananchi.
Wiki mbili zilizopita Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikaririwa akiwataja mawaziri wanne ambao wanatakiwa kutoa majibu ya uwajibikaji wao kwenye Kikao cha Kamati Kuu (CC) ya chama hicho kinachotarajia kufanyika wakati wowote kuanzia sasa.
Nape aliwataja mawaziri hao kuwa ni Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, naibu wake Adam Malima, Waziri wa Uvuvi na Mifugo, David Mathayo na Waziri wa Maji, Jumanne Maghembe.
-tanzania daima

Popular Post

 
Support : OBAMA | OBAMA | OBAMA
Copyright © 2013. DiraYaLeo - All Rights Reserved
Template Created by Barakaeli Aremu Published by Dira Ya Leo
Proudly powered by Blogger